Umoja wa Ulaya utaingilia mzozo wa Ukraine na Urusi?

IKIONEKANA kama vita ambavyo iko mbali sana na ardhi ya baadhi ya nchi za Ulaya ikifananishwa na Vita Kuu ya Kwanza na Vita Kuu ya Pili ya dunia, hatua ya vita ya kijeshi kati ya Ukaraine na Urusi inaweza kuwa na madhara ya kiuchumi hasa kwa baadhi ya nchi za Ulaya ambazo zinazotegemea mafuta na gesi asilia kutoka nchi ya Russia

Rais wa Urusi, Vladmir Putin, amesema yeyote atakayejaribu kuingilia mgogoro huo atashughulikiwa kikamilifu. Kwa maana hiyo, taifa lolote ambalo litaungana na Ukraine katika mzozo huu, kwa namna yoyote linaweza kujiweka katika mazingira ambayo Urusi inaweza kufanya lolote dhidi yake, hasa katika eneo la mafuta na gesi.

Kwa mujibu wa takwimu za OPEC, Urusi ni nchi ya pili kwa uuzaji wa mafuta, yakiwemo mafuta ghafi kwenda nchi mbalimbali duniani zikiwemo za bara Ulaya. Kwa hiyo, mzozo huu una athari kubwa kwa nchi za Ulaya hasa zile zitakazoonesha kuiunga mkono serikali ya Ukaraine ya Zelesky.

Kwa nchi za Ulaya bado Urusi ni nchi inayotegemewa sana kwa nishati ya mafuta na gesi. Asilimia 35 ya gesi asilia inayoingizwa Ulaya inatoka Urusi.

Lakini pia Urusi inaingiza asilimia 27 ya mafuta yanayotumiwa barani Ulaya ambayo ni kiungo muhimu katika sekta ya uchumi.  Kutokana na ndoa hii ya kibiashara kati ya Urusi na bara la Ulaya, huenda nchi washirika wa Marekani pia wasiweze kushiriki katika mzozo huu ili kulinda maslahi yao ya kibiashara.

Mataifa ya NATO hapo awali yalionekana kujitayarisha kuingia katika mzozo huu, huku picha zikisambaa mitandaoni mwishoni mwa mwaka jana kuwa majeshi ya NATO yanajiandaa kujibu jaribio lolote la kijeshi litakalofanywa na Urusi dhidi ya Ukraine.

Lakini swali ni je, mataifa ya bara Ulaya pamoja na wanachama wa NATO watathubutu kuingia katika mzozo huu? Jibu la swali hili ni la muda huku maslahi ya kibiashara yakitangulia kwa sasa.

 Katika kile kinachoonekana kama kujibu mapigo tayari Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, amesema ni wakati sasa wa Umoja wa Ulaya kusitisha utegemezi wake wa mafuta kutoka taifa la Urusi.

Baadhi ya wachambuzi wa uchumi wanasema ni vgumu kwa mataifa mengi ya Ulaya kuingilia mzozo huu kwani bado wana kumbukumbu ya mzozo wa mwaka 2014 na kile kilichotokea katika bei za mafuta.

Uvamizi wa Urusi katika eneo la Crimea mwaka 2014, ulifanya mataifa mengi ya Ulaya kuiwekea vikwazo Urusi kwa kuingilia eneo hilo la pembe ya Ukraine. Lakini matokeo yake ni kupanda kwa bei ya mafuta kote duniani huku waathirika wakubwa wakiwa ni nchi za Umoja wa Ulaya. 

Ndani ya saa chache baada ya Rais Putin kutangaza hatua ya kijeshi dhidi ya Ukraine, tayari bei ya mafuta katika soko la dunia imepanda na kufikia kiwango cha mwaka 2014 wakati wa mzozo wa Crimea. 

Je mzozo huu una athari gani za kiuchumi kwa Ulaya?

Kwa baadhi ya nchi Ulaya, jaribio lolote la kuingilia mzozo huu linaweza kuwa na athari za moja kwa moja katika uchumi wao. Nchi za Ujerumani, Ufaransa, Uholanzi, Poland, Italia na Ubelgiji wote wanategemea Urusi kwa uuzwaji wa bidhaa zao pamoja na uingizwaji wa baadhi ya bidhaa kutoka Urusi.

Kwa pamoja bara la Ulaya litaathirika kwa kiasi kikubwa kwani ndio wawekezaji namba moja nchini Urusi wakiwa na uwekezaji wa Euro billioni 311.4 kwa takwimu za mwaka 2019. Kwa sasa, uuzaji wa bidhaa za mataifa ya Ulaya kwa Urusi kwa mwaka ni wastani wa Euro bilioni 80 kwa mwaka. Kiwango hicho ni asilimia 0.6 ya pato la mataifa ya Ulaya.

Athari nyingine zinaweza kuonekana katika kupanda kwa bei za nafaka. Ukraine ni mzalishaji mkubwa wa nafaka kwa baadhi ya nchi za Ulaya. Kwa namna yoyote ile, vita katika ardhi ya Ukraine utaathiri uzalishaji na usafrishaji wa nafaka kwenda Ulaya.

Matokeo mengine ya mzozo huu kwa bara la Ulaya ni kupanda kwa gharama za bidhaa na uzalishaji kwa ujumla kwani kama Urusi itafanya maamuzi yoyote ya kusitisha uingizwaji wa mafuta barani Ulaya, basi gharama za uzalishaji zinaweza kuwa kubwa.

Kwanini Urusi inaingilia maeneo na majimbo ya Ukraine?

Tangu kuanguka kwa shirikisho la Urusi lililojulikana kama Union of Soviet Socialist Republics (USSR) miaka ya 1990 baada ya vita baridi, bado Urusi haijakubali baadhi ya maeneo ambayo ilikuwa na mamlaka nayo. Baadhi ya maeneo haya yana mashlahi ya kiuchumi na kiusalama kwa taifa la Urusi ambalo linazidi kujiimarisha kiuchumi dhidi ya Ulaya na Marekani.

Kwa sasa, Urusi inatetea majimbo mawili yanayotaka kujitenga na Ukraine ya Donestika na Luhanska. Jimbo la Donestika, kwa mfano ndio jimbo kubwa nchini Ukraine likiwa na mchanganyiko wa raia wake.

Asilimia kubwa ni Waukraine huku karibu robo yao ikiwa na Warusi asilia. Kwa vyoyote vile, Urusi inataka kunufaika na majimbo haya ambayo kama yatajitenga yatakuwa mshirika kwa Urusi.

Katika kile kinachoonekana kuwa mipango ya Rais Putin katika mzozo wa Ukraine, kwanza Urusi inataka nchi wanachama wa NATO waondoe majeshi yao karibu na mipaka ya Urusi, huku ikitaka mataifa ya NATO kutounga mkono Ukraine katika mgogoro wa majimbo yanayojitenga.

Pili, bado Rais Putin ana hofu kubwa ya taifa la Ukraine kujiunga na mataifa ya NATO, jambo ambalo linazua hofu za kibiashara na kiusalama hasa katika eneo la Crimea. Urusi inaamini endapo Ukraine itajiunga na Mataifa ya NATO, basi wanaweza kuungana katika juhudi za pamoja za kurudisha eneo la Crimea kwa Ukraine jambo ambalo Rais Putin hawezi kukubali.

Like
1