WhatsApp, Facebook, Instagram zazimika ghafla. Watumiaji dunia nzima wahaha

MITANDAO ya kijamii ya Facebook, WhatsApp na Instagram imekumbwa na msukosuko wa ghafla wa uliosababisha mkatiko wa mawasiliano kwa mamilioni ya watumiaji wa mitandao hiyo sehemu mbalimbali duniani leo Oktoba 4, 2021.

Kwa mujibu wa tovuti ya Downdetector.com, hali hii imetokana na App za Facebook Inc na Instagram kutohimili kishindo cha wingi wa watumiaji wa mitandao hiyo kwa wakati mmoja.

Zipo taarifa kuwa hata ndani ya kampuni ya Facebook, mambo yamekuwa magumu kwa sababu hata wafanyakazi wenyewe wamekatikiwa mawasiliano kiasi kwamba hata wanaojaribu kufungua email zao wanashindwa kwa kuwa zimejifunga.

Akitumia ukurasa wake wa Twitter, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Facebook, Andy Stone, ameandika: “Tunatambua kuwa baadhi ya watu wanashindwa kutumia mtandao wetu. Tunajitahidi kuhakikisha kila kitu kinarejeshwa katika hali ya kawaida haraka iwezekanavyo. Tunaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza.”

Hali hiyo imesababisha hitilafu ya kiufundi ambayo pia imeathiri watumiaji wa WhatsApp, mtandao mwingine unaomilikiwa na Facebook

Hadi SAUTI KUBWA inaandika habari hii, zilikuwa zimepita saa 3 tangu mitandao hiyo ilipombwa na msukosuko huo. 

Mkatiko huo wa ghafla wa mawasiliano umeathiri zaidi ndugu, marafiki na jamaa wanaotegemea mitandao hiyo kama njia muhimu ya mawasiliano. 

Vile vile, walioathirika ni maelfu ya wananchi wanaoshiriki mijadala kupitia makundi ya mitandao hiyo.

Kwa sababu hiyo, kimbilio la haraka limekuwa mitandao ya Signal, Telegram, Clubhouse  na Twitter – ambayo walau hadi sasa haijaathirika kwa msukosuko huu.

Like