Wafugaji na viongozi wao Ngorongoro wapinga kanusho la serikali

Mwenyekiti wa Kijiji Kayapus amesema kuwa athari ya sumu hiyo haikuwa kwa mifugo pekee, bali pia kwa binadamu waliokunywa maziwa na kula nyama ya ng’ombe hao. Wengine walikufa, na baadhi yao wanaendelea na matibabu hospitalini wakisumbuliwa na magonjwa ya ini.

WANANCHI wa Ngorongoro wametoa ushahidi wa matokeo ya maabara nne tofauti za serikali yanayoonyesha kuwa madini ya chumvi ya mifugo yaliyosambazwa na serikali 2021 yalikuwa na viambata vya sumu ambayo iliua mifugo yao.
Wamewasilisha matokeo ya vipimo yaliyotolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali, Shirika la Viwango Tanzania,(TBS), Chuo Kikuu chw Sokoine (SUA), na Wakala wa Maabara ya Mifugo Tanzania (TVLA) ambayo yote yanaonyesha kuwa madini chumvi hayafai kwa matumizi ya mifugo.
Aidha wananchi hao wametaka  waliohusika na hujuma hiyo wawajibishwe sanjari na wafugaji kulipwa fidia ya mifugo yao iliyokufa huku wakitaka utaratibu wa awali wa kuingiza mifugo kreta kwa ajili ya kunywa maji yenye madini asilia urejeshwe kwani hawana imani na chumvi ya kupewa na serikali.
Pia wamedai kuwa, mzabuni kampuni ya vifaa vya ujenzi ya  Panga  ililipia kibali cha kuingiza kemikali nchini kutoka mamlaka ya maabara ya mkemi mkuu wa serikali jambo linaloibua maswali  mengi zaidi kwani madini ya mifugo hayana uhusiano wa aina yoyote na kemikali ambazo ni sumu.
Wananchi hao wameyasema hayo Oktoba 15, 2023 jijini Arusha wakati wakiongea na waandishi wa habari ikiwa ni siku chache baada ya mtandao huu wa SAUTI KUBWA kuibua, sakata la madini ya chumvi yaliyosambazwa na serikali kwa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro na kuua mifugo mingi ya wafugaji hivyo kuwafanya wananchi kuwa mafukara.
Baada ya SAUTI KUBWA kutoa taarifa hiyo iliwasukuma Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro.(NCAA) kutoa taarifa ya kukanusha madai hayo ya wananchi huku wakidai kuwa hakuna utafiti wa kisayansi na kimaabara umethibitisha hayo.
Diwani wa kata ya Ngorongoro, Simon Saitoti, ambaye alikuwa ni mmoja wa wajumbe wa timu ya watu wanne  iliyoundwa na Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala, kupeleka madini chumvi hayo, anasema hivi. 
Bonyeza hapo juu upate video ya kauli ya Saitoti.
Mkazi wa kata ya Ngorongoro,Kasale Mwaana akitoa ufafanuzi namna madini hayo ya chumvi yalivyoua mifugo na kuleta madhara kwa waliotumia nyama huki akidai kuwa jambo hilo  limefanywa kwa nia ovu ya kupunguza si tu idadi ya mifugo lakini na idadi ya watu ndani ya eneo hilo ambalo mara nyingi NCAA wamekuwa wakilalamika idadi ya watu na mifugo imekuwa ikiathiri shughuli za uhifadhi.
Diwani wa Misigiyo, Rokoine Moti, amemuomba Rais, Samia Suluhu kuingilia kati na kuwanusuru huku akidai wasaidizi wake wanampotosha huku akufafanua kuwa kwenye kata ya Ngorongoro jumla ya mifugo 10,020 wamekufa.
Naye, Mkazi wa kijiji cha Oloirobi, Melubo Ndara Poshe amesema hawana Imani na NCAA kuwaletea chumvi nyingine.
Mwenyekiti wa kijiji cha Oloirobi, Mbarnot Tipiliti amesema kuwa ni vema serikali ikaruhusu mifugo kunywa maji ya madini kreta kwa sababu hawana Imani tena na madini watakayopewa na serikali kama hayataua tena mifugo yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Mokilal, Thomas Marite, ameelezea namna walivyokuwa wakiwapa mifugo chumvi hiyo huku akieleza kuwa kumekuwa na propaganda inaenezwa kuwa Ngorongoro wananchi wote wamehamia Msomera jambo ambalo si kweli.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kayapus, Osoi Naitwat alisema kuwa jumla ya mifugo 6,294 walikufa kwenye kijiji chake jambo lililosababisha baadhi ya wanakijiji kufa kwa mshituko wa moyo baada ya kuona namna mifugo yao imekufa.
 Amesema kuwa athari ya sumu hiyo haikuwa kwa mifugo pekee bali pia kwa binadamu waliokunywa maziwa na nyama ambapo tayari watu kadhaa wamekufa na wengine wako hospital wakisumbuliwa na magonjwa ya ini. Juhudi za kumpata mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mwangwala kuzungumzia suala hilo ziligonga mwamba kwani simu yake ya kiganjani ilikuwa inaita muda wote bila kupokelewa.  Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno, hakujibu.
 Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mwandamizi Kitengo Cha Uhusiano wa Umma wa NCAA, Kassim Nyaki, alipoulizwa juu ya malalamiko hayo ya wananchi alisema kuwa wameshatolea ufafanuzi suala hilo kupitia tamko lao kwa umma la Oktoba 7, 2023.
Hata hivyo, juhudi za kumpata mkurugenzi wa kampuni ya vifaa vya ujenzi ya Panga, Marco Panga, kupitia namba zake za simu mbili tofauti alizoweka kwenye nyaraka za kuingiza mzigo huo kutoka nchini Kenya hazikupatikana muda wote.
BONYEZA HAPA kusikiliza kauli za madiwani wengine na wenyeviti wa vijiji wanaopinga kanusho la serikali.
Like
1