Waislamu Tanzania watoa waraka mzito kwa serikali

WAISLAMU nchini Tanzania wameandika na kusambaza waraka wa Idd wakiwaomba wananchi kutafakari mustakabali wa nchi katika kipindi hiki kigumu kinachosababishwa na serikali kutojali haki za raia na kuendekeza siasa za kibabe na kikatili.

Waraka huo, ambao umetolewa na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, unaitwa Waraka wa Idd El Fitr 1439H 2018, na unazungumzia haki na amani, haki na uhuru wa habari na wa kujieleza, uhuru wa bunge na mahakama, uhuru wa kuchagua, utii wa katiba na sheria, uhuru wa kisiasa, haki za kimahakama, jamii na uchumi, shughuli za uchumi, na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma.

Kwa ujumla wake, waraka huo unasema nchi imetetereka, na unawaasa waamini kujitetea dhidi ya uonevu unaosababishwa na watawala ambao katika awamu hii ya tano wameonekana kugandamiza haki za raia, zikiwamo pia za viongozi wa Kiislamu wanaonyanyaswa na kunyimwa haki zao za msingi.

Waraka huo unazungumzia pia hitaji la katiba mpya kama msingi wa mwafaka wa kitaifa, ukiitaka serikali kurejesha mchakato wa katiba mpya uliokwama baada ya Bunge Maalumu la Katiba kuuuza maoni ya wananchi na kutengeneza katiba inayopendekezwa kwa kufuata maoni ya chama tawala.

Waraka huu umetolewa katika wakati ambapo serikali imekuwa inasuguana na makanisa mawili makubwa ya Katoliki na Kilutheri kutokana na nyaraka za kichungaji zilizotolewa na maaskofu wa makanisa hayo katika kipindi cha Kwaresma na Pasaka mwaka huu.

Katika wiki mbili zilizopita, serikali ilifikia mahali pa kutishia kufuta makanisa hayo na  kuyataka yaaandike nyaraka za kuomba radhi na kufuta kauli walizotoa katika nyaraka zao juu ya masuala yale yale ambayo sasa hata Waislamu wanayajadili katika waraka wao wa Idd El Fitr.

Hata hivyo, ubabe wa serikali ziligonga mwamba baada ya kelele kupigwa kila kona, ikabidi waziri wa mambo ya nje atafute jinsi ya kunusuru serikali, akidai kwamba serikali haijatisha makanisa, na kwamba barua ya onyo iliyokuwa inasambaa mitandaoni ikidaiwa umetoka serikalini dhidi ya makanisa hayo, haikuwa ya kweli.

Hata hivyo, vyanzo vyetu ndani ya makanisa hayo na wizarani kwake vinasisitiza kuwa barua hiyo ilikuwa ya kweli na iliandikwa kwa “maagizo kutoka juu,” na kwamba licha ya kuandikiwa barua, maaskofu walisumbuliwa hata kufikia kuitwa na kuhojiwa ana kwa ana katika wizara ya mambo ya ndani – jambo ambalo halijawahi kutokea katika uhai wa taifa tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961.

Waraka huu wa Waislamu unaongeza chachu katika harakati za viongozi wa dini kukemea uovu unaotendeka nchini ukisimamiwa na vyombo vya dola ambavyo kwa miaka miwili sasa vimekuwa vinatumika dhidi ya raia wanaokosa utendaji au mwenendo wa serikali ya awamu ya tano.

SAUTI KUBWA linakuwekea nakala halisi ya waraka wa Waislamu.

Like
10

Leave a Comment

Your email address will not be published.