Staha Bungeni: Kwanini wanaume wanadhibiti mavazi ya wanawake? 

JANA tarehe 1 Juni 2021, Spika wa Bunge Job Ndugai alimwamuru mbunge mmoja wa kike, Condester Sichalwe (Momba), aondoke kwenye ukumbi wa Bunge kwa maelezo kuwa hakuvaa nguo za staha. Spika alitoa agizo hilo baada ya mbunge wa kiume, Hussein Nassor Amar (Nyang’wale), kulalamikia uvaji wa mbunge huyo. Hatua hiyo ya spika imezua gumzo kila kona. Katika uchambuzi huu mfupi, mwanaharakati wa jinsia Laeticia Mukurasi anajadili udhaifu wa upande mwingine unaojidhihirisha katika tukio hili. Endelea.

Kitendo cha Spika wa Bunge, Job Ndugai, kumfukuza mbunge mmoja wa kike kwa kigezo kuwa amevaa nguo zisizostahili jana Juni Mosi 2021, ni cha kusikitisha. 

Kwa kweli ni dhahiri kwamba dhana ya usawa wa kijinsia itachukua miongo kadhaa kutekelezwa iwapo vitendo vya unyanyasaji kama hivi havitakomeshwa. 

Kitendo alichofanyiwa mbunge huyu kimeonyesha mtazamo hasi wa hali ya juu wa  kuumeni  (male chauvinism) dhidi ya wanawake. 

Condester Michael Sichalwe akiwa amevalia vazi “lililovunja heshima ya spika na mbunge mwingine wa kiume” jana bungeni

Kama hali hii haitakemewa inaweza kuwa kikwazo kikubwa dhidi ya harakati za haki za wanawake hasa katika nafasi za uongozi na kuchochea vitendo hasi vya aina hii nje ya bunge. 

Taswira inayojitokeza ni kuwa wenye hati miliki ya nafasi zote za umma, yaani public spaces, ni wanaume ambao wao tu ndio wana haki  ya kuamua nani avae nini katika maeneo gani. 

Swali ni kwamba kwa nini wanaume daima wanataka kudhibiti vitendo vya wanawake? 

Wanaume wanaotetea udhalimu huu dhidi ya wanawake hupenda kuhalalisha vitendo vyao kwa kujitetea kwamba vinawashawishi kuwa na fikra za ngono. 

Esther Bulaya na Halima Mdee katika viwanja vya Bunge

Hata hivyo, ikumbukwe – na  kuna ushahidi wa kutosha – kwamba hata wanawake katika nchi kama Saudi Arabia, Iraq na Iran ambao huvaa baibui, burka na hijab kila mara watokapo majumbani mwao, nao hubakwa na kushambuliwa kingono. Hivyo hoja hiyo haina mashiko. 

Ukweli ni kwamba uhusiano wa kijinsia ni uhusiano wa kimadaraka (power relations) kati ya wanaume na wanawake. 

Wanaume walio wengi hujihisi kwamba wana haki ya kudhibiti uamuzi muhimu katika ngazi za kaya, mitaa, kitaifa na kimataifa. 

Madaraka hayo wakati mwingine hutumika vibaya kama ilivyokuwa katika tukio hili. Hakika tulichokiona ni utunishaji wa nguvu za kiume kulazimisha utashi wao kwa kuonyesha matumizi ya madaraka kwa njia ambazo ni tata na batili dhidi ya mwanamke. 

Hussein Nassor Amar (akiomba mwongozo uliosababisha mbunge wa kike aondolewe ukumbini)

Pia kimeonyesha aina ya hulka inayojulikana kama “inferiority complex” kwa kiingereza, ambayo huwafanya wanaume wapende  kujisikia kwamba wao ni viumbe bora zaidi ya  wanawake na kujikweza kwa kujiaminisha kwamba wao si duni kwa wanawake.

Kilichotokea bungeni jana kimetusononesha wengi tunaofuatilia nyendo za Bunge. Hiki ni chombo muhimu ambacho kinatarajiwa kutupatia mifano ya hekima. 

Kwa kifupi, ni kwamba mbunge mmoja wa kiume aliamka na kusema kuwa kulikuwa na  mbunge mwanamke aliyevaa nguo zisizo za staha. Bila hata kutoa mwanya wa mwanamke kujitetea, Spika alitoa amri kwa mwanamke aliyetajwa atoke nje mara moja, hivyo akinyimwa  kisheria fursa ya  mchakato unaostahili.

 Lakini cha kushangaza, mama huyo alipoondoka ilidhihirika kwamba hakuwa amevaa nguo tata au tofauti sana na wanazovaa wabunge vijana wa kike wengineo.

Kushoto: Naibu Spika Tulia Ackson. Kulia: Mbunge aliyeondolewa ukumbini – hili ndilo vazi lililomponza.

Kichekesho ni kwamba badala ya wabunge wanaume pale bungeni kufunika nyuso zao ili wasione “nguo za aibu” alizovaa mbunge, walimsindikiza kwa macho manne manne, bila haya, mpaka alipotoka kabisa nje ya ukumbi wa Bunge!

Kitendo alichofanyiwa mbunge huyo kinaonyesha chuki ya wazi dhidi ya wanawake (yaani misogyny) ambayo huchukua sura nyingi kama; kuwafanyia vitendo vinavyoonyesha dharau, ubaguzi, ukatili kuwadhoofisha na  kuwakatisha tamaa. 

Lakini kama Profesa Wangari Maathai (Mungu amlaze mahali pema) alivyosema, kitu ambacho kinahitaji kuwekewa umuhimu zaidi si mwonekano au kile kilicho ndani ya suruali au chini ya kitovu, bali kilicho ndani ya kichwa cha mhusika. 

Wanawake wasiangaliwe  na kudhalilishwa kwa sababu ya mavazi au jinsi yao, bali wathaminiwe kwa michango yao katika kuleta mitazamo mbadala na kutetea masuala ya maendeleo. 

Mbunge huyu anastahili kulindiwa heshima yake na kuombwa msamaha. 

Ikumbukwe kuwa tuna rais mwanamke sasa ambaye matendo yake yanaonyesha uimara na busara kubwa. Ametupatia ridhaa ya kukosoa mahali ambapo tunaona mambo hayaendi sawa. Tujisahihishe.

Imeandikwa na Laeticia Mukurasi, mtaalamu na mwanaharakati wa maswala ya jinsia na siasa, mstaafu  kutoka Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB). 

Like