Mbowe azungumzia “bajeti hewa” ya serikali

FREEMAN Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema, ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni (KUB), amesema serikali imepeleka bungeni bajeti hewa.

Mbali na kuzungumzia bajeti ya mwaka huu, Mbowe amechambua pia bajeti zilizopita akionyesha kuwa baadhi ya wizara nyeti zilinyimwa fedha na kupewa asilimia mbili hadi 11 za fedha iliyoidhinishwa,  huku mafungu manono yakipelekwa ofisi ya rais kwa zaidi ya asilimia 300.

Akizungumza na vyombo vya habari leo, Mbowe amesema serikali imekuwa inapanga bajeti inayotegemea makusanyo ya fedha ambayo yapo juu ya uwezo wake kukusanya, hatimaye yanashindikana. Amesema:

“Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 29.54 lakini iliweza kukusanya mapato kutoka vyanzo vyote yaliyofikia shilingi trilioni 20.7 sawa na asilimia 70.1 ya lengo. Hii ina maana kwamba, asilimia takriban 30 iliyobaki (sawa na shilingi trilioni 8.83) ilikuwa ni makusanyo hewa.

“Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali ilipanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 31.71 lakini iliweza kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 21.89 sawa na asilimia 69 ya lengo. Hii ina maana kwamba asilimia 31 iliyobaki (sawa na shilingi trilioni 9.82) ilikuwa ni hewa.”

Vile vile, Mbowe amesema serikali ya awamu ya tano imekuwa inashindwa kutekeleza hata bajeti inayoidhinishwa na bunge kwa ajili ya wizara na sekta mbalimbali. Akitoa mfano wa hoja, alisema katika kilimo, mwaka 2016/17 seriikali ilitenga asilimia mbili tu ya fedha za wizara hiyo zilizokuwa zimeidhinishwa bungeni. Asilimia 98 zilikuwa hewa.

Kati ya shilingi bilioni 100.527 zilizoidhinishwa mwaka 2016, hadi Machi, 2017 serikali ilikuwa imetoa shilingi bilioni 2.252 sawa na asilimia 2.22. Katika mwaka wa fedha unaomalizika mwezi huu, bunge liliidhinisha shilingi bilioni 150.253, lakini hadi Machi 2018 serikali ilikuwa imetoa bilioni 16.5 ambazo ni asilimia 11 ya fedha zote.

Katika wizara ya mifugo na uvuvi, bunge liliidhinisha shilingi bilioni nne mwaka 2016, lakini serikali ilitoa  shilingi milioni 130 tu sawa na asilimia 3.25. Hali ilikuwa mbaya mwaka huu wa fedha, kwani kati ya shilingi bilioni nne zilizoidhinishwa na bunge, hadi Machi 2018 hakuna hata senti moja iliyopelekwa katika wizara hiyo.

“Pesa iliyotolewa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya wavuvi na wafugaji nchi nzima inatosha kununulia gari moja Land Cruiser mkonga,” alisema.

Sababu kuu ya kutozingatiwa kwa bajeti, kwa mujibu wa Mbowe, ni serikali kukosa uadilifu na nidhamu ya matumizi ya fedha.

Hii ni taarifa nzima ya Mbowe kwa waandishi wa habari: PRESS RELEASE – THE MOST CURRENT

Like
6

Leave a Comment

Your email address will not be published.