Tusishobokee wawekezaji wa Kichina. Wengi wao ni wahujumu mamboleo

Katika uchambuzi huu, Raia Mzalendo anazungumzia baadhi ya matukio na vituko alivyoshuhudia kutoka kwa wawekezaji wa Kichina ambao kwa mtazamo wake ni mabeberu wa zama mpya na wahujumu mambo leo. Endelea.

TANZANIA ni miongoni mwa nchi zinazopendwa zaidi na wawekezaji kutoka nje ya mipaka yake; hawa wanakuja kuwekeza mitaji yao kwa ajili ya kufanya biashara mbalimbali.

Wapo wanaoanzisha viwanda, wanaoagiza bidhaa na wengine kufanya biashara mbalimbali wakifungua viwanda, kuuza bidhaa na wengine wakiingia kwenye shughuli za uchimbaji madini.

Wapo pia wanaofanya shughuli zao katika bahari. Hawa wanavua samaki na utajiri mwingine ndani ya maji chumvi, hasa Bahari ya Hindi, kwenye ukanda wa Tanzania unaokubalika kwa sheria za mipaka ya maji.

Hata hivyo, pamoja na nia njema ya kuruhusu uwekezaji, kuna baadhi yao wanaohujumu uchumi, kuvuruga ustawi na neema ya Tanzania na watu wake kwa mgongo wa uwekezaji.

Miongoni mwao ni wawekezaji kutoka China. Hapa nazungumzia wale wanaofanya shughuli za uvuvi ndani ya Bahari ya Hindi. Wale wanaovua kaa hai na kamba kochi.

Wachina wengi wanaofanya biashara hii, walianza kuvua majongoo bahari, lakini serikali ilipiga marufuku  kubainika kupungua kwake baharini. Hata hivyo, baadhi ya wawekezaji hao walikimbilia Zanzibar na Msumbiji sababu walijua nchi hizo hazijapiga marufuku kuvuliwa na hata kusafirishwa.

Kwa wale walioendelea kubaki, waliamua kuingia kwenye biashara ya kaa hai na kamba kochi hai.

Hata hivyo, ikabainika kuwa hawa wanaofanya biashara hiyo siyo wawekezaji wa eneo hilo, bali ni wale wenye kuwekeza katika maeneo mengine, hasa maduka ya ujenzi, wenye viwanda na mahoteli na wale wenye kujihusisha na michezo ya kamari, iliyoko Dar es Salaam.

Hawa wamewekezaji mitaji mikubwa huko kwenye uvuvi wakijua kuwepo kuwepo kwa fedha nyingi kuliko biashara halali na zile walizosajili kuzifanya wakiwa Tanzania.

Imebainika kuwa Wachina wanaofanya biashara hii maeneo ya ukanda wa pwani; Zanzibar, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara, wamekuwa pia wakiwatumia vijana wa Tanzania kuvua na kuwauzia kamba kochi na kaa hai wakiwa bado wadogo. Hatua hii ni mbaya na haikubaliki kwani inamaliza kizazi cha viumbe hao wa baharini.

Wachina hawa hawana uchungu na maliasili za nchi hii, ndiyo maana wanafanya hivi na wanajua kabisa kuwa wakimaliza kuvua viumbe hao, basi wao hawana la kupoteza, wanafunga virago na kuondoka.

Pia imebainika kuwa Wachina hawa wanawatumia wananchi wenye leseni za uvuvi kuwakusanyia mazao mengine ya majini ambayo hayarhusiwi kwa wageni. Hawa Wachina wamekuwa wakiwapa pesa wananchi na kuwakusanyia viumbe hao wasiokuwa na ukubwa wa kutosha. Wao hawajali.

Habari za kuwepo kwa uvuvi huu haramu zimesharipotiwa kwa baadhi ya taasisi za serikali, lakini kitu cha ajabu ni kwamba hakuna hatua zinazochukuliwa, isipokuwa kuonekana biashara hizo zikiendelea kama kawaida.

Kufuatia malalamiko ya wazalendo wa nchi hii kwa vyombo husika, habari zilifika Ubalozi wa China nchini na balozi akalazimika kutuma wasaidizi wake kutembelea maeneo ya pwani na kujiridhisha kwamba kuna ukweli.

Hata hivyo, wasaidizi hao walipomaliza ziara yao waliondoka na hatukuona kinachoendelea kwa maana ya kukoma kwa biashara hiyo haramu.

Ifahamike kuwa tatizo lingine kubwa kwa Wachina wengi wanaowekeza hapa nchini ni dharau; wanadiriki hata kusema kwamba wao hawawezi kufanywa lolote na serikali kwa kuwa China – nchi yao, inasaidia sana Tanzania na kuwa Rais Magufuli anawapenda sana. Wamekuwa wakisema mara kwa mara kwamba Watanzania wanapenda sana rushwa.

Kutokana na tabia zao hizi, ni vyema Watanzania wakajua kuwa kuishi na kufanya kazi na Mchina, inabidi kuwa makini na kutumia akili zaidi ilia ache kuinyonya nchi yetu.

Kitu kingine ni kuwa Wachina wamekuwa wakiua sana biashara za wanyonge, hasa kunapokuwepo na minada ya mazao ya baharini.

Wao wananunua kwa bei yoyote. Bei kubwa ambazo wachuuzi wengine hawazi kumudu, hivyo kuchukua kila kinachopigwa mnada.

Hatua hii inawanyima nafasi wachuuzi wadogo kupata biashara na mitaani kukosekana kwa samaki wanauzwa kwa bei nafuu kwa ajili ya matumizi ya familia za wananchi wenye vipato vya kawaida.

Kitu kingine ambacho nimekibaini ni kuwepo kwa kampuni za Tanzania ambazo zinasaidia kusafirisha mazao ya bahari kwenda nje ya mipaka ya nchi yetu.

Kampuni hizi kwa kutumia njia ileile ya kupewa rushwa na Wachina, zinahusika kubeba hata mizigo ambayo ni haramu. Nazo zinatumika kugawa rushwa kwa waendaji wa serikali ili kuruhusu kutendeka kwa uhujumu uchumi.

Wahusika wakuu ni baadhi ya watendaji wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvivu. Hawa wanashiriki katika kuhujumu nchi yetu kwa manufaa ya Wachina kwa kupewa rushwa na kuruhusu kufanyika kwa jinai.

Ni kutokana na tabia hizo za rushwa, wafanyabiashara wazawa wanaolipa kodi kihalali, wasiotoa rushwa, wanakosa biashara, hivyo wengi wako njiani kufilisika kwa kuwa wanashindwa kushindana na Wachina waliobobea kwa rushwa.

Ni muda muafaka sasa kwa Tanzania kuzuia biashara yam azo ya bahari, hasa kwa viumbe hai ambao ni wadogo, hivyo ktofaa kuvuliwa wala kuuzwa popote.

Ikiwa hali ya sasa itaendelea, upo uwezekano wa kumalizika kwa samaki na viumbe wengine muhimu kwa ikolojia ya majini na zaidi sana kuneemesha maisha ya Watanzania kwa biashara halali na neema kwa afya ya walaji.

Like