Corona yapukutisha majenerali wa jeshi watano ndani ya wiki mbili

TANZANIA imepoteza wapiganaji wake – wenye vyeo vya juu jeshini – mabrigedia jenerali watano – ndani ya wiki mbili kutokana na kile kinachoelezwa na serikali kuwa ni changamoto ya upumuaji.

Uchunguzi unaonyesha kuwa kwa siku 13 tu, viongozi hao wakubwa ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walipoteza maisha baada ya kupatwa ‘nyumonia kali’ (acute pneumonia).

Taarifa zilizopatikana kwa ndugu, jamaa na wanafamilia wa karibu, zinaeleza kuwa maofisa hao wakubwa ndani ya jeshi hilo waliugua ghafla na kukimbizwa hospitalini baada ya kapata shida katika mfumo wao wa hewa na kupumua.

Dalili za ugonjwa uliowakumba wanajeshi hao ni pamoja na kubanwa kifua, kushindwa kupumua, homa kali, kukosa hisia za kunusa na kuumwa kichwa.

Dalili zote hizi ndizo zinazoelezwa na wataalamu wa afya kuwa ni mnyumbuliko wa viashiria vyote vya kuambukizwa kwa ugonjwa wa Corona.

Madaktari nchini Tanzania wamezuiwa kutangaza popote kuwepo kwa ugonjwa wa Corona na kwamba hata mgonjwa anapofariki, vyeti vyake huandikwa sababu za kifo kuwa ni nyumonia kali au changamoto ya upumuaji.

Wanajeshi hao, wote wakiwa ni wastaafu ni pamoja na Brigedia Jenerali mstaafu, Emmanuel Maganga amefariki dunia Januari 22, 2021 katika Hospitali ya Jeshi ya Mirambo, Tabora alikokuwa akipatiwa matibabu. Alizikwa kijini kwao, Tuliani, Morogoro Januari 25. Baada ya kustaafu utumishi ndani ya jeshi, Rais John Magufuli alimteau kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Baada ya wiki moja kufariki Maganga, Brigedia Jenerali Martin Likubuka Mwankanye aliaga dunia Januari 29, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali Kuu ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam. Alizikwa Kijiji cha Kibisi, Wilaya ya Rungwe, Mbeya Februari Mosi, 2021.

Siku moja baada ya Mwankanye kufariki dunia, Brigedia Jenerali Matata Juma Mang’wamba alikumbwa na umati Januari 30, 2021 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Cardinal Rugambwa, Ukonga, Dar es Salaam. Alizikwa makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam Febaruari Mosi, 2021.

Baada ya kupita siku moja ya kufariki kwa Mang’wamba, Brigedia Jenerali Abdallah Mwemnjudi, alifariki Februari Mosi, 2021 katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, Dar es Salaam na kuzikwa Februari 4, Kijiji cha Kibindu, Wilaya ya Handeni, Tanga. Huyu aliwahi kuwa Ofisa Utendaji na Mafunzo wa Jeshi la Wanamaji wa Tanzania.

Siku moja kabla ya kuzikwa kwa Mwemnjudi, Brigedia Jenerali Ezra Wilson Ndimgwango, aliyewahi kuwa Ofisa Mkuu  wa JWTZ, alifariki dunia Februari 03, 2021 katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, Dar es Salaam. Alizikwa katika makaburi ya ‘Air wing,’ Ukonga, Februari 06, 2021.

Mbali na viongozi hao wakuu wa JWTZ, mpiganaji mwingine, Kanali Faustine Itangaja, alifariki Januari 22, Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuzikwa nyumbani kwake Makongo, Dar es Salaam, Januari 28. Aliwahi kuwa Mkuu wa Kikosi cha Askari Jeshi (MP) ndani ya JWTZ.

Kiongozi mwingine, askari wa ngazi ya ju ndani ya Jeshi la Magereza, naibu kamishina wa jeshi hilo, Julius Sang’uti alifariki dunia Januari 20, 2021 katika hospitali ya Benjamini Mkapa. Alizikwa Januari 23, 2021 katika Kijiji cha Ikulilo-Mwandete Mkoani Simiyu.

Katika kipindi hichohicho, tasnia ya sheria nayo ilikumbwa na mtikisiko mkubwa baada ya mawakili tisa kufariki dunia ndani ya siku 40.

Hao ni pamoja na mawakili wawili wa mkoani Morogoro, Alex Sikalumba na Allen Mwakyoma. Wengine ni Angel Korosso aliyefariki Januari 28, Edson Mkisi aliyefariki Januari 26, Lord Munuo Ng’uni aliyefariki Januari 25, Profesa Nicholaus Nditi aliyefariki Januari 27, Tumaini Pius aliyefariki Januari 21 na Hashim Ngole Januari 9.

Mikoa iliyotikiswa na vifo hivyo vya mawakili wa kujitegemea ambao ni wanachama wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) ni Kilimanjaro, Dar es Salaam, Tabora, Dodoma, Morogoro na katika orodha ya mawakili waliokufa yuko pia Aneth Lwiza.

Rais wa TLS, Dk Rugemeleza Nshala amesema wanachama zaidi ya 10 wamefariki ndani ya siku 45 kuanzia Desemba mwishoni – mwaka jana, 2020 hadi mwanzoni mwa Februari, 2021.

Dk. Nshala alisema wanachama hao wamefariki kwa sababu tofauti kama vile ugonjwa wa sasa wa homa kali ya mapafu pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza kama vile kisukari, figo na shinikizo la damu.

Tanzania, pamoja na Korea Kaskazini ndizo nchi pekee duniani ziazoficha taarifa na takwimu za kuwepo kwa janga la Corona. Viongozi wake; Rais John Magufuli na mwenzake, Kim Jong Un, wanakataa kuwepo kwa ugojwa huo, huku wakiweka makatazo makali kwa yeyote anayetangaza lolote kuhusu chochote kwa ugonjwa huo ambao unaendelea kuangamiza mamlioni ya watu. Viongozi hao pia hawataki kuruhusu chanjo ya Corona kutumika ili kukinga wananchi wao dhidi ya maambukizi ya ujonjwa huo hatari zaidi.

Like
4