Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar hatihati kumeguka

SERIKALI ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), iko hatarini kumeguka. Chama mshirika ACT-Wazalendo kinadai “kuminywa” na chama tawala, CCM.

Kuminywa huko kunatajwa na viongozi wote wa juu wa ACT-Wazalendo, akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar (MKR), Othman Masoud Othman.

“Inaonekana kama hakuna dhamira ya kweli ya kubadilika kivitendo, itabidi chama kikae kitafakari tunaendaje,” anasema Othman.

Baadhi ya viongozi waandamizi wa ACT-Wazalendo kufuatia hali hii, wameieleza SAUTI KUBWA kwamba chama chao kinajipanga kufanya kikao kikubwa“kupima nafasi yao” ndani ya serikali ya sasa.

“Hivi karibuni, vikao vikubwa vitakaa na kuona kama upo ulazima wa kuendelea kuwemo ndani ya serikaliau viginevyo, maana kuna mengi yanaendelea yanayokatisha tamaa ikiwa CCM na viongozi wake wanathamini Katiba inayoruhusu kuwepo kwa serikali ya pamoja,” amesema mmoja wa viongozi hao.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu (Zanzbar) wa ACT- Wazalendo, Salim Bimani akizungumza na SAUTI KUBWA kuhusu uimara wa SUK amesema “bado kuna hali tete, kunatakiwa uwazi na nia ya dhati ya viongozi wa CCM walioko serikalini ili kuimarisha umoja na kusukuma maendeleo zaidi ya Zanzibar.

Bimani kuhusu kufanyika kwa vika vya juu vya chama chake kuhusu mustakabali wa serikali hiyo ya umoja amesema; “ni kweli kutakuwa na vikao, tena kamati kuu na mtajulishwa ni lini, lakini kutakuwepo ili kujadili masuala kadhaa, likiwamo hilo la msimamo wetu ndani ya serikali.”

Makamu wa kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman

SAUTI KUBWA inazo taarifa kwamba baadhi ya taarifa na mlolongo wa kisheria ambao Ofisi ya Rais wa Zanzibar, Ikulu inapaswa kuufuata kufikisha taarifa kwa Ofisi ya MKR, hautekelezwi ipasavyo.

Kwamba hata baadhi ya mashauriano kutoka Ofisi ya MKR kwenda kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, hayapewi uzito unaostahili.

“Yapo mambo ambayo yanasikitisha na hayaonyeshi dhamira ya kweli ya kuendesha serikali ya umoja wa kitaifa ya Zanzibar, makamu wa kwanza hapewi uzito unaostahili kikatiba, yupoyupo tu,” amesema mmoja wa maofisa waandamizi wa SUK ambaye hakupenda kutajwa jina.

Anaeleza kwamba katika kuendesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa umoja, mambo mengi yanaamuriwa na chama kimoja; Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa maelezo kwamba serikali inatekeleza ilani ya chama hicho tawala, huku ushirikishwaji wa viongozi wa ACT-Wazalendo waliomo serikalini ukiwa mdogo.

Katika kuendesha serikali ya sasa ya umoja wa kitaifa, ACT-Wazalendo inaingia katika mfumo huo kwa kuwa na makamu wa kwanza wa rais, mawaziri wawili; biashara na viwanda pamoja na afya, ustawi wa jamii.

Juma Duni Haji, Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo ameeleza kutoridhishwa na kasi ya Rais Dk. Mwinyi katika kushirikisha chama hicho kuhusu masuala muhimu ya mandeleo ya visiwa hivyo.

Duni anasema Rais Dk. Mwinyi anapaswa kuonyesha Wazanzibari na dunia kwamba ana nia ya dhati ya kuijenga Zanzibar kwa umoja na kuzika tofauti za kisiasa, ambazo kwa kiasi kikubwa zimezorotesha uchumi wa visiwa hivyo.

Ofisa mmoja kutoka Ofisi ya Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, ameiambia SAUTI KUBWA kwamba serikali anayoongoza Rais Dk. Mwinyi, haijawahi kuwatenga wala kuacha kushirikisha jambo lolote linalohitaji kutekelezwa kwa pamoja na viongozi wa SUK.

Katika kukoleza moto wa kuwepo kwa mmomonyoko wa umoja katika serikali hiyo na kushikilia “usawa na haki,” matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Konde, Pemba, yamezidi kuonyesha kuwepo kwa mpasuko.

Baada ya Tume ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mgombea wa uchaguzi wa ubunge wa CCM kuwa mshindi, viongozi na wanachama wa ACT-Wazalendo walihoji utayari wa Rais Dk. Mwinyi kusimamia haki, kwani walidai kuwepo kwa mkono wa serikali yake na NEC kupokonya ushindi wao. Uchaguzi huo ulifanyika Julai 18, 2021.

Katika taarifa yake kwa umma baada ya matokeo hayo, ACT-Wazalendo ilisema “matokeo hayo ni ya kupikwa na kwamba yameiba haki ya Wazanzibari waliopiga kura kumchagua mbunge wao.

Taarifa hiyo ilionyesha kwamba matokeo halisi yanayotokana na kura halisi zilizopigwa na kuhesabiwa yalionyesha kuwa ACT-Wazalendo kiliongoza kwa kupata kura 1871 sawa na asilimi  asilimia 66, huku CCM ikipata kura 1007 – sawa na asilimia 36.

Duni ameyaita matokeo hayo kuwa ni zao la ushirika wa shetani kati ya NEC na serikali ya Zanzibar kwani wamelazimisha kuiba haki za wapiga kura.

Bimani ameyataja matokeo hayo kuwa ni hila na wizi wa haki na kudharau matakwa ya wananchi wa Zanzibar ambao waliamua kumpata kiongozi wa jimbo lao na siyo wa kuletwa kwa nguvu za dola na NEC.

Katika taarifa kwa umma chama hicho kilieleza kusononeshwa kile kichodai kuwa ni dhuluma iliyofanyika Konde na kwamba kamati ya uongozi itakutana kwa dharura kujadili dhuluma hiyo ili kupata hatua sahihi za kuchukua.

Juma Duni Haji
Like
1