Miradi ya kimkakati Chato yakwama

Mikakati kamambe ya kuigeuza Wilaya ya Chato mkoani Geita kuwa kitovu cha uwekezaji na neema ya maendeleo nchini Tanzania, sasa imekwama, SAUTI KUBWA inaeleza pasipo shaka.

Wachambuzi wa kisiasa nchini wanasema lukwama kwa mikakati hiyo kumetokana na kifo cha Rais John Pombe Magufuli, mwenyeji wa Chato, ambaye alitangazwa kufariki dunia tarehe 17 Machi 2021.

Wanasema miradi yote iliyopelekwa Chato katika kipindi cha utawala wake ilikuwa inasukumwa na rais mwenyewe kwa shabaha za kupafanya nyumbani kwake kuwa kituo na kivutio kikubwa cha maendeleo, jambo lililolalamikiwa chini chini hata miongoni mwa baadhi ya watendaji wa serikali aliyoiongoza.

Ukiwa umebaki mwezi mmoja tu kutimiza mwaka tangu alipoaga dunia, pilikapilika nyingi na mikakati ya kuendeleza Chato ama vimesimama au vimeachwa kabisa.

Katika miaka mitano ya uongozi wake, Magufuli alianzisha miradi mingi kwa shabaha ya kuiweka Chato katika ramani ya dunia kqma moja ya makazi rais ambayo yangepewa upendeleo maalumu wa kuwa na viwanda vingi, vyuo vikuu, viwanja vya ndege, mbuga za wanyama, hoteli za kifahari, hata kama wananchi – hasa wapinzani – walipinga kuwa ni upendeleo usio wa lazima unaojenga msingi mbaya wa baadaye.

Magufuli alidhamiria kuifanya Chato kuwa na bandari kubwa katika Ziwa Victoria. Sasa mradi huo umekwama.

Magufuli alikuwa ameagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuipa kipaumbele Bandari ya Nyamirembe ili iwe ya kimkakati kwa msingi kwamba itahudumia upokeaji mizigo itokayo nchi jirani za Rwanda, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Tayari TPA ilipokea maelekezo hayo na kuanza mchakato wa kuihuisha bandari hiyo ya Nyamirembe ‘iliyokufa’ miaka mingi iliyopita kwa kukosa tija kwa nchi.

Chanzo cha habari kutoka TPA ambacho hakikupenda kutajwa jina kilisema kwa kifupi,”tumekwama.”

Kiongozi mmoja mwandamizi mbaye hakupenda kutajwa cheo wala jina lake alisema:

“Unapelekaje bandari Chato ambako hakuna uhakika wa mapato? Hiyo bandari ilishakufa. Bwana mkubwa tu alitaka kuirejesha kwa matamanio yake, lakini ni hasara, hakuna tija, na si sahihi serikali kuendelea kutupa pesa huko – labda rais akilazimisha kwa sababu za kisiasa – tusije kuhojiwa mbele ya safari tukakosa majibu yenye tija.”

Mradi mwingine wa “kimkakati,” kama ulivyokuwa ukitamkwa na Rais Magufuli mwenyewe ni ujenzi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji.

Mradi huu uliokuwa chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ulielezwa kuwa ungekuwa mkubwa zaidi Afrika Mashariki, ukiwa na lengo la kuzalisha samaki anuai kwa kuanzishwa mabwawa makubwa, na viumbe wengine wa maji laini.

Sababu ya kujenga mradi huko Chato ilielezwa kuwa ni “uwepo wa maji baridi jirani” – kwa maana ya Ziwa Victoria.

Katika maendeleo ya mradi huo, tayari serikali ililipa wananchi waliokuwa wakimiliki maeneo kijijini Rubambagwe ambako kituo hicho kilipangwa kujengwa. Wananchi hao walilipwa Sh. Milioni 42 kwa ajili ya fidia kwa maeneo yao.

Gharama ya mradi huo ilipangwa na kupitishwa na serikali kuwa ni Sh. bilioni 3.8 hadi kukamilika kwake, ikiwa ni pamoja na majengo ya ofisi, mabweni, mabwawa, karakana, ofisi na miundombinu.

Uchunguzi wa SAUTI KUBWA umebaini kwamba Rais Magufuli aliidhinisha Sh. milioni 710 zipelekwe katika mradi huo.

Wakati ule, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ni Dotto James, mpwa wa Rais Magufuli, ambaye sasa ameondolewa.

Mmoja wa maofisa waandamizi katika wizara hiyo alipoulizwa kuhusu mradi huo, alieleza: “Sitaki kuhusishwa katika sakata la mradi huo.” Alipobanwa kwanini anasema mradi huo ni sakata, alisema atafutwe msemaji wa wizara. Msemaji hakupatikana hadi tunaenda mitamboni.

SAUTI KUBWA haikuona mradi huo katika orodha ya miradi inayotajwa na tovuti ya wizara husika. Waziri wa wizara hiyo, Mashimba Ndaki, alipoulizwa kuhusu kinachoendelea, alisema kwa kifupi, “ngoja nifuatilie, nitakupigia.”

Mradi mwingine ni ujenzi wa uwanja wa michezo Chato, ambao ulielezwa na Rais Magufuli kwamba ungekuwa wa kisasa na wenye hadhi ya kimataifa. Magufuli alisisitiza kuwa lazima ujengwe ili kuwa chachu ya kuvutia wawekezaji na kukuza vipaji kwa vijana.

Hata hivyo, jitihada za SAUTI KUBWA kupata uhakika iwapo serikali bado inalea ndoto hiyo hazikufanikiwa. Ofisa mmoja mwandamizi wizarani alidai kuwa wao hawana bajeti hiyo na kwamba mradi huo ulikuwa ni mpango binafsi wa Rais Magufuli.

“Mpango wa ujenzi huo haupo wizarani, na hakuna mahala popote wizara inaelekeza kwamba kutajengwa uwanja mkubwa wa kisasa Chato, ingawa tunafahamu kwamba Rais Magufuli alipanga kujenga uwanja huo. Sasa tusingeweza kuuliza anapata wapi fedha, na hata michoro yake hatujui kama ipo au haipo hapa kwetu…Tafadhali tusitajane,” alisema ofisa huyo.

Ujenzi wa kampasi kubwa wa Chuo cha Utumishi wa Umma nao sasa umekwama. Rais Magufuli aliaga dunia kabla hata ya kuanza ujenzi huo.

Taarifa za uhakika zinaeleza kwamba chuo hicho kilipewa eneo la ekari takribani 42 bure katika Kijiji ch Rubambagwe. Hivi sasa uongozi wa chuo hicho hauzungumzii tena mradi huo, na SAUTI KUBWA ilielezwa kuwa “ujenzi huo ulibebwa na upepo wa siasa za Magufuli, na ulizimika naye.”

Mradi mwingine mkubwa ambao ulikuwa uambatane na kukamilika kwa ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Kanda ya Ziwa Chato, ni kuwepo kwa tawi la Chuo Kikuu cha Tiba na Sayasi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS). Hata hivyo, baada ya Rais Magufuli kufariki, mipango yote iliyoonekana ikienda kwa kasi kuanzishwa kwa tawi hilo, “imekufa.”

Habari kutoka ndani ya Wizara ya Afya na Chuo Kikuu cha Muhimbili zinaeleza kwamba mpango wa kuwa na tawi la MUHAS Chato haupo tena kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

SAUTI KUBWA ilitembelea katika hospitali hiyo ya rufaa ya Chato na kuona majengo mengi na vifaa tiba vya kisasa, lakini kulikuwa na wagonjwa wachache. Pia iligundua kuna vitanda na ofisi katika majengo yaliyotajwa kuwa yalipangwa kwa ajili ya chuo hicho kikuu.

Mbali na maendeleo hayo kusimama kwa taasisi za umma, pia SAUTI KUBWA imegundua kukwama au kuachwa kwa majengo mengi makubwa yaliyokuwa yamepangwa kuwa hoteli, hasa katika maeneo ya ‘fukwe za Ziwa Victoria.’

Mmoja wa matajiri wakubwa wa kanda hiyo, Mwita Gachuma, ambaye alikuwa na ujenzi mkubwa wa ghala la vinywaji baridi Chato, hivi sasa amehamisha mawe katika eneo hilo, huku akieleza kwamba “hakuna hela Chato baada ya Magufuli kufariki.”

Like
1