KATIKA wiki mbili hizi, tayari kuna kila dalili kwamba Watanzania wengi, hasa wakazi wa Dar es Salaam, wamezinduka na kuanza kuzingatia njia za kujikinga na maambukizi ya janga la Corona baada ya miezi mingi ya uzembe uliosababishwa na tangazo la Rais John Magufuli kuwa “Tanzania haina Corona.”
Idadi kubwa ya watu wanaotembea na wanaosafiri ndani ya vyombo vya usafiri wa ummaa, katika daladala na mabasi ya mwendokasi, wanaonekana kuvaa barakoa, huku wengine wakibeba vitakasa mikono.
Hatua hii inaonyesha kuwa Watanzania wameanza kuepuka kauli na misimamo ya baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wanadai kuwa ugonjwa wa Corona haupo Tanzania.
Wananchi wamemua kupuuza wanasiasa hao, wakiongozwa na Rais John Magufuli ambaye amekuwa akitumia mimbari za makanisa kutangazia taifa kuwa Mungu ameliponya taifa dhidi ya Corona. Sasa wanasikiliza dhamiri zao na sauti za viongozi kadhaa wa dini – hasa Wakatoliki na Walutheri – ambao wameamua kusema ukweli na kuandika nyaraka za kichungaji zilizosambazwa na kusomwa makanisani kwa wiki mbili sasa.
SAUTI KUBWA, katika kuthibitisha hatua hii, imezungukia baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, hasa kutoka kituo cha mabasi ya mwendokasi Morocco hadi Stesheni, na kubaini idadi kubwa ya abiria ambao sasa wanavaa barakoa.
Katika mzunguko mmojawapo, basi la mwendokasi liliondoka Morocco saa 3.30 asubuhi. Baada ya kufika Stesheni saa 4.12, waandishi wetu walitembelea maeneo ya katikati ya jiji na kukutana na watu wakiwa wamevaa barakoa.
Ndani ya Benki ya Mwalimu, Mtaa wa Samora, tumekuta sanitaiza na askari alielekeza wateja wote kutakasa mikono yao kabla ya kupanga mstari kwa ajili ya kupewa huduma.
Katika jengo liitwalo Jubilee Tower, jengo lililopo Mtaa wa Ohio, kulikuwa na foleni ya wageni wakielekezwa kunawa mikono kabla ya kuingia ndani. Jengo hilo lina ofisi nyingi.
Katika Hospitali ya Taifa, Muhimbili, kulionekana vijana wengi wakiuza barakoa kwa Sh.1,000 kila moja. Vijana hao walikuwa wakimkimbilia kila anayepita kuelekea hospitali iwapo alionekana hajavaa barakoa. Waendesha pikipiki waliobeba waandishi wetu nao walivaa barakoa.
“Mama, wewe huwezi kuingia hospitali hadi uwe na barakoa, utazuiwa,” kijana mmoja alimweleza mwandishi wetu kwa sauti ya juu. Mwandishi hakuwa ameivaa kwa sababu za kiuchunguzi, lakini alikuwa nayo. akaichomoa mfukoni na kuivaa alipokaribia geti.
Mmoja wa waandishi wetu aliyefika katika geti la hospitali, alielekezwa kunawa mikono kwa maji tiririka, ndipo akaruhusiwa kuingia hospitalini hapo. Idadi kubwa ya wananchi waliokuwa katika hospitali hiyo walivaa barakoa.
Jiji la Dar es Salaam limekuwa linatajwa kuwa na maambukizi mengi ya Corona, licha ya madai na amri ya Rais Magufuli juu ya maambukizo hayo.
Ongezeko la maambukizi na matukio mengi ya vifo vitokanavyo na “changamoto za upumuaji” yamesikika katika mikoa mingi ya Dar es Salaam na miji mingine, hasa Arusha, Moshi na Bukoba. Baadhi ya madaktari wamethibitisha kwa siri kuwepo maambukizi mengi, na kuwataka watu wachukue hatua za kujilinda.
Daktari mmoja wa Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam, anasema: “Wananchi wasiwasikilize wanasiasa. Uhai ni wao na familia zao.” Hii ni kauli inayofanana na ya Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe (KKKT) ambaye Jumapili iliyopita alisema kuwa “uhai ni mali ya mtu binafsi, si wa serikali, hivyo kila mmoja alinde uhai wake.”
Kiongozi, gazeti la Kanisa Katoliki, lilichapisa habari kuu yenye kichwa: “Korona ipo.” Ni baada ya Baraza la Maaskofu kutoa waraka na kuwataka waamini na wananchi kujulinda dhidi ya Corona.
Kabla yao, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha alikuwa ametoa waraka akionya waamini kwa kusema “tusitembee juu ya mbigiri.” Alifuatiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadei Ruwa’ichi, aliyewataka waamini waache mzaha na Corona kwani ipo na inaua.
Baadaye ulifuata waraka kutoka kwa Kiongozi wa KKKT, Askofu Frederick Shoo aliyewataka waamini kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya Corona.
Matamko haya ya viongozi wa dini hizi kubwa yamekuwa kama uasi dhidi ya msimamo wa serikali, na yamegeuka chachu ya mabadiliko ya mwenendo kwa wananchi, na yanaweza kunusuru wengi, ingawa tayari wengi wameumia na kufarikia dunia katika miezi ambayo rais aliachiwa atumie mimbari za makanisa kusema “hakuna Corona.”
Shirika la Afya Duniani (WHO) limeitaka Tanzania kuchuka hatua zinazofaa kutoa taarifa na takwimu endelevu za ugonjwa huo, ili kuepusha Watanzania na maambukizi na hata vifo vinavyoweza kuzuilika kwa kufuata taratibu za kuzuia kuenea kwa Corona. Tanzania bado inasisitiza kwamba ugonjwa huo haupo.
WHO inaelekeza kuwa njia nzuri za kuzuia maambukizi ni pamoja na kuacha kuwepo kwenye mikusanyiko na kama ikilazimu, basi kila mtu akae mbali na mwenzake; lazima kuvaa barakoa; lazima kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka, kufunika midomo kila mtu anapokwenda mwayo au kupiga chafya.
Tanzania ndiyo nchi pekee katika Afrika ambayo viongozi wake wamekuwa wakakanusha uwepo wa Corona- kwa sababu za kisiasa. Rais Magufuli alizuia serikali kutangaza takwimu na taarifa zozote za Corona tangu Mei 29, mwaka jana. Hadi wakati huo, Tanzania ilikuwa imerekodi vifo 21 na na maambukizi 509.