UVUVI HARAMU: SAMAKI WA DILI WANATAJIRISHA

LICHA ya sheria kali dhidi ya uvuvi haramu ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho mbalimbali mwaka 2020, serikali imeshindwa kuzuia kosa hili.

Sheria inasema: “Mvuvi atakayekamatwa amevua samaki kwa mabomu/baruti, samaki hao watataifishwa na serikali pamoja na vifaa na vya uvuvi walivyonavyo, kufunguliwa mashtaka, kutozwa faini ama kufungwa pale atakapobainika kuwa na kosa.”

Biashara ya samaki wanaovuliwa kiharamu imeshamiri na kuendelea katika fukwe za Pwani ya Bahari ya Hindi jijini Dar es salaam.

Wafanyaji wa biashara hiyo ya samaki haramu ni wavuvi wenyewe ambao huvua kiharamu (bila ya kufuata taratibu za uvuvi) kwa kusaidiana na madalali wao.

Uchunguzi wa SAUTI KUBWA, umebaini kuwa wavuvi haramu hufanya kazi hiyo usiku wa manane na kuwasambazia wateja wao mzigo majumbani ama maeneo ya biashara zao.

Biashara hiyo inafanyika kuanzia majira ya saa saba hadi tisa usiku alfajiri katika maeneo ya vificho au wavuvi kuwapelekea wateja wao moja kwa moja majumani kwao. 

Wateja wao ni wafanyabiasha wakubwa na wadogo wa samaki na dagaa ambao huchukua mzigo wa kuanzia ndoo tatu na kuendelea, kulingana na namna walivyofanikiwa kupata mzigo baharini.

Na sababu kubwa za kufanya shughuli hizo usiku ni kukwepa kulipa kodi ya nchi ambayo wanadai kuwa ni kubwa.

Pia biashara hiyo hufanyika usiku ili kuwahi kufanya mauzo kabla ya wanunuzi kudamkia katika minada ya samaki katika fukwe mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Wavuvi kadhaa waliliambia SAUTI KUBWA kuwa sababu hizo ndizo kubwa. Sababu nyingine ni ya kupata faida kubwa ya mzigo waliovua, ambayo inategemea na bahari ilikuwaje usiku huo.

“Pale tunapotoka baharini huo usiku kwa usiku… tuna maeneo yetu maalumu ya kuuza samani hao, lakini pia wateja wetu wengine tunawapelekea waliko ili kumaliza mzigo.

“Shughuli hii inahitaji roho ngumu  ya kukabiliana na vyombo vya sheria na pindi tunapokutana navyo, tunajua namna ya kumalizana ili maisha yaendelee,” anasema mvuvi moja ambaye hakutaka jina lake lijulikane 

Wafanyabiasha wa samaki wanena

Hamis Haji (39) ni mfanyabiashara wa samaki ambaye husambaza mzigo wake katika hotel kubwa maarufu jijini Dar es Salaam. 

Anasema ana uzoefu na kazi hiyo, na sasa ni mwaka wa 10. Awali anafuata mzigo katika minada halali ya samaki katika fukwe mablimbali, lakini kwa sasa analetewa mzigo nyumbani.

“Sasa nakaribia mwaka wa tano, naletewa mzigo hadi nyumbani na wavuvi wangu au madalali wao… ninalipa kulingana na mzigo nilioupata.”

Hamis anasema kuna tofauti kubwa ya faida anayoipata endapo atanunua samaki asubuhi na samaki wa “dili” anaoletewa usiku wa manane na wateja wake.

“Si mimi tu ninayenunua samaki hawa wa dili, tupo wafanyabiasha wengi wengi wakubwa kwa wadogo … wakina mama wanaokahanga dagaa mtaani ni wateja wauri sana wa wavuvi hao.” 

Naye Husna Ally Mkazi (45) wa Kawe jijini Dar es salaam anasema samaki wa dili wana faida kuliko wa mnada wa sokonikatika fukwe zilizopo.  

Anasema anakaanga samaki na dagaa wa bahari ya Hindi, na sasa ni mwaka wa 30 bila ya kuchoka kwa sababu wana faida kubwa kwake.

“Biashara hii nimeanza nikiwa msichana wa miaka 20 na sasa nina miaka 46 ambaye ni mama mwenye watoto watano na mjukuu mmoja,” anaeleza Husna Ally Mkazi wa Kawe Jijini Dar es Salaam.

Husna anasema alianza kukahanga samaki pamoja na dagaa ndoo moja yenye mtaji wa sh 50,000 ambao alikuwa kiwafuata katika fukwe tofauti kama Bweni, Kunduchi, Ununio hata Kigamboni za Pwani ya Dar es Salaam.

Anasema  akiendelea na biashara hiyo, aliolewa na Bwana Salum Juma na kubahatika kuzaa watoto watano  ambao waliwalea kwa biashara hiyo ya kukahanga dagaa na samaki yeye na mumewe.

“Hatuna mambo makubwa na mume wangu, watoto wetu wanasoma shule za seikali kuanzia msingi hadi sekondari, na mwaka jana mwanangu mkubwa Hadija naye tulimwozesha yupu kwa mumewe na ana mtoto mmoja.”

Kwa sasa wana mtaji wa sh milioni tano ambazo zimetokana biashara hiyo ya kukaanga dagaa na samaki.

Anasema hata mwanaye Hadija mara baada ya kuolewa, alimpatia mtaji wa kukaanga samaki ambao anaendelea.

Gladness Usweo (37), mfanyabiashara ndogondogo wa dagaa wa kukaanga, anasema kuuziwa mzigo wa dili, yaani usiku, kumesababisha kupata faida kubwa ambayo imewawezesha kuweka vibanda vinne maeneo mbalimbali kuajiri akina mama wengine.

“Kwa kweli biashara ya samaki na dagaa inalipa. Sasa nina magoli manne (vibanda vya kukaangia) nimewaweka rafiki zangu ambao wananilipa kwa makubaliano tuliojiwekea.

“Sina wasiwasi na matumizi ya nyumbani, kijamii hata ada za watoto za shule nalipa bila shida … nawasihi wamama wenzangu wasichague kazi maana zote ni kazi,” anasema Gladness.  

Usimamizi wa Sera na Sheria nchini Tanzania

Katika Bajeti ya fedha ya  mwaka 2023/2024 Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatarajia kufanya maboresho ya sheria ya uvuvi sura 279 katika maeneo mbalimbali  na kanuni zinazosimamia  sekta ya uvuvi ili kuakisi mabadiliko katika sekta ya uvuvi. 

Wizara hiyo itatoa elimu ya sheria za sekta ya uvuvi kwa wadau wa uvuvi wa kanda za Ziwa Victoria, Tanganyika, Pwani na Nyanda za Juu Kusini  ili kuiwezesha nchi kunufaika na uchumi wa buluu

Pamoja na hayo, serikali imesikiliza kilio cha wavuvi kuhusu tozo na imedai kuzishughulikia kwa kiasi kikubwa ili zitakapokamilika ziwe na nafuu  kubwa kwa wavuvi.

Hata hivyo, changamoto kubwa zilizowasilishwa na wadau wa sekta ya uvuvi kwa serikali ni pamoja na uvuvi haramu, matumizi yasiyo sahihi ya taa za kuvulia samaki, mlundikano wa tozo kwa mazao ya uvuvi na uhaba wa masoko ya mazao ya uvuvi.

Tamko la kimataifa kuhusu Uvuvi Haramu

Tarehe 5 Disemba 2017 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliafiki kupitisha azimio lililopendekezwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO) kuhusu uvuvi endelevu na kuitangaza Juni 5 kila mwaka kuwa ni siku kimataifa ya kupinga uvuvi haramu usiofata kanuni na maadhimisho ya kwanza kufanyika mwaka 2018.

Uvuvi haramu usiofuata kanuni unakadiriwa kuwa ni tani milioni 26 kwa mwaka au sawa na moja ya tano ya samaki wote wanaovuliwa duniani.

Mbali ya kupora rasilimali za jamii, pia unachangia katika uharibifu wa mazingira ya bahari na kuathiri viumbe vilivyomo.

Na kwa mujibuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uvuvi ya Thailand Adsorn Promthep, soko ndilo chachu ya kuendelea kwa uvuvi huo.

FAO inakadiria kuwa uzalishaji wa ulimwengu ulifikia karibu tani milioni 179 mnamo 2018. 

Sekta za uvuvi na ufugaji wa samaki zimekua sana katika miongo ya hivi karibuni. 

“Watumiaji, wataalamu na wapenzi wa bahari ulimwenguni kote lazima wazuie mazoea haramu,” imesisitiza. 

FAO inakadiria kuwa uvuvi haramu, usioripotiwa na usiodhibitiwa husababisha upotezaji wa tani milioni 11 hadi 26 za samaki kila mwaka. Hasara za kiuchumi ni kati ya dola bilioni 10 hadi 23. 

Shughuli inayozingatiwa kama chanzo muhimu cha chakula, ajira, starehe, biashara na ustawi wa uchumi inakabiliwa na mazoea haramu katika ulimwengu ambao idadi ya watu inakua, na njaa inaendelea. Samaki ni bidhaa muhimu kwa kuhakikisha uhakika wa chakula.

Lengo la 14 la Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu linalenga hasa kudhibiti uvuvi wa samaki, kutokomeza uvuvi wa samaki kupita kiasi na haramu, uvuvi usioripotiwa na usiodhibitiwa, pamoja na vitendo vya uharibifu vinavyofanyika katika sekta hii.  

 

Like