Wananchi KIA waishika pabaya serikali wakipigania ardhi yao, fidia

“Ni jambo la kushangaza leo wanasema sisi ni wavamizi, si kweli. Haya anayosema msemaji wa serikali juu ya ardhi ya vijiji vya KIA ni upotoshaji tu.”

MGOGORO wa ardhi kati ya serikali na wakazi wa vijiji vinavyozunguka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) umechukua sura mpya baada ya wakazi wa eneo hilo kudai kuwa wamehamishwa kwa nguvu na kuvunjiwa nyumba zao bila kulipwa fidia yoyote. Wananchi hao wanataka majina ya waliolipwa fidia yawekwe hadharani ili waikamate uchuku serikali.

Wakazi hao wameeleza kuwa wao si wavamizi, bali walirithi ardhi hiyo kutoka kwa mababu zao waliokuwepo hapo kabla ya uhuru wa Tanganyika. Mzee Yohana Mollel, mkazi wa eneo la Kaloleni, Kata ya Majengo, alisema, “Pori Tengefu la Sanya Lelatema lilitukuta hapa, na hili linathibitishwa na barua kutoka kwa mkuu wa mkoa wa Arusha ya Januari 11, 1965, iliyoruhusu wenyeji kumiliki ekari 3,500.”

Mzee Mollel aliongeza, “Uwanja wa ndege ulipoanza kujengwa mwaka 1971, mimi nilikuwa kijana na nilishuhudia Mwalimu Julius Nyerere akizindua kwa kuchinja ng’ombe wa mzee Ngodede Kiroiye, baba yetu.

BONYEZA HAPA KUSIKIA KAULI ZAO.

Wananchi hao wametoa madai hayo Mei 20, 2024 jijini Arusha, siku chache baada ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, kutembelea eneo hilo na kutoa taarifa kwa waandishi wa habari. Matinyi alieleza kuwa eneo hilo lilianza kumilikiwa na serikali kabla ya mwaka 1969 likijulikana kama Pori Tengefu la Sanya Lelatema, na lilipimwa rasmi mwaka 1989 likiwa na ukubwa wa hekta 11,080.

Mzee Mollel aliendelea kueleza kuwa: “Ni jambo la kushangaza leo wanasema sisi ni wavamizi, si kweli. Haya anayosema Msemaji wa Serikali juu ya ardhi ya vijiji vya KIA ni upotoshaji tu.”

Mzee Mollel pia alisema: “Hatimiliki anayozungumzia Matinyi ya Aprili 2006 ni batili na ilitolewa kinyume cha sheria kwenye eneo lenye mgogoro. Hata Novemba 10, 2003, aliyekuwa mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, alifikisha mgogoro huo bungeni akiitaka serikali upatie ufumbuzi.”

Aidha, Mzee Mollel alisema: “Mobhare alipotosha aliposema kuwa wananchi hao waliingia kwenye eneo hilo mwaka 2007, huku wakieleza kuwa walikuwa eneo hilo hata kabla ya ujio wa wakoloni wa Ujerumani. Mwaka 1975 vijiji vitano vilisajiliwa kwenye eneo hilo, ambavyo ni Majengo, Malula, Samaria, Sanya Station, na Mtakuja.”
Hoja ya kuwa serikali inachukua eneo hilo ili kuboresha shughuli za uwanja wa ndege uendane na matakwa na viwango vya kimataifa haina mashiko kwani, kwa mujibu wa Mzee Mollel, eneo halali la uwanja wa KIA ni hekta 460 ambapo limezungushiwa uzio na kwa kiasi kikubwa hawajamaliza kuliendeleza. Aliwashauri waendelee kutumia eneo hilo kukidhi viwango vya kimataifa.
Wananchi wanapinga hoja kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza wapewe kifuta jasho cha shilingi bilioni 11.3 kwa maendelezo waliyofanya na wananchi hao ambayo kisheria ni mali ya serikali. Mzee Mollel alihoji: “Inakuwaje mtu avamie kisha alipwe fidia? Hili ni jambo lililolenga kuhalalisha kukwepa kufuata sheria za unyakuaji ardhi.”
Kwa upande wa kijiji cha Tindigani, ambacho Msemaji wa Serikali anasema robo tatu kiko ndani ya uwanja huku kikiwa kimebaki na eneo kubwa linalotumiwa na wananchi, wakazi wanapinga madai hayo. Wanadai kuwa kijiji hicho kilisajiliwa kama sehemu ya Sanya Station mwaka 1976 na kuchukua ardhi hiyo iliyokuwa ikitumiwa na zaidi ya wanakijiji 2,000 na kuwaachia robo si sahihi.
Wakazi wanasema kuwa serikali ilishaweka wazi kuwa hailipi fidia kwa mujibu wa sheria bali inalipa kiinua mgongo huku ikisisitiza ardhi ni mali ya serikali. Wanakijiji Esther Laizer akisoma tamko hilo alisema: “Wanakijiji walioathiriwa na jambo hili ni 20,000 na si 1,712 kama ambavyo Mobhare alivyoeleza na hakuna hata mmoja ambaye ameshalipwa fidia ya shamba lake, wala eneo la malisho au maeneo ya ibada.”
Akisoma tamko hilo, Lemirai Siria alisema: “Hoja kuwa wananchi wameshalipwa fidia ya shilingi bilioni 11.3 ina walakini mkubwa. Inawezekana waliolipwa si wahanga ambao ardhi yao imechukuliwa. Tunamuomba Rais aunde timu ije ikusanye data, data hazidanganyi. Hakuna mtu amelipwa fidia ya ardhi. Tatizo ni wale wanaotupora ndiyo wanapewa nafasi ya kuongea na sisi hatupewi.”
Mmoja wa wananchi, huku akiungwa mkono na wenzake, alisema: “Sisi hatupingi maendeleo ya nchi yetu, lakini hatushirikishwi. Tunaishi kwenye maeneo halali yaliyopimwa kisheria. Tatizo ni wale walio kwenye ofisi za umma hawamwelezi Rais ukweli. Sisi tunapiga kura kuchagua viongozi kwenye eneo letu, hivyo si wavamizi.”
Like