Magufuli ni somo tosha la Katiba – Salum Mwalim

Wazanzibari tukisema wa-Tanganyika mnatuona kama ni walalamishi, lakini angalia Zanzibar tuna mawaziri wetu kule, lakini hawatambuliki hata Nairobi(Kenya) hapo, wanaotambulika ni wa Serikali ya Muungano hata katika sekta ambazo hazihusiki kabisa na masuala ya Muungano, hii sio sawa, ni lazima tuandike Katiba mpya

SALUM Mwalim, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema miaka saba ya utawala wa Hayati, Rais John Magufuli, ilikuwa ni somo tosha kuhusu udhaifu wa Katiba iliyopo na haja ya kuandikwa kwa katiba mpya bila kuchelewa.

Mwalim ameyasema hayo wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Kata ya Kirando, Jimbo la Nkasi Kaskazini, katika mfululizo wa mikutano ya Oparesheni +255, inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe.

Amesema madaraka makubwa aliyopewa Rais kwa mujibu wa katiba ya sasa, ni moja ya eneo la katiba ya sasa, lililompa Magufuli mwanya wa kuminya demokrasia, haki na uhuru wa watu na kusababisha maumivu makubwa kwa Taifa, huku kukiwa hakuna mipaka wala udhibiti wowote.

“Tanzania haihitaji utafiti wa kuoneshwa udhaifu wa katiba ya sasa kwenye eneo la madaraka ya Rais wala kwenye namna ya kuendesha uchaguzi. Maumivu tuliyoyashuhudia wakati wa Magufuli ni utafiti tosha”, alisema Mwalim ambaye pia alikuwa mgombea mwenza wa urais (CHADEMA) katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Alisema ni wazi kuwa katiba inayotumika sasa si tu imepitwa na wakati, bali pia imechoka na haiwezi kuisaidia nchi katika kujenga umoja, kukuza haki, demokrasia na kuulinda Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.

“Oparesheni hii tumeipa jina la “+255:Katiba Mpya”, ili kusukuma vuguvugu la madai ya Katiba Mpya. Tunataka maeneo makuu manne yanayolalamikiwa kwa muda mrefu yaangaliwe zaidi, maeneo hayo ni madaraka makubwa ya Rais, haja ya kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, Mifumo ya Haki na Demokarasia na Muundo wa Muungano wetu”, aliongeza Mwalim.

Alisema Katiba iliyopo imempa rais wa Tanzania hadhi ya umungu mtu, na madhara yake yalionekana zaidi wakati wa Magufuli.

“Tulikuwa tukimuona akiamka (Rais Magufuli) amenuna basi wananchi wote mnune. Ukienda kinyume ni kosa. Hivyo hivyo, akiamka amecheka wote mcheke hata kama una msiba wa mama yako mzazi nyumbani! Maisha yale hayakuwa sawa”, aliendelea Mwalimu.

Kuhusu eneo la haki,uhuru,usawa na demokrasia amesema Chadema inatamani kuona vyombo vinavyosimamia haki na demokrasia vikilindwa zaidi kikatiba, ikiwa ni pamoja na Polisi,Mahakama na vyombo vingine vya dola tofauti na ilivyo sasa, ambapo mwananchi anaweza kuonewa au vyombo hivyo kudhibitiwa.

“Mnagombana kwa mambo ya mtaani, jamaa anakwenda Polisi anatoa elfu tano anakusukumia kesi. Unakamatwa unaonewa na hakuna kinachofanyika. Hii sio sawa, lazima misingi ya haki za raia na udhibiti wa vyombo vya dola uwe wazi na uwe wa kuheshimika kikatiba, ndicho Chadema tunachokipigania kwenye Katiba Mpya”

Aidha, Mwalim ameendelea kusimama kwenye hoja ya Muungano wa Serikali tatu, ili kutoa haki,uhuru na mamlaka sawa kwa nchi mbili huru, ya Zanzibar na Tanganyika, kujiamulia na kuendesha mambo yake ya ndani pasi na kuminyana.

Mwalim ameendelea kujipambanua katika ajenda ya Muungano, akiitumia mikutano ya Oparesheni +255 tangu ilipozinduliwa Mei mwaka huu mkoani Kigoma, akielimisha wananchi juu ya dhana ya serikali tatu, ambapo alirudia msimamo wake wa wakati wote wa kutokuwa tayari kuona Muungano ukivunjika.

Kwamba hatokaa kimya katika kudai uhuru na mamlaka kamili ya Zanzibar, akitumia mifano kadhaa kuonesha namna Zanzibar inavyopoteza heshima na hadhi yake mbele ya uso wa dunia.

“Wazanzibari tukisema wa-Tanganyika mnatuona kama ni walalamishi, lakini angalia Zanzibar tuna mawaziri wetu kule, lakini hawatambuliki hata Nairobi(Kenya) hapo, wanaotambulika ni wa Serikali ya Muungano hata katika sekta ambazo hazihusiki kabisa na masuala ya Muungano, hii sio sawa, ni lazima tuandike Katiba mpya”

Mikutano hiyo iliyositishwa kwa muda ili kutoa utulivu wa kutosha kwa mikutano ya darasa la nne, itaendelea tena katika mkoa wa Rukwa kabla ya kuingia zaidi mkoa wa Songwe na kufuatiwa na Mbeya, Iringa na Njombe.

Like