Luis Suarez: Barcelona walinichukulia poa

BAO la Luis Suarez ambalo ni la 21 msimu huu, liliwahakikishia Mabingwa wapya wa Uhispania Atletico Madrid ushindi dhidi ya Real Valladolid hiyo jana.

Ushindi huo wa Atletico, uliwanyima ubingwa mabingwa watetezi na mahasimu wao wa jadi ambao pia wanatoka katika Jiji moja la Madrid, Real Madrid.

Alipokuwa na Barcelona, Luis Suarez alifunga mabao 195 ndani ya misimu sita kabla ya kuruhusiwa kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu uliopita na kujiunga na Atletico Madrid.

Nyota huyo mwenye miaka 34, aliwanyamazisha watesi wake kwani ni goli lake la 21 la msimu huu hapo jana, lililowapatia ubingwa Atletico Madrid. Baada ya mwamuzi kupuliza kipenga kwa mara ya mwisho, Suarez alishindwa kujizuia na kumwga machozi ya furaha hadharani.

“Nimepitia wakati mgumu sana, nilidharaulika mno, lakini Atletico walinipokea kwa mikono miwili,” anasema, akiliambia gazeti la Marca baada ya mchezo, na kuongeza:

“Ni wengi walioumizwa -mke wangu na watoto wangu. Kila siku ni wao ambao wamekuwa wakiumia zaidi kutokana na kazi yangu hii. Msimu huu umekuwa mzuri sana, hatukujali magumu tuliyoyapitia, tumekuwa thabiti mpaka leo tumekuwa Mabingwa, hii ni kutokana na nusu ya kwanza ya msimu ambayo tulikuwa na ufanisi mkubwa sana ambao haukuwa na mfano.”

Mabao yaliyowekwa kimiani na Angel Correa na Suarez kipindi cha pili cha mchezo, yaliwawezesha Atletico kutoka nyuma kwa Bao moja lililokuwa limewekwa kambani na Oscar

Plano katika kipindi cha kwanza. Kutokana na ushindi huo wa mabao mawili kwa moja, Atletico Madrid walitwaa Ubingwa wa La Liga kwa msimu huu.

Kwa Diego Simeone ‘Cholo’, ushindi huo ulikuwa na umuhimu mkubwa sana kwani licha ya kuwashusha daraja wapinzani wao katika mtanange huo Real Valladolid, kama Atletico wangepoteza huku Mabingwa watetezi Real Madrid wakashinda mchezo wao dhidi ya Villareal, Atletico wangeambulia patupu.

Hata hivyo shindi wa Real Madrid kutoka nyuma na kushinda kwa mabao mawili dhidi ya moja, haukufua dafu kwani Atletico walinyakua Ubingwa wa La Liga kutokana na ushindi walioupata kwnye mchezo wao na hivyo kuumaliza msimu wakiwa juu ya Real Madrid kwa alama mbili zaidi kwenye msimamo wa ligi.

Mara ya mwisho kwa kocha Diego Simeone kunyakua ubingwa huo ni msimu wa 2013/14, ila mara hii alijawa na hisia kali sana.

“Wamejawa na hisia tofauti, hivi sasa dunia inapitia kipindi kigumu sana na ni matumaini yangu kuwa tumewapa watu hamasa,” anasema, “sio kitu rahisi kukaa juu ya ligi kwa wiki 32. Nawashukuru kwa dhati wachezaji waliocheza michezo michache kuliko wengine. Tulibaki kuwa timu moja na hilo ndilo lililokuwa lengo letu mpaka dakika ya mwisho.”

Suarez akizungumza na familia yake kwa simu baada ya ushindi

Simeone amekuwa kocha wa Atletico kwa muongo mmoja, na licha ya kuhofia kibarua chake, amekiri kuwa na imani kuwa timu yake hiyo imezidi kuimarika.

“Ni dhahiri kuwa watu wanaweza kunichoka. Lakini ni imani yangu kuwa klabu hii itazidi kukua na kuimarika zaidi na tukaendelea kama hivi. Klabu inazidi kukua, na ni watu ambao hamuwaoni ndio wameipatia klabu hii utulivu nyuma ya matokeo haya. Hawapo hapa kusherekea nasi lakini muda sio mwingi tutajumuika nao,” anasema.

Like
1