‘Chumvi ya serikali’ yapukutisha mifugo Ngorongoro

Familia ya David Kondoro ya Kijiji cha Oloirobi Kata ya Ngorongoro ilipoteza ng’ombe 35, kati ya 40. Pichani, familia yake inashuhudia mabaki ya mifupa ya mifugo yao iliyokufa kwa kula chumvi yenye sumu iliyotolewa na serikali.

“MIFUGO yangu zaidi 140 ilikufa baada ya kulishwa madini ya chumvi yenye sumu. Kwa kweli ilikuwa ni hasara kubwa sana kwa sababu mifugo ndiyo naitegemea kiuchumi.”

Hii ni kauli ya Sululu Olong’oi, mmoja kati ya  wafugaji wengi wa Tarafa ya Ngorongoro, akieleza namna mifugo yake na wengine ilivyoteketea baada ya kulishwa madini ya chumvi waliyosambaziwa na serikali.

Hata hivyo anaona ni kama kilio chao kinapuuziwa mbali. Wafugaji wanahisi serikali haina nia ya kushughulikia suala hili.

Sululu anaongeza kwa uchungu: “Sikuona wa kuniasaidia baada ya kupata hasara hiyo, nilisema nalalamikia wapi wakati chumvi hiyo tumepewa na NCAA,(Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) na ndiyo serikali… wala haijamchukulia hatua mzabuni aliyetusambazia.

“Kwenye mfuko wa madini ya chumvi wa kilo 20 ukiukoroga kwenye maji unakuta  kilo 9 mpaka 12 ni mchanga wenye rangi nyekundu… hakika walidhamiria kudhuru mifugo.”

Sululu ni mwenyeji wa Kijiji cha Oloirobi kilichopo Tarafa ya Ngorongoro. Ana simulizi refu la hasara na madhara aliyopata kiuchumi baada ya mifugo yake kufa.

Hayupo peke yake. Kilio chake ni sehemu ndogo ya vilio vya wananchi wa  Tarafa ya Ngorongoro ambayo ni kama imegeuka kisiwa cha mateso ndani ya taifa huru la Tanzania baada ya wananchi wake kujikuta wakikabiliwa na changamoto za ukosefu wa huduma za jamii baada ya serikali kuacha kutenga fedha za miradi ya maendeleo kwa ajili yao.

Aidha, wanafunzi katika shule za lata hiyo sasa wanajisaidia porini baada ya vyoo vya shule zao kujaa, huku wakiwa kwenye hatari ya kudondokewa na kuta na paa za madarasa wanayosomea. Serikali imezuia  utoaji wa vibali vya ujenzi, ukarabati na uingizaji wa  vifaa vya ujenzi kuingia.

Vile.vile, fedha zilizokuwa zikitolewa kwa ajili ya kusomesha watoto wa jamii hiyo zinatolewa kwa kusuasua huku chakula kilichokuwa kikipatikana kwa bei nafuu baada ya serikali kuzuia kilimo cha kujikimu ndani ya eneo hilo tokea mwaka 2009 nacho kikiyeyuka kwani wananchi hawapatiwi licha ya juhudi za kufuatilia zilizofanywa na wawakilishi wa wananchi zikishindwa kuza matunda.

Tarafa hiyo yenye  Vijiji 25 na Kata 11  ipo ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro linakaliwa na wafugaji wa Kimaasai ambao wapo hapo kwa mujibu wa sheria iliyoanzisha hifadhi hiyo mwaka 1959 iliyoipa NCAA jukumu la kutunza na kuendelea shughuli za Utalii, Uhifadhi na Jamii ya wafugaji walio ndani ya eneo hilo.

Ili uifikie Tarafa hiyo ni lazima upite kwenye lango kuu la NCAA ambapo wao ndiyo wataamua uingie au usiingie vilevile ndiyo wenye maamuzi ya mwisho juu ya vitu vinavyopaswa kuingia .

Hilo halikuwa kuwa tatizo kwa wanachi wa Tarafa ya Ngorongoro mpaka mwaka 2017 baada ya serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kuanza kampeni ya kupunguza watu na mifugo ndani ya NCAA wakidai kuwa wanaharibu shughuli za uhifadhi na utalii.

Serikali inadaiwa kuzuia miradi ya maendeleo  hali inayosababisha wananchi wa tarafa ya Ngorongoro kuishi kwa mateso huku wakiwa kwenye hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko baada ya wanafunzi kuanza kujisaidia porini baada ya vyoo vya shule zao kujaa na NCAA kukataa kutoa vibali ya uingizaji wa vifaa vya ukarabati wala kuruhusu magari ya kunyonya maji taka kuingia ndani ya eneo hilo.

Kama hiyo haitoshi Serikali inadaiwa kuandaa mpango wa kuwafukarisha wananchi hao ambapo inadaiwa kwa nia ovu walisambaza madini ya chumvi ya mifugo yenye sumu hali iliyosababisha mifugo mingi kufa.

Fuatana nami kwenye makala hii maalum itakayokueleza kwa kina juu ya hali halisi ya maisha  ilivyo kwa wakazi wa tarafa hiyo, hatua walizochukua kukabilina nayo na nini serikali na NCAA wanaeleza juu ya kinachoendelea kwenye tarafa hiyo.

Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji, Edward Maura anaeleza:

“Mwaka 2022 tumepoteza mifugo mingi sana karibia asilimia 55 ya mifugo yote Ngorongoro,  watu wengi wanasadiki imesababishwa na chumvi ya mifugo ambayo tulipatiwa na NCAA.

“Mimi nimepoteza ng’ombe 92 japo sikuwapeleka kwa daktari wafanyiwe uchunguzi lakini kila ng’ombe kabla ya kufa walikuwa wanadhoofika sana ukiwachinja unawakuta na mchanga kwenye utumbo.”

NCAA walikuwa wanatoa chumvi hiyo bure kwa wananchi baada ya kuzuia mifugo isiingie eneo bonde la Ngorongoro kwa ajili ya kupata maji ambayo yana magadi  ambapo aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliagiza NCAA wawe wanasambaza madini ya chumdvi kwa wafugaji wa eneo hilo na kila mtu apatiwe kulingana na idadi ya mifugo aliyo nayo.

Nimeongea na Diwani wa Kata ya Ngorongoro,  Simon Saitoti ambaye pia ni taalamu wa mifugo kitaaluma amesema kuwa madini ya chumvi ya mifugo iliyosambazwa kwenye kata yake na wakala aliyepewa tenda na NCAA 2021ilisababisha  asilimia 68 ya mifugo kufa ingawa pia ukame ulichangia lakini zaidi ilisababishwa na chumvi ya madini iliyothibitika kuwa na sumu.

Anasema kuwa madini hayo ya chumvi yalisambazwa na mzabuni huyo kweye vijiji vya Irkeepus, Misigiyo, Mokilal, Oloirobi na Kayapus ambapo mifuko 1,000 ilipelekwa Irkeepus na vijiji vingine vilipata mifuko 250 kila kimoja.

“Yale madini ya  chumvi inaonyesha ililetwa na lengo ovu kwa ajili ya kuua mifugo na ilithibitika maabara hiyo chumvi ililetwa Novemba 2021 tukasambaziwa mwezi wa 12 tukagundua ni mbaya,” anasema Saitoti bila kumung’unya maneno na kuongeza:

…Mifugo ilianza kudhoofika wakawa wanakufa ukiwachinja kabla hawajafa damu inakuwa kama maji,”.

Saitoti anasema akiwa kama mwakilishi wa wananchi aliamua kuchukua hatua kwa kumpigia simu, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mwangwala, daktari wa mifugo wa wilaya na idara ya maendeleo ya jamii NCAA ambao walihusika kutuletea chumvi ya mifugo.

“DC alikuja akaangalia ile chumvi tukabaini vitu vitatu kwenye ile chumvi kuna rangi nyekundu, mawe madogo sana (mchanga)  na chumvi hapo tukashangaa kwa sababu tunajua kwenye mifugo wanaotumia mchanga ni jamii ya kuku tu,” anasema Saitoti.

Anasema DC, Mwangwala  akaunda tume ya watu wanne kwenda kuchunguza ile chumvi akiwemo  Afisa Mifugo na Uvuvi Wilaya ya Ngorongoro, Dk Chobi Chubwa,  Afisa Mifugo na Mkaguzi wa vyakula vya Mifugo Wilaya ya Ngorongoro, Kaayenye Samson Laizer,  Afisa Mifugo wa NCAA, Kilasi Mollel ,  Diwani kata ya Ngorongoro,  na Mwakilishi wa Baraza la Wafugaji PC, Simon Saitoti .

Saitoti anasema kuwa kazi ilianza mara moja ambapo walichukua sampuli ya madini ya chumvi yaliyokuwa yametolewa kwenye  vijiji vitano vya  Irkeepus, Misigiyo, Mokilal, Oloirobi na Kayapus .

“Sampuli zilikusanywa na afisa mifugo wa NCAA, Neema . Tulizichukua mimi nikiwakilisha jamii na afisa mifugo wa wilaya na msimamizi wa chakula cha mifugo wilaya na afisa mifugo wa NCAA,” anafafanua Saitoti kuwa umakini mkubwa na kuongeza

“…Tulipeleka chumvi hiyo kwa mzabuni aliyeleta chumvi hiyo ambaye ni Mmiliki wa kampuni ya Panga Buiding Company LTD, Marco Panga maarufu kama Shalalii ambaye kampuni yake inajishughulisha na biashara ya vifaa vya ujenzi ingawa ndiye elileta na  kuuza chumvi ya mifugo aina ya Naju Feed Stock Lick kutoka Nakuru nchini Kenya baada ya kushinda tenda iliyotangazwa na  Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro.”

“Alikiri kuleta chumvi hiyo mifuko 2,000 yenye ujazo wa kilogramu 20 kila mmoja ambayo kwa jumla ni sawa na Tani 40 ya chumvi yenye thamani ya Tsh 40,000,000.

“Tukaomba kibali alichotumia kusafirisha chumvi tukapata vyote. Kamati  tukaanza safari ya kuelekea Dar es Salaam kwenye vituo vitatu tofauti kwa ajili ya kuhakiki.

“Sampuli za mifuko ya chumvi iliyochukuliwa Irkepus, Misigiyo, Kayapus na Mokilal zilipelekwa katika kituo cha Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania(TVLA) kwa ajili ya uchunguzi wa kina wa uwepo wa mchanga, mawe na rangi nyekundu kwenye chumvi hiyo.”

Sampuli kutoka Misigiyo na Mokilal ilipelekwa kwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali  kwa ajili ya kuangalia uwepo wa sumu katika chumvi.

“Sampuli kutoka Oloirobi ilipelekwa Tanzania Bereau of Standards (TBS) kwa ajili ya kuangalia ubora wa chumvi na sampuli kutoka vijiji vya Irkeepus na Kayapus zilipelekwa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, (SUA), Department of Soil and Geological Science (DSGS) kwa ajili ya kuangalia Madini yaliyo ndani ya chumvi,”.

Diwani Saitoti anasema ripoti zote zilionyesha chumvi hiyo haifai kwa mifugo kwani inakula ‘bonemaro’ Uboho inafanya damu inakuwa haina vitamini kwa sababu inaharibu seli nyeupe ya mwili hivyo kuharibu kinga ya mwili, mifupa inaanza kulika kwa sababu mifugo inakosa ile nguvu ya kukabiliana na maradhi.

Kamati wakakabidhi ripoti hiyo kwa Mkuu wa wilaya, Mwangwala  April 4, 2022 ambaye aliita watu kutoka taasisi mbalimbali wakiwemo  wa NCAA, Usalamawa Taifa,Idara ya mifugo wilaya na wawakilishi wa jamii ya watu wanaishikwenye Tarafa ya Ngorongoro.

“Akasoma ile ripoti akaniahidi atakuja kwenye kata ya Ngorongoro kuwaeleza wananchi kilichotokea ni nini lakini mpaka sasa hajawahi kuja pia aliahidi kuwa ataunda timu ya kuja kuteketeza hiyo chumvi ambapo mimi pia nilikuwa kwenye timu hiyo wakiwemo maafisa usalama, daktari wa mifugo wa wilaya, afisa mifugo wa mamlaka na watu wa vyakula vya mifugo,” anaeleza Saitoti akiwa na nakala ya taarifa hiyo na kuongeza:

“Wakati nikiendelea kufuatilia suala hilo mimi nikaja kukamatwa na polisi ile issue ikaishia japo,”.

‘Nilikamatwa nikakaa gerezani miezi sita kwa kesi niliyobambikiwa ya mauaji ya askari polisi kwenye tarafa ya Loliondo. Nilipokuwa magereza hakuna mtu aliyefuatilia na hakuna chochote kilichofanyika.

“Nilipoenda gerezani niliacha mifugo 146 kwenye boma langu lakini nilipotoka baada ya miezi sita nilikuta wamebaki 12 bahati nzuri wananchi wamekuja kunichangia walau sasa nina mifugo 90.

“Mifugo wanapochinjwa ndani ya utumbo kunakuwa na mchanga na damu yake inakuwa haigandi kama inavyotakiwa kwa sababu chumvi hiyo ilikuwa inasaba isha ukosefu wa vitamin k inayofanya damu igande na nyama yake inakuwa dhaifu sana,” anasisitiza Saitoti.

Makala zijazo zitaangazia changamoto ambazo wakazi wa Tarafa ya Ngorongoro wanakabiliana nazo katika sekta muhimu kama vile elimu, afya na huduma nyingine za kijamii.

Like
11