Zanzibar yaridhia chanjo ya Corona

WAKATI wowote kuanzia sasa, Zanzibar itaanza kupokea chanjo dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona, baada ya serikali kuridhia matumizi yake.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Ikulu ya Zanzibar na baadhi ya maofisa wa juu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto zinaeleza kuwa mipango ya kuwasili kwa chanjo hizo imekamilika.

Hata hivyo, vyanzo hivyo havikuwa tayari kuweka bayana ni chanjo aina gani na kutoka nchi ipi, zitawasilishwa visiwani humo kwa ajili ya kuanza zoezi la kutoa chanjo kwa wananchi ili kujikingana COVID-19.

Mmoja wa washauri wa Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuhusu masuala ya afya, amekiri kufikia hatua nzuri ya kuletwa kwa chanjo hizo Zanzibar na kwamba mipango inakamilishwa ili kutangazia umma juu ya uamuzi rasmi wa serikali.

“Tuko katika hatua nzuri,  hivi punde mtaona shehena ya chanjo hizo ikitua Zanzibar na wananchi wakae tayari kupokea na kuchanjwa,” daktari huyo ameiambia SAUTI KUBWA kwa sharti la kutotajwa majina.

Mmoja wa wakurugenzi wa idara ya afya Zanzibar amethibitisha kuwepo kwa hatua chache kabla ya chanjo hizo hazijaanza kuwasili visiwani humo.

Amesema kuwa Serikali ya Zanzibar, kupitia wizara ya afya, imekamilisha uchunguzi wake na kubaini kwamba chanjo hizo ni salama kwa matumizi ya binadamu.

“Sasa tuko tayari kuanza kutoa chanjo na wizara yetu itatoa utaratibu mzuri wa kuchanja watu etu ilikujikinga na ugonjwa wa Corona ambao umekuwa tishio kubwa duniani,” ameongeza mtaalamu huyo wa afya.

Tayari Rais wa Zanzibar Dk. Mwinyi ameeleza utayari wa Zanzibar kupokea na kuanza kutoa chanjo dhidi ya Corona.

Juzi akiwa katika ziara ya kushukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Mjini Unguja, Dk. Mwinyi alisema Zanzibar itapokea chanjo na kwamba wananchi watakaokuwa tayari watachanjwa.

Alisema serikali haitalazimisha wananchi wake kupata chanjo kwani ni hiari kwa kila mtu kuchanjwa au kukataa.

Hata hivyo alitahadharisha kwamba dunia nzima sasa inahimiza wananchi wake kupata chanjo ili kujikinga dhidi ya COVID-19 na kwamba baadhi ya nchi zimeweka utaratibu wa kutopokea wageni wasiokuwa na chanjo hiyo.
“Kwa wale wanaojiandaa kwenda Hijja, watambue kwamba huwezi kuingia Saudia kama hujapata chanjo, sasa ni hiari ya kila mmoja kuamua na hakua atakayelazimishwa,” alionya Rais Dk. Mwinyi.

 Hadi sasa chanjo ambazo zinasambazwa bure kwa nchi masikini, kupitia utaratibu maalum wa Shirika a Afya Duniani (WHO) maarufu kwa jina la Covax, ni pamoja na Chanjo ya Pfizer-BioNTech – kutoka Marekani (inayotolewa kwa dozi mbili; baada ya siku 21 kutoka kupata ya kwanza); chanjo ya Moderna – kutoka Marekani yenye dozi mbili (ya pili baada ya siku 28) na chanjo ya Johnson & Johnson – kutoka marekani na Uholanzi yenye dozi moja tu.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, haijaweka bayana kuanza kupokea chanjo hizo, licha ya kuonyesha utayari wa kukubali na kuridhia matumizi yake kwa binadamu.

Msimamo huo wa serikali ya sasa ni kinyume na mtazamo wa Rais John Magufuli aliyeamini kutofanya kazi vyema kwa chanjo hizo, huku awali akipinga kuwepo kwa Corona nchini mwake. Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 kwa ugonjwa unaoelezwa na baadhi ya vyanzo kuwa ni Corona, ingawa serikali ilieleza chanzo cha kifo kuwa matatizo ya moyo kwa muda mrefu.

Like