Tundu Lissu anyamazisha wapika propaganda wa Lumumba wanaotunga maneno kuhusu tukio la kuumizwa kwake

WAPIKA propaganda wa CCM wamekuwa wanahangaika na tukio la Tundu Lissu kupigwa risasi tarehe 7 Septemba 2017; wakitaka kulnda uhalifu aliofanyiwa kama ambavyo serikali imelinda askari polisi waliomuua Akwilina Akwiline. Wanatafuta watu wa kubambikia hatia hiyo, hasa wapinzani. Lissu mwenyewe amejitokeza kuwajibu. Anasema:

Huwa sipendi sana kujibizana na watu wa aina hii kuhusu jaribio la mauaji dhidi yangu. Hata hivyo, kwa vile Joseph Yona na/au wanaomtuma wanafikiria maswali yake hayana majibu kutoka kwa viongozi wa CHADEMA, naomba mimi niliyeshambuliwa na ambaye pia kiongozi wa CHADEMA na mwajiri wa dereva wanaojaribu kumvisha uhusika wa shambulio hilo, nijibu ujinga huu.

1. Mimi na dereva wangu tulitoka bungeni saa saba mchana tukaelekea nyumbani kwangu Area D kula chakula cha mchana.

2. Hatukukutana na mtu yeyote njiani na wala hatukusimama mahali popote mpaka tulipofika nyumbani.

3. Tulianza safari ya kwenda Area D takriban saa saba mchana. Bunge lilikuwa limeahirishwa kwa ajili ya chakula cha mchana.

4. Sio kweli kwamba ni mguu wa kulia tu ndio ulioathirika. Maeneo mengine yaliyopigwa na kuumizwa vibaya ni haya:

(a) Mguu wa kushoto ulipigwa mara mbili ijapokuwa hakuna mfupa uliovunjika.

(b) Mkono wa kushoto ulipigwa na kuvunjwa vibaya chini ya kiwiko. Aidha, kipande cha risasi kilitolewa kwenye kiwiko chenyewe.

(c) Mkono wa kulia ulipigwa na kuvunjwa vibaya chini ya kiwiko.

(d) Risasi sita zilitolewa tumboni na nyingine imebaki karibu na uti wa mgongo.

5. Mwenyekiti Mbowe hakuwepo kwenye eneo la shambulizi lakini watu wengine walikuwepo:

(a) Mfanyakazi wangu wa nyumbani alikuwepo.

(b) Mke wa Waziri wa Madini Medard Kalemani ambaye tunaishi jengo moja alikuwepo.

(c) Kulikuwa na watu nyumbani kwa Katibu Mkuu wa TAMISEMI (???) ambaye naye tunaishi jengo moja na alikuwa amehamia muda sio mrefu.

(d) Kwenye jengo jirani anakoishi Naibu Spika Tulia, mfanyakazi wake wa nyumbani alikuwepo na ndiye aliyenikimbiza hospitalini.

(6) Baada ya kushambuliwa na wakati nakimbizwa hospitali, mimi ndiye niliyemwambia dereva wangu ampigie simu Mwenyekiti Mbowe na wabunge wengine kuwapa taarifa. Walifika hospitalini more or less muda huo huo niliofika mimi. Nilikuwa na fahamu muda wote mpaka nilipoingizwa theatre ndio nikapoteza fahamu.

7. Mwenyekiti Mbowe anaishi upande wa pili wa Area D. Site 3 (ninakokaa mimi) na Sengia (anakoishi Mwenyekiti) zinatenganishwa na ukuta mmoja. Yote ni majengo ya TBA na njia yetu ya kwenda au kutoka bungeni na mjini ni moja.

8. Dereva wangu aliondokea Dodoma kuja Nairobi na aliletwa na Mheshimiwa Goddie Lema. Hakukuwa na wito wowote kutoka polisi ambao hakuutii. Polisi walipoanza kuulizia habari zake tuliwaambie wamfuate Nairobi alikokuwa. Tuliwaambia wafuate utaratibu wa Sheria ya Kusaidiana Katika Masuala ya Jinai ili dereva wangu na mimi mwenyewe tuhojiwe kuhusiana na shambulio dhidi yangu. Waliahidi kuja Nairobi. Tuliwasubiri, hawakuonekana mpaka tuliposafiri kuja Ubelgiji.

9. Dereva wangu alisafiri kuja Ubelgiji kwa pesa zile zile nilizosafiria mimi. Misaada ya Wasamaria Wema.

10. Dereva wangu ana familia yake nyumbani kwao Singida. Hiyo inahusikaje na shambulio dhidi yangu???

Like
9

Leave a Comment

Your email address will not be published.