Mawe ya Mwigulu yamkera Magufuli. Yaibua matukio manne yaliyotafuna uwaziri wake

MWIGULU Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi, ameondolewa katika wadhifa wa waziri wa mambo ya ndani kwa sababu “ameshindana na rais” katika kutekeleza baadhi ya “maagizo kutoka juu,” SAUTI KUBWA linaeleza kwa uhakika.

Ingawa Rais John Magufuli alitoa malalamko mengi juzi wakati anaapisha wateule wake wapya Ikulu; kwamba haridhiki na utendaji wa wizara hiyo, na baadhi ya vyombo vya habari vikayasambaza jinsi yalivyo, imedhihirika kwamba kuna matukio makubwa manne yaliyochafua uhusiano wa rais na waziri wake, hata akamwona Nchemba kama mshindani wake ndani ya serikali.

Tukio la kwanza ni la tarehe 7 Septemba 2017, siku alipopigwa risasi Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki.

Siku hiyo, Nchemba alikuwa nje ya mji wa Dodoma kikazi. Baada ya rais kupata habari za Lissu kupigwa risasi, alimtafuta Nchemba kwenye simu, akamkosa kwa kuwa simu za waziri zilikuwa zimezimwa akiwa kwenye tukio nje ya mji. Hatimaye alimpata kupitia simu ya mtu mwingine, akamwagiza waziri aite vyombo vya habari mara moja, aseme kwamba “serikali haihusiki na shambulio dhidi ya Lissu.”

Nchemba hakuona mantiki, lakini hakubisha. Alipofika mjini kabla hajaita vyombo vya habari, aliteta na Waziri Augustine Mahiga, naye akamwambia kuwa hata yeye alikuwa ameagizwa afanye hivyo, lakini alisita kwa kuwa hadi wakati huo hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa ametuhumu serikali.

Nchemba alielekea Hospitali ya Mkoa Dodoma, akakuta watu wengi, wakiwemo waandishi wa habari, lakini kwa sababu hakuwa na habari ya kuwapa, baada ya kuwa ameshauriana na Mahiga, hakuwaita.

SAUTI KUBWA linatambua kuwa kitendo hicho kilimuudhi Rais Magufuli kiasi kwamba katika moja ya vikao vya Baraza la Mawaziri, aliwakemea mawaziri hao akidai “walionyesha dharau.”

Tukio la pili lililomponza Nchemba ni kauli na hatua yake dhidi ya Merlin Komba, msajili wa vyama wa wizara ya mambo ya ndani, ambaye aliandika barua kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) akitaka makanisa hayo yakanushe nyaraka zao za kichungaji za Kwaresima na Pasaka mwaka huu.

Uchunguzi wa SAUTI KUBWA unaonyesha kuwa Komba aliandika barua hizo kwa maelekezo kutoka Ikulu. Hata mabaraza hayo yalipojibu barua hiyo, serikali ilipuza majibu ya maandishi, ikaita na kuhoji kiongozi mmoja mmoja – Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa aliyekuwa rais wa TEC na Askofu Frederick Shoo mkuu wa KKKT.

Nakala ya barua ya KKKT ilipovuja mitandaoni na kuleta sokomoko katika jamii, Nchemba alitoa kauli (akiwa amechelewa) ya kukanusha barua ya wizara, akidai haikuwa imeandikwa na serikali bali ilikuwa feki. Alimsimamisha kazi msajili wa vyama kwa ajili ya “uchunguzi,” jambo lililozua hisia kwamba kama wizara isingekuwa imehusika na barua hiyo msajili asingesumbuliwa.

Wiki iliyopita, katika hali isiyo ya kawaida, msajili huyo aliandikiwa barua ya kurejeshwa kazini, bila hata waziri (ambaye ndiye alimsimamisha) kujua au kuhusishwa. Uchunguzi wetu umeonyesha kuwa aliyeandika barua hiyo ni naibu katibu mkuu, baada ya kupewa agizo kutoka Ikulu. Watu walio karibu na waziri wanasema hatua hiyo ilimshtua, na alijua kuwa mamlaka yake yalikuwa yameingiliwa.

Kwa tukio hili, Nchemba amekutwa na hali inayofanana na ya Nape Nnauye, aliyekuwa waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo, ambaye aliponzwa na uamuzi wake wa kuunda kamati ya kuchunguza kitendo cha Paul Makonda, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, kuvamia kituo cha televisheni usiku Machi 2017. Waliojua uhusiano wa karibu uliopo kati ya rais na Makonda waliona kama Nape alikuwa anaingiza mkono wake kinywani mwa mwamba.

Matokeo ya uchunguzi huo yalimgharimu uwaziri; na alipoita waandishi wa habari na wasanii ili kuzungumza nao baada ya kuwa amevuliwa uwaziri, alizuiwa barabarani, na akatishwa kwa bastola mbele ya polisi. Hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya mtu huyo aliyemtisha kwa bastola; na baadaye ilifahamika kuwa mtishaji huyo alikuwa askari katika kikosi cha ulinzi wa rais. Baadhi ya askari hao walipewa jukumu la kumlinda Makonda na ndio walioambatana naye usiku alipovamia kituo cha televisheni; na ndiyo maana rais hakutaka waguswe.

Vyanzo vyetu vimesema Nchemba ameondolewa wizarani kwa kuwa kuna wasaidizi wake wamemzunguka, na yeye “ameshindwa kula na kipofu bila kumgusa mikono.” Kama ilivyokuwa kwa Nape, uamuzi wa waziri ulilenga kuficha udhaifu wa serikali na kuipatanisha na waamini wa makanisa yaliyotishwa. Lakini wachambuzi wanasema macho ya Magufuli yalitazama “umaarufu” wa waziri, kwamba amejipatia sifa isiyo yake.

SAUTI KUBWA linafahamu kuwa rais amekuwa na uhusiano wa karibu na makamishna wa vyombo vya ulinzi na usalama ambao anawatumia “kuchimba” mawaziri wao. Ana kawaida ya kuwasiliana nao moja kwa moja bila kujulisha mawaziri. Hata katika hotuba yake Ikulu juzi, rais alisifu makamishana kuwa “wako vizuri kuliko viongozi wa juu wa wizara zao.”

Mtu mmoja mzito serikalini anasema: “Bwana mkubwa anataka mawaziri misukule. Ukiwa waziri mbunifu, ukataka kufanya jambo ambalo hajakuagiza, ujue utalipa gharama yake. Ndiyo maana unaona wengi wetu hatufanyi lolote hadi yeye aagize.

“Sasa Mwigulu alijisahau akafikiri kuwa anaweza kumu-impress rais kwa njia hiyo… Alisahau kwamba rais ameshaonyesha kuwa yeye peke yake ndiye anapaswa kuwa maarufu. Na usisahau, Mwigulu alichuana naye katika kinyang’anyiro cha urais 2015 ndani ya chama, na rais amekuwa anaonya wanaotaka urais.”

Tukio la tatu lililomponza Nchemba lilitajwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kilichofanyika Ikulu wiki kadhaa zilizopita, wakati Rais Magufuli anatambulisha wateule wapya wa NEC – Mizengo Pinda na Makongoro Nyerere. Rais aliwambia wajumbe kuwa ameteua wajumbe hao kwa sababu wanamuunga mkono. Chanzo chetu kimemnukuu Rais Magufuli akieleza wajumbe wa NEC, kwamba:

“Ingawa nilichuana nao katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya chama, Pinda na Makongoro wamekuwa na nidhamu, huwasikii wanapigapiga kelele, na wananiunga mkono kwa kila hatua ninayochukua. Lakini kuna wengine humu, tena baadhi yao wamo serikalini, utawasikia mara wapo mkoa huu mara ule, mara wapo kanisa hili mara lile; hawana muda wa kufanya kazi zangu, bado wapo bize wanajijenga kutafuta urais!”

Katika mikoa yote ya Tanzania Bara, vijijini na mijini, kuna majabali, mawe, miamba na miti ambayo imeandikwa jina la Mwigulu ikimnadi kwa urais mwaka 2015. Baadhi ya watu walio karibu na rais wanasema amekuwa anakerwa na “mawe hayo,” na anatamani siku moja yapasuliwe ili ujumbe wa Mwigulu usisomeke. “Hata waziri alipokuwa na ziara za kikazi mikoani, rais amekuwa anamtazama kama mtu aliyekwenda kujifanyia kampeni ya urais,” kinasisitiza chanzo hicho.

Kwa mtazamo wa Rais Magufuli, hatua ya Nchemba kutotekeleza maagizo yake au kujaribu kuyatekeleza kwa namna inayomwonyesha kama kiongozi mwangalifu, ni sawa na kushindana naye. Ndiyo maana katika kauli yake ya juzi Ikulu, rais alisema kuna baadhi ya watendaji wa serikali wanaogopa kuchukua hatua ngumu ili wapendwe, yeye achukiwe na wananchi.

Kuna tukio la nne; nalo limetokana na jinsi Nchemba alivyoshughulikia masuala kadhaa bungeni kuhusu bajeti ya wizara yake katika bunge la bajeti lililoahirishwa Ijumaa iliyopita.

Katika mjadala wa bajeti ya wizara ya mambo ya ndani, baadhi ya wabunge, hasa wapinzani, walitaka majibu ya waziri kuhusu mauaji Kibiti, kutekwa kwa Ben Saanane, Azory Gwanda, kupigwa risasi Tundu Lissu, kupotea kwa Simon Kanguye, mwenyekiti wa halmashauri Kibondo, na matukio mengine mengi yanayotishia usalama wa raia.

Kama ilivyo kawaida, mawaziri huwa wanaomba ushauri kutoka kwa wataalamu wanaosimamia idara husika kwenye wizara zao. Nchemba naye amekuwa anatumia utaratibu huo huo.

Lakini maofisa kutoka vyombo vya dola, ambavyo ndivyo vilipaswa kumshauri juu ya masuala hayo, waligoma kumpa ushirikiano wa kutosha katika maeneo hayo nyeti. Vyanzo vyetu vinasema kuna waliomwambia: “Sisi kuna mambo hatuwezi kukwambia uyaseme vipi. Haya unayotuuliza, tuna majibu yake, lakini hatuwezi kukupatia useme bungeni. Wewe ni mwanasiasa, utajua jinsi ya kusema.”

Vyanzo hivyo vinasema kuwa wakati Nchemba anajipanga kutafuta maelezo ya kutoa kwa wabunge kabla ya kuhitimisha bajeti yake, alipokea simu “kutoka juu” ikimhoji kwanini anataka kuzungumza mambo nyeti bungeni.

Chanzo kinanukuu mkubwa wake akimuuliza:  “Wewe mambo ya Saanane, Lissu na hao wengine yanakuhusu nini? Achana nayo, nenda ujibu jinsi utakavyoboresha maslahi ya polisi wako.”

Kutokana na ujumbe huu “kutoka juu” Nchemba alijiepusha na majibu kuhusu masuala hayo muhimu.

“Tangu mapema, kulikuwa na dalili kwamba mwenzetu asingeendelea na uwaziri, na hata baadhi yetu tulidhani asingemaliza hata bunge la bajeti. Ameshindwa kabisa kuendana na bwana mkubwa, na hali hii ndiyo inatufanya na sisi tuliobaki kushindwa kuwa wabunifu, maana hujui kama bwana mkubwa atafurahi au atakasirika.

“Tunabaki kusikiliza tu anachotaka, hata kama tunaona hakina maana, tunatenda tu kulinda nafasi zetu. Ni jambo baya sana, maana tunaonekana wanafiki mbele ya wananchi, lakini kwa hali ilivyo hatuna jinsi, tusamehewe tu,” kinasema chanzo kimoja cha habari kilicho serikalini.

Kilio bandia cha Rais Magufuli

Akizungumza kwa kulalama juzi Ikulu, Rais Magufuli alimweleza Kangi Lugola, waziri mpya, kwamba:

“Wizara ya mambo ya ndani haijani-impress (hainiridhishi), inafanya mambo ya hovyo. Huku juu sijawa-impressed, na lazima niwaeleze ukweli. Nimekupeleka pale ukafanye kazi, na wewe bahati nzuri ni askari.

“Kupitia kamati ya Bunge, ilifanya uchunguzi wa mikataba mbalimbali ikiwemo wa Lugumi; tulipewa maagizo na kamati ya Bunge na mpaka leo hayajapata solution (ufumbuzi). Magari 777 yaliagizwa kupitia mkataba wa hovyo. Magari ambayo yameagizwa kuletwa yameandikwa mapya, lakini yametembea zaidi ya kilometa 4,000. Yapo hayajaandikwa year of manufacture.

“Nimempeleka (Ramadhani) Kailima ambaye alisimamia vizuri kwenye uchaguzi, ukishinda umeshinda na ukishindwa umeshindwa. Mkataba ni wa hovyo hata bei ya magari ni ya hovyo, kuna mambo ya uniform hewa, niliowapeleka pale hawakutatua matatizo haya, mabilioni hayaonekani. Wewe kaa tu yako mengi.

“Kuna suala la NIDA, kuna pesa zilipotea kule hovyo hovyo, sijaona hatua ambazo zimechukuliwa. Kuna mambo yanafichwa fichwa. PCCB nao naona wanapachezea chezea, Nataka leo tuambizane ukweli.

“Nimechoka kutoa rambirambi. Mfano mzuri ni mkoa wa Mbeya. Ndani ya wiki mbili wamefariki watu 40. Hakuna hatua hata za RPC kujiuzulu, si umpunguzie nyota ili ajue damu zilizomwagika pale? Kaanze na RPC wa Mbeya na RTO.

“NGO, nyingine za hovyo na zinafanya mambo ya hovyo kinyume na maslahi ya Watanzania. Tunahitaji NGO zinazofanya kwa maslahi ya Watanzania na sio ya wenye NGO.

“Promotion ya maaskari, nashukuru IGP naliangalia hili, kashughulikie hili. Vibali vya working permit vinatolewa kama njugu, kashughulikie hili. Kuna kesi watu wameshikwa Oysterbay wanatoa working permit wao na wana mitambo yao. Ilibidi taarifa nitoe mimi mwenyewe na mmoja wa watuhumiwa ni mfanyakazi wa Immigration. Haya yalitakiwa kufanywa na waziri au naibu waziri, mnanichosha.

“Sijui nizungumze mangapi! Katika wizara zinazoongoza kwa madai ya hovyo yaliyopelekwa wizara ya fedha ni wizara ya mambo ya ndani. Magereza kawafanye wafungwa wafanye kazi, nchi nyingine duniani zinatumia wafungwa kuzalisha, hapa sisi tunawalisha, sasa ulimfunga wa nini?

 “Kuna mashamba hayatumiki, wafanye kazi kwelikweli. Mbona tumefanya amendment ya korosho, huyu wa mambo ya ndani mbona hapeleki kama wafungwa waliohukumiwa kifo sheria inawazuia kufanya kazi.”

Wachambuzi wanajadili kauli ya rais

Baadhi ya wachambuzi wa siasa waliozungumzia hotuba yake, bila kutaka kutajwa majina, wanasema “kuna maneno hayapaswi kutoka kinywani mwa rais,” na kwamba kuna dalili kwamba bado anasumbuliwa na kiwewe cha uchaguzi mkuu 2015, hasa pale anaposema, “ukishinda umeshinda, na ukishindwa umeshindwa.”

Wanasema bado rais anaamini kwamba kuna watu wanatilia shaka ushindi wake wa 2015, ambao ulisimamiwa na Kailima, ambaye alikuwa mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Sasa amempeleka kwenye wizara ya mambo ya ndani kuwa naibu katibu mkuu.

Vile vile, wanasema hata kuzungumzia masuala ya kashfa ya Lugumi ni kuibua mjadala mzito ulioibuliwa na wapinzani katika kikao cha kwanza cha Bunge mwaka 2016; wala hayana uhusiano na utendaji wa Nchemba., hasa katika mazingira ambayo yanaonyesha kuwa mwenye uamuzi wa mwisho ni rais, na wahusika wamekuwa wanahusishwa na rais mstaafu na huyu aliyepo.

Mmoja, mwanaharakati wa haki za binadamu, anasema: “Kinachoonekana hapa ni kwamba, yeyote anayechunguza lolote lazima kwanza ajue msimamo wa rais kuhusu uchunguzi huo. Yaliyompata Nape, na sasa haya ya Mwigulu, yanatuma ujumbe mzito kwamba ukichunguza jambo ambalo rais ana maslahi nalo, utaondoka tu.

“Inawezekana ndiyo sababu hata suala la NIDA liliachwa, kwani Mheshimiwa John Heche (mbunge wa Tarime Vijijini) amelisema sana bungeni, hadi limemsababishia kesi, maana aligusa wakubwa na kuwataja kwa majina. Na mbona rais hazungumzii ufisadi wa e-passport? Kama kweli yeye ni mwadilifu, mbona hazungumzii kivuko kibovu (mv Bagamoyo) alichonunua kwa pesa nyingi za walipa kodi akiwa waziri?”

Mchambuzi mmoja ambaye ni mwanasiasa wa chama tawala, anasema: “Hata hili la rambirambi linaleta hisia hasi. Hivi anaposema anatuma rambirambi, hajui anatonesha vidonda vya watu? Anataka wananchi kule Bukoba waseme nini? Maana hadi leo wanamlaumu kwa “kuchikichia” rambirambi na misaada waliyochangiwa walipopigwa na tetemeko. Huu uchungu anauona baada ya askari wake kufa katika ajali? Hao ndio anaona wana roho zinazopaswa kuhurumiwa?

“Mbona haonyeshi huruma au uchungu wowote kuhusu damu ya Lissu, hadi serikali imegoma kumtibu kwa mujibu wa sheria? Avae viatu vya wazazi wa Akwilina au yule diwani wa Morogoro aliyakatwa mapanga kama mnyama pori, aone uchungu walionao wananchi. Hivi anadhani Watanzania wote wanameza hizo propaganda zake?

“Atawatisha tu, lakini yana mwisho, ipo siku watasema. Na kwa kauli yake ya dharau na vitisho juu ya wabunge wa Kusini, waliokuwa wanatetea wakulima wa korosho, rais ameonyesha anavyojibidisha kutawala Bunge ili lisifanye kazi yake.

“Maaskofu waliposhauri kuwa mhimili wa utawala ujitahidi usishikilie mihimili ya bunge na mahakama, yeye na watu wake waliwatisha, na sasa amemfukuza waziri kutokana na sakata la maaskofu hao hao. Sasa mbona amethibitisha kwa vitendo kuwa hataki kupingwa au kukosolewa hata na vyombo vilivyowekwa rasmi kwa mujibu wa katiba?

“Na hili ka kutisha NGO, ni kielelezo cha moja ya sababu zilizomwondoa Mwigulu. Kwa Magufuli, hata makanisa ni NGO pale tu yanapomwambia ukweli asiopenda kusikia. Lakini ni vema aelewe kuwa wananchi wa kawaida wanasikiliza zaidi viongozi wa dini kuliko rais na serikali yake. Wamenyamaza tu, lakini wanaelewa kinachoendelea.

“Mawaziri hawafanyi kazi kwa kuwa wanajua waziri halisi ni rais, wao ni watu wa kuagizwa tu kama watoto wadogo. Ulisikia alivyomwagiza Dk. Harrison Mwakyembe, na sasa anavyomwagiza Lugola; ni kama vile anatuma mtoto mdogo dukani. Rais anaonea wivu mawaziri wake hadi anazindua vijimiradi vidogovidogo ilimradi wao wasionekane, eti wasipate umaarufu?”

Mchambuzi mwingine, mwanasheria, anasema: “Hata anavyo-mu-address waziri mkuu mbele ya watu, ni kwa dharau, kama kijana wake wa nyumbani. Na bila aibu, anasema eti angepiga hata shangazi zake; na watu wanachekelea tu! Kuna maneno hayapaswi kutoka kinywani mwa rais, walau akiwa hadharani. Kiongozi ukiheshimu wenzio, nao watakuheshimu.

“Kwa haya anayosema, hakuna shaka rais ana tatizo kubwa mahali fulani. Kama ingekuwa Marekani, kungekuwa kumetolewa hoja apimwe akili, kama walivyofanya kwa Rais Donald Trump. Si bure, kuna tatizo mahali. Yaani anakosa huruma na utu kwa rais wake, hata kama ni mfungwa aliyehukumiwa kifo. Sheria yenyewe inaona kile asichoona yeye.

“Mfungwa anapohukumiwa anapewa adhabu. Kulima si sehemu ya adhabu yake, hiyo ni shughuli kama nyingine, iwapo atapangiwa na magereza. Lakini rais anaona kilimo ni adhabu!

“Kadiri Rais Magufuli anavyozidi kuhutubia ndivyo anavyozidi kufunua udhaifu wake mbele ya umma. Kuna tatizo la msingi kabisa mahali fulani, hata kama watu wanaogopa kusema; na dhambi hii wataibeba waliompitisha wakati wanalijua.”

SAUTI KUBWA: “Ni tatizo gani hilo unalosisitiza?” Mchambuzi: “Silitaji leo. Ipo siku Watanzania wayalijua. Lipo!”

Like
44

Leave a Comment

Your email address will not be published.