IKULU IMETEKWA AU MAHAKAMA IMETEKWA?

President Samia Suluhu Hassan

KESI ya ugaidi inayomkabili Freeman Mbowe na wenzake inazidi kufunua mambo mengi yaliyokuwa sirini.

Watu wengi na taasisi kadhaa za ndani na nje wamekuwa wakimshauri Rais Samia Suluhu aondoe kesi hii mahakamani, lakini yeye amegoma kwa kisingizio kuwa hawezi kuingilia uhuru wa mahakama, na kwamba mahakama iachwe ifanye kazi yake. Sawa. 

Wanaofahamu utendaji na taasisi zetu hizi na mamlaka makubwa ya rais, wamekuwa wanahoji kuwa hata kama rais anadai haingilii mahakama, kuna mtu yeyote makini anaweza kuamini kuwa rais haingilii mahakama?

Hata rais mwenyewe anaamini kauli yake kuwa hawezi na haingilii mahakama? Hata kama asingekuwa yeye mwenyewe moja kwa moja, wangapi wanaojituma kwa jina la rais na kuingilia mahakama? 

Urais ni taasisi, na mikono mingi ya taasisi hiyo inahusika kuiteka mahakama hiyo kwa kutumwa naye au kwa maofisa wake kujipendekeza kwake.

Sasa katika shauri hili la Mbowe, SAUTI KUBWA imepata ushahidi kutoka ndani ya Ikulu na mahakama kwamba uamuzi wa Jaji Joachim Tiganga kwamba Mbowe na wenzake kuwa wana kesi ya kujibu ulibarikiwa na Ikulu kabla ya kusomwa mahakamani.

Saa tano (5) kabla ya uamuzi kusomwa mahakamani jana, baadhi ya maofisa wa Ikulu walikuwa wanahaha kufikia watu kadhaa wenye ushawishi na wanaoweza kumfikia Mbowe ili wamshauri aandike ujumbe kwa rais, na katika ujumbe huo aombe radhi ili mambo yaishe. 

Ujumbe mmoja wao, saa tano kabla ya hukumu, ulisema: “…WAMEPATIKANA NA MAKOSA 5”

Akaulizwa: “kwa nini lakini?” Naye akajibu: “SERIKALI HAIKO TAYARI KUSALIMU AMRI.” 

Akaongeza: “ILE NJIA YA KUOMBA RADHI INATAKIWA NA MAMA.”Baada ya majibizano ya muda mrefu, ofisa wa Ikulu anabembeleza: “YAANI KESI YA FREEMAN INAHARIBU MAMBO MENGI, NA HATA MISUKUMO KUTOKA NJE NI MINGI, LAKINI UNAMUACHILIA KATIKA MAZINGIRA GANI? TAFADHALI NAKUSHAURI KIMBIA UMSHAURI ACHUTAME NA KUMALIZA SUALA HILI. AANDIKE BARUA YEYE MWENYEWE KUTOKA GEREZANI AIPITISHE KWA KIONGOZI WA DINI….(anataja jina) ILI IMFIKIE MAMA HARAKA. MAMA ANACHUKUA UAMUZI HAPO HAPO KWA SIMU.”

Na kweli, ndicho kilichotokea. Ujumbe huu una tafsiri moja kuu – Ikulu yetu imetekwa. 

Mtu huyu, awe ofisa wa Ikulu wa kweli au kishoka, ni dalili kuwa Ikulu yetu imetekwa. Walioiteka Ikulu ndio wameteka mahakama. 

Mtu huyu huyu anaweza kumwamuru jaji afanye chochote. Na anaweza kufanya hivyo kwa kutumwa au bila kutumwa na rais. Majaji wetu wana simulizi nyingi mioyoni mwao.

Katika mazingira haya, kinachotafutwa ni ushindi wa dola dhidi ya Mbowe na wenzake kwa namna yoyote. Dola haitaki kushindwa. 

Kuna namna nyingine ya kulitazama suala hili. Watu wa namna hii wanaweza kumdhuru hata rais, iwapo hakubaliani nao. 

Swali muhimu ni hili: Hawa wanaoiteka ikulu na kuigeuza mahakama, kisha wakaiteka mahakama na kuigeuza ikulu, wana nia gani na Watanzania?

Malizia kwa kutazama uchambuzi huu katika VIDEO HII.

Like
17