Uamuzi kesi ya Mbowe: Shitaka moja lafutwa, washitakiwa wana kesi ya kujibu

Kama ilivyowasilishwa na ripota raia, BJ, leo tarehe 18 Februari 2022.

Jaji tayari ameshaingia mahakamani na kesi imeanza saa 7:55 mchana. Kesi namba 16 ya Mwaka 2021 Jamuhuri dhidi ya Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe inatajwa.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji. Ikupendeze naitwa Robert Kidando na hapa nipo pamoja na wakili

  1. Pius Hilla
  2. Abdallah Chavula
  3. Jenitreza Kitali
  4. Nassoro Katuga
  5. Esther Martin
  6. Ignasi Mwinuka
  7. Tulimanywa Majige

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji. Ikupendeza naitwa Peter Kibatala na hapa nipo na

  1. Iddi Msawanga
  2. Sisty Aloyce
  3. Michael Mwangasa
  4. Seleman Matauka
  5. Alex Massaba
  6. Gaston Garubindi
  7. Hadija Aron
  8. Evaresta Kisanga
  9. Maria Mushi
  10. Paul Kisabo
  11. Edward Heche
  12. Jeremiah Mtobesya
  13. Nashon Nkungu
  14. John Mallya
  15. Fredrick Kihwelo
  16. Dickson Matata

KIBATALA: Ni hayo tu Mheshimiwa Jaji.

(Jaji anawaita washitakiwa wote wanne na wote nao wanaitika kuwa wapo Mahakamani).

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji shauri limekuja kwa ajili ya kutolewa uamuzi mdogo baada ya upande wa mashitaka kufunga kesi yetu. Tupo tayari kupokea uamuzi Mheshimiwa Jaji.

KIBATALA: Nasi pia Mheshimiwa Jaji tuko tayari kwa ajili ya kupokea uamuzi mdogo.

(Jaji anaandika kidogo).

(Mahakama iko kimya).

JAJI: Kama ambavyo mawakili wamezungumza kwamba shauri lipo Mahakamani kwa ajili ya uamuzi mdogo. Na uamuzi upo mdogo. Na uamuzi huu mdogo upo tayari. Nafanya chini ya kifungu cha 41 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200. Ikitaka kujibu kama washitakiwa wana kesi ya kujibu au hapana. Kwa kupima ushahidi, naangalia kama kuna chochote cha kuita washitakiwa waweze kujitetea. Kama Mahakama ikiona kwa ushahidi ulioletwa wana kesi ya kujibu, watapa nafasi ya kujitetea. Na kwa maana hiyo Mahakama ikiona pia kwa ushahidi ulioletwa hawana vya kujibu, basi Mahakama itawaachia.

JAJI: Kwa Mujibu wa Sheria Kesi ya Mahakama ya rufani ‘Phillip Vs Jamuhuri’ kesi namba 217/2020, Mahakama ilisema kwamba Mahakama hii inakwenda kutekeleza jukumu hilo. Mahakama Kabla haijafika ni vizuri ikasema washitakiwa ni akina nani na wameshtakiwa kwa makosa gani. Washitakiwa ni Khalfani Bwire, Adam Kasekwa, Mohammed Ling’wenya na Freeman Mbowe. Washitakiwa wameshtakiwa kwa makosa sita. Makosa ya kula njama kutenda vitendo vya kigaidi, kwamba walivunja kifungu namba 4(3)i, 2(2), 9, na kifungu cha 27(c) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi.

Shitaka la pili ni la mshitakiwa wa nne. Anashtakiwa kwa kosa la kufadhili ugaidi kinyume cha kifungu cha 57, 62. Kosa lingine ni kushiriki kikao cha kula njama za kutenda vitendo vya kigaidi. Hapa wanadaiwa kuvunja sheria kifungu cha 4(1) 3,5 na 57 ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi, na kosa la tano ni mshitakiwa wa kwanza peke yake kukuta na vifaa ambavyo ni vya kutendea ugaidi.

Anadaiwa kuvunja sheria Kifungu cha 6(1), 3(1). Maelezo ya mashitaka ni kwamba washitakiwa wote wanne wanadaiwa siku ya tarehe 1 Mei 2020 wakiwa katika Hotel ya Aishi na maeneo mbalimbali ya Arusha, Mwanza na Morogoro, walikula njama ya kutaka kuchoma vituo vya mafuta. Vitendo ambavyo walikuwa wanataka kuleta hofu kwa Watanzania. Katika kifungu hicho hicho washitakiwa wanadaiwa kula njama za kutaka kumdhuru Lengai Ole Sabaya Mkuu wa Wilaya ya Hai, kutaka kuleta hofu na taharuki kwenye nchi. Mshitakiwa namba nne katika vipindi mbalimbali yeye mwenyewe alitoa fedha mbalimbali kwa mshitakiwa namba moja, mbili na tatu kama sehemu ya kutaka kufadhili ugaidi.

Vitendo ambavyo vilikuwa vilete madhara kwa Watanzania na kuleta hofu kwa Watanzania. Washitakiwa namba moja, mbili, tatu na nne wanadaiwa kushiriki katika vikao kwa nia ya kutaka kulipua vituo vya mafuta, vitendo vilivyolenga kuleta hofu kwa Watanzania. Kosa la tano ni mshitakiwa namba mbili, eneo la Rau Madukani mshitakiwa alikutwa anamiliki bastola aina ya Luger A5340 ambayo silaha hiyo ililenga kutumika katika vitendo vya kigaidi. Kosa la sita mshitakiwa namba moja ndiye anayeshtakiwa peke yake, ambapo mshitakiwa namba moja alikutwa anamiliki pair (sare) nne za suruali za JWTZ, pair moja la shati la JWTZ, pair moja ya shati la JKT, jacket, kofia tano za JWTZ, overall la JWTZ, Ponjol ya JWTZ, berret mbili za kofia za JWTZ.

Beji mbili za Hassan HD, ranks mbili za vyeo vya Koplo mali ya JWTZ, kidaftari cha 5 Star alichokutwa nacho, mikanda minne ya JWTZ, pair moja ya soksi, pair moja ya rackets ya JWTZ, kukutwa na ‘wing’ moja ambayo ni beji ya ku- attend mafunzo ya parachute. Kisu cha AK 47 cha JWTZ. Vitu vyote vililenga kutumika katika matendo ya ugaidi. Washitakiwa wote waliposimamishwa mbele ya Mahakama walikana makosa. Mbele ya kaka yangu Jaji Siyani walikana mashitaka yao. Walikubali tu maelezo yao ya particulars. Walikubali kuwa waliwahi kufanya kazi katika kambi ya Ngerengere.

Mshitakiwa namba nne alikiri kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema na kwamba alikamatwa Mwanza Nyamagana. Upande wa mashitaka waliongozwa na mawakili Robert Kidando, Pius Hilla, Abdallah Chavula, Jenitreza Kitali, Nassoro Katuga, Ignasi Mwinuka na Wakili wa Serikali Tulimanywa Majige. Upande wa Utetezi walikuwa mawakili 19. Mtobesya na Nashon Nkungu wakimwakilisha mshitakiwa wa kwanza. John Mallya mshitakiwa wa pili, Fredrick Kihwelo na Dickson Matata wakimwakilisha mshitakiwa wa tatu wakati Peter Kibatala na mawakili wengine wakimwakilisha mshitakiwa wa nne.

Mashahidi waliokuja walikuwa ni ACP Kingai, Kaaya, Hafidh, Mahita, Madembwe, Gladys Fimbari, Luteni Denis Urio, Tumaini Sostenes Swila, ….

(Upande wa mashtaka) walileta vielelezo, silaha … bastola aina ya Luger A5340, risasi hai (moja), maganda mawili ya risasi, barua kutoka TiGO, muamwala wa fedha kutoka TiGO, KYC, barua kutoka kwa Marajisi, certificate ya Handing Over ya bastola, Seizure Certificate ya kukamata uniform za mshitakiwa wa kwanza, barua ya Kamishina wa Forensic Bureau, KYC ya 0784-779 944, KYC ya 0782-237 913, Financial Transactions Report ya 0787-555 200, Financial Report ya 0784-779 944, taarifa ya uchunguzi kutoka _Extraction Report, simu moja ya Tecno labeled A, labeled B, labeled C, labeled D na simu labeled H, certificate of handing over ya pistol, certificate ya Inspekta Swila na Luteni Denis Urio.

Upande wa Mashitaka wakati wanasikilizwa, upande wa utetezi waliweza kuingiza kielelezo kama maelezo ya Justine Kaaya, maelezo ya Anitha Matalo, maelezo ya shahidi Mahita, maelezo ya shahidi Luteni Dennis Urio, maelezo ya Sostenes Swila kama kielelezo namba tano (5). Katika hatua hii ni vizuri kujua kuwa vielelezo vyote vilivyopokelewa kwa upande wa utetezi vilipokelewa baada ya Mahakama kufanya kesi ndogo. Jukumu la Mahakama ni kupitia ushahidi na kuona kama kesi imetengenezeka. Kwa mujibu wa maelezo ya DPP vs Philip katika ukurasa wa 14 na 15, jukumu la Mahakama ni kupitia ushahidi kuona kama washitakiwa wanayo kesi ya kujibu, shahidi wa maneno na ushahidi wa nyaraka kisha kujibu swali moja tu. Kesi ya upande wa mashitaka kufunga imetengenezeka. Mahakama ya Rufaa ilisema kwamba…

(Jaji anasoma…)

Kwa uelewa wangu ni kwamba katika hatua hii, katika kungalia washitakiwa kama wana kesi ya kujibu, Mahakama inatakiwa kungalia ushahidi kwa ujumla wake. Mahakama iangalie ushahidi wa juu kama ushahidi uliletewa kama kuna kesi ya kujibu kisha washitakiwa waitwe kwa ajili ya utetezi. Katika siku hizi tatu nimepitia ushahidi wote na vielelezo vyote 39 na baada ya kupitia vyote maamuzi ni haya yafuatayo. Naanza na kosa la namba sita kwa mshitakiwa namba moja.

Anadaiwa alikuwa na mali/Vifaa vinavyodaiwa kutendea ugaidi, kwamba akivunja vifungu ambavyo nimeshavitaja, mali ambazo zilikuwa nyumbani kwake nimeshazitaja. Katika kosa hili ushahidi uliletewa Mahakamani katika kosa hili, walileta uniform (sare). Mahakama ilikataa kupokea vielelezo hivyo kwa sababu wakati wanakamatwa kimsingi hawakukamata vielelezo hivyo. Hapakuwa na vielelezo vingine hapakuwa na ushahidi mwingine. Mshitakiwa hana kesi ya kujibu, na Mahakama imeenda kuangalia kuwa katika kifungu hicho cha 21 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, hakuna jambo ambalo Mahakama imeelekezwa inapokuwa Mahakama imeelekezwa kwamba kama Sheria ya Uhujumu Uchumi hakuna … kielelezo na hakuna maelekezo ya Sura namba 200 ya Sheria ya Uhujumu Uchumi … Katika kifungu hicho Mahakama imeona hakuna kesi kwa hiyo Mahakama haiwezi kuwaita kwa utetezi bali wataachiwa. atika kosa hili hakuna ushahidi wa kufanya mshitakiwa awe na kosa la kujibu na Mahakama inamuachia huru mshitakiwa kwa kosa hilo.

Mahakama imepitia vielelezo vyote vya upande wa mashitaka na utetezi. Bila kwenda ndani, Mahakama hii inaona kwamba upo ushahidi kwamba washitakiwa wana kosa la kujibu. Kwa maana hiyo Mahakama hii imewakuta washitakiwa wa kwanza, wa pili na watatu na wanne wana kosa la kujibu kwa makosa yanayofuata. Kwa maana hiyo Mahakama inawapa nafasi ya kujitetea na wanayo haki ya kukaa kimya. Mahakama inaruhusu kufanya adverse comment. Katika hatua hii kosa la shitaka moja la sita mshitakiwa hana kesi ya kujibu. Kwa maana hiyo nawaalika kwamba … kwa utaratibu gani wataamua kujitetea. Kwa maana hiyo natoa AMRI.

MTOBESYA: Mheshimiwa Jaji naomba kujadiliana na mteja wangu.

JAJI: Na wengine wote mnaweza kufanya hivyo kwa wateja wenu.

(Mawakili wa utetezi wanaelekea kizimbani kuongea na wateja wao).

MTOBESYA: Mheshimiwa Jaji sijui kama naruhusiwa kuweka maneno kwa niaba ya mteja wangu.

JAJI: Kwa kifungu hicho inaruhusiwa kwa niaba ya mshitakiwa.

MTOBESYA: Mshitakiwa wa kwanza, wa pili na wanne baada ya kuwasiliana naye anategemea kujitetea chini ya kiapo na kuleta mashahidi watano pamoja na yeye ni wa sita.

MTOBESYA: Na kwamba atatoa vielelezo vitano katika ushahidi wake.

Mallya: Kwa niaba ya mshitakiwa wa pili tumepokea uamuzi wa Mahakama. Na mshitakiwa wa pili kwa makosa ya kwanza, pili na nne na la tano ambalo anashtakiwa peke yake.

Mallya: Anakusudia kujitetea yeye mwenyewe chini ya kiapo na kuleta mashahidi wengine wawili na anakusudia kuleta vielelezo vinne katika utetezi wake.

Wakili Fredrick Kihwelo: Mheshimiwa Jaji, kwa niaba ya mshitakiwa wa tatu tumepopkea uamuzi wa Mahakama. Mshitakiwa atajitetea mwenyewe chini ya kiapo na atakuwa na mashahidi watano na vielelezo vitano.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, mshitakiwa wa nne atajitetea chini ya kiapo na ataleta mashahidi 10 pamoja na yeye watakuwa 11 na anategemea kutumia vielelezo 20.

JAJI: Baada ya hapa, nafahamu kwamba natakiwa kutoa nakala ya mwenendo wa kesi. Kwa hiyo nikipata siku saba natarajia kuwa itakuwa tayari.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, nilikuwa napitia Rule 15(2) The Economic and Bribe Crimes za mwaka 2016. Moja ya kanuni za uendeshaji wa shauri hili, pande zote mbili zinatakiwa kutoa majina na anuani za mashahidi pamoja na orodha ambazo zitatumika katika kesi. Katika shauri dogo wenzetu upande wa utetezi wakiwa wanafanya uwakilishi wa pamoja, waliorodhesha mashahidi wanne na waliomba ruhusa ya kuficha shahidi wa tano. Walipewa ruhusa mpaka pale walipohitajika kukutwa na kesi ya kujibu walipaswa kutoa majina.

MTOBESYA: Mheshimiwa Jaji, kwa kutokutaja majina imejielekeza katika kifungu cha ulinzi wa mashahidi. Ukipata jina na usipomuita utakuwa umepata value gani?

JAJI: Wewe hayo umeyatoa wapi?

MTOBESYA: Ndiyo maana nasema tunaweza kutaja majina 100 na tukaleta mtu mmoja atakuwa amefaidika nini?

JAJI: Labda niseme kwamba je, kuna amri ya kuficha majina ya mashahidi?

MTOBESYA: Ipo. Ndiyo.

JAJI: Ndiyo hiyo ruling inasema hivyo?

MTOBESYA: Vyovyote vile itakavyokuwa, Mahakama wakati ule ilitoa ruling wakajitetea kwa pamoja. Kwa Pamoja kwa sasa labda Mahakama irejee maamuzi yake.

JAJI: Kwa sasa ukitaja majina kuna tatizo?

MTOBESYA: Ndiyo. Kwa sababu kifungu cha kutaja majina ni kidogo sana mbele ya kifungu cha kumlinda shahidi.

JAJI: Turudi kwenye hoja ya msingi. Je, Mahakama inaamua tu bila kufuata utaratibu? Mahakama inafikiaje hapo ndipo uamuzi ufanywe? Je, huo utaratibu umefuatwa?

MTOBESYA: Sasa Mheshimiwa Jaji, tusomee kama utaweza.

JAJI: Ambapo kwa bahati mbaya sina hapa. Itabidi nikatafute. Au kama mnatuhakikishia ruling inasema hivyo tuendelee.

MTOBESYA: Mheshimiwa Jaji, wenzetu hawajasema kwamba tukitaja mashahidi 100 akaja mmoja watakuwa wamefaidika nini?

JAJI: Kama ambavyo wa walitaja mashahidi na hawakuja wote.

MTOBESYA: Sasa wao wana sheria kabisa inawataka wao.

JAJI: Naomba Kibatala anisaidie.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji hakuna sheria inayotaka baada ya kuwa na kesi ya kujibu, tunatakiwa kutaja majina. Mheshimiwa Jaji, mimi sikusudii kutaja majina ya mashahidi wala kutaja anuani zao. Wataje sheria ipi inayotubana. Je, tutazuiwa tusilete mashahidi? Wakati wa committal tulisema kwamba mashahidi wawili ni wanajeshi. Wanaogopa kutajwa kwanza kabla ya ushahidi kwa ulinzi wao. Sisi tumetaja idadi na hakuna kinachotubana.

KIBATALA: Uamuzi wako umesema kwamba tunatakiwa kusema kama tutajitetea na kuleta mashahidi, wala hakuna na sehemu ya ruling yako kwamba tunapaswa kutaja majina na anuani zao.

MALLYA: Mheshimiwa Jaji nini kimebadilika? Hakuna kilichobadilika baada ya Jaji Siyani kuruhusu mashahidi wasitajwe.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji, siku ile ya preliminary hearing walitakiwa kutaja mashahidi wao, wakataja shahidi IGP na wengine.

JAJI: Hoja ni kwamba hiyo ruling haipo, na je, inasema kwamba amri hiyo itakuwepo mpaka baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wao? Je, ipo? Ina ukomo? Kama amri haina ukomo itaamisha kwamba kutoka mwanzo mpaka mwisho hawatataja mashahidi. Na hii ni kama bado upande wa utetezi wakiwa wanashikilia uamuzi wake.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji huo ndio msimamo wetu na tupo tayari kufanya submission.

JAJI: Naahirisha nikaangalie.

Jaji anaondoka kwenye chumba cha mahakama.

Jaji amerejea Mahakamani. Ni saa 9:29 alasiri.

JAJI: Nilisema nijiridhishe kama amri hiyo ipo. Kumbukumbu zinaonyesha tarehe 10 Septemba 2021 upande wa utetezi ulitaja mashahidi saba.

JAJI: Ukaomba mashahidi wanne msiwataje kwa mujibu wa kifungu cha 21(4) Sheria ya Ushahidi Sura ya 367 ya mwaka 2020. Ukizuka ubishi. Baada ya hapo Jaji alitoa uamuzi kwamba kama upande wa utetezi utakutwa na kesi ya kujibu, amri itaisha. Kwa maana hiyo kama hamtaki kuwataja naomba utaratibu ufuatwe.

MTOBESYA: Nimesoma sheria ya kuzuia ugaidi, sheria ….

JAJI: Naomba kusema ilikuwa kama amri hiyo ilitajwa. Lakini kama amri imeisha mtapaswa kufuata utaratibu.

JAJI: Hata hivyo, kama amri hii itaendelea inawahusu mashahidi wanne.

MTOBESYA: Wakati huo Kibatala anazungumzia upande wote wa utetezi. Sasa tumeshajigawa. Je, amri hiyo ni valid katika kazingira hayo?

JAJI: Mimi nakazia amri ya Mahakama, kwamba sasa mmetaja mashahidi 21.

JAJI: Kama ninyi mnahitaji kuwalinda mashahidi wenu basi, mui- move Mahakama ili Mahakama ione itoe muda au isitoe.

MTOBESYA: Basi tunaomba muda tushauriane.

JAJI: Sawa.

(Mawakili wa upande wa utetezi wako pamoja wanajadiliana).

JAJI: Naona maombi hayo yalikuwa in common, huenda yalikuwa ya msingi.

MTOBESYA: Ndivyo. Hata Wakili wa Serikali Robert Kidando alishiriki Mheshimiwa Jaji. Mheshimiwa Jaji tunaomba tusimame kidogo tutete ofisini kwako na wenzetu wa Serikali.

JAJI: Kwa dakika ngapi?

MTOBESYA: Dakika tano.

JAJI: Sawa.

Jaji anaamka na kutangulia ofisini kwake.

Jaji amerejea Mahakamani wakati mahakama ikiwa kimya. Ni saa 9:54.

JAJI: Ndiyo!

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji quorum yetu ipo vile vile kama awali.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, na sisi pia tupo vile vile.

KIBATALA: Mheshimiwa Jaji, baada ya majadiliano ya maombi, iwapo au la hitaji la kutaja majina na anuani ni lazima, yatajadiliwa siku ambayo Mahakama itakapopanga kwa ajili ya washitakiwa watakapoanza kujitetea. Ukizingatia Mheshimiwa Jaji kwamba nyaraka za hukumu ndogo na nakala za proceedings zitakuwa tayari baada ya siku saba, ambayo tarehe 4 Machi 2022 ambapo washitakiwa wataanza kujitetea.

WAKILI WA SERIKALI: (Robert Kidando) Mheshimiwa Jaji hatuna pingamizi kwamba utetezi waanze tarehe 4 Machi 2022. Lakini pia yajadiliwe maombi hayo siku hiyo. Asante Mheshimiwa Jaji.

JAJI: Basi maombi ya ahirisho yanakubaliwa. Shauri litakuja Machi 4, 2022 saa tatu asubuhi. Upande wa utetezi muwe tayari kuanza kujitetea. Proceedings zitakuwa tayari baada ya siku saba. Washitakiwa wataendelea kuwa rumande chini ya Magereza mpaka tarehe 4 Machi 2022 watakapoanza kujitetea. Baada ya maneno hayo naahirisha shauri hili.

Jaji anaondoka katika chumba cha mahakama.

Like
2