Serikali ya Magufuli yatumia “kesi mbaya” kuchuma mapesa kwa kutesa wafanyabiashara, waandishi wa habari, wanaharakati

HATUA ya Serikali ya Rais John Magufuli kukamata na kutesa raia, kuwafungulia kesi mbaya na hatimaye kuwanyang’anya fedha, imeelezwa kuwa ni mkakati wa kujinufaisha kwa pesa za haraka haraka, kutisha na kukomoa “wabaya” wa rais, na kuminya uhuru wa kujieleza, SAUTI KUBWA inaripoti.

Katika miaka mitano iliyopita, miongoni mwa waathirika wakuu wa unyanyasaji huu ni baadhi ya wafanyabiashara, waandishi wa habari, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu ambao, kwa sababu kadhaa, walionekana kutokuwa katika uhusiano mzuri na serikali ya Magufuli.

Moja ya mbinu zinazotumiwa na serikali kutimiza matamanio yake na kuzuia kukosolewa, ni kuwakamata na kuwafungulia kesi zisizokuwa na dhamana wale wanaoonekana au wanaodhaniwa kutetea au kupigania uhuru na haki za wananchi, au wanaokosoa mwenendo wa serikali kibiashara na kiuchumi au waliokosana na Magufuli zamani alipokuwa hajapata urais au wanaodhaniwa kuunga mkono wapinzani na washindani wake wa kisiasa.

Imebainika kuwa baada ya serikali kukamata watetezi hao, huwaweka muda mrefu korokoroni polisi, huku mashitaka dhidi yao yakiendelea “kutengenezwa” na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili tu kuwabambika kesi zisizokuwa na dhamana; hasa uhujumu uchumi, utakatishaji fedha au kile kinachoelezwa kuwa ni “kushiriki genge la uhalifu.”

Kana kwamba “mateso” ya kuwekwa korokoroni na hata mahabusi kwa muda mrefu hayatoshi, serikali huamua kupora fedha za watuhumiwa hao kupitia kile kinachoitwa ‘makubaliano maalum” ya kumaliza kesi nje ya mahakama kupitia kwa DPP.

Baadhi ya wachambuzi wameita hatua hii kuwa “uchochoro wa ufisadi uliotengenezewa mwanya wa kisheria.”

Mabilioni yaliyovunwa na serikali

Hadi mwanzoni mwa mwaka huu, serikali imevuna mabilioni ya shilingi kwa njia hii, huku ikilalamikiwa kuwa kwa kupitia utaratibu huo wa kuusanya mapato bila kuhusisha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni ufisadi wa watawala.

Kwa mfano, uchunguzi wa SAUTI KUBWA unaonyesha kuwa hadi Januari 2020, serikali imevuna kiasi cha Sh 290,601,582 kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu watatu tu  – Tito Magoti, Ofisa  wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC); Theodory Giyan, mtetezi wa haki ya mawasiliano anayejitegemea, na Erick Kabendera, mwandishi wa  habari za uchunguzi.

Tito na Theodory waliamuariwa kulipa Sh. 17, 354,535, huku Kabendera akitakiwa kulipa jumla ya Sh. 273,247,047. Fedha hizi ni fidia na faini. Zote tayari zimelipwa serikalini.

Tito na Theodory walihukumiwa Januari 5, 2021 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam baada ya washtakiwa hao kukiri makosa yao kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP). Kabendera alitiwa hatiani na mahakama hiyohiyo Februari 24, 2020 akitakiwa kulipa faini ya Sh. 100,000,000 na fidia Sh. 173,247,047.

Vile vile, serikali imevuna Sh. 123,327,000,000 kwa kipindi cha mwaka mmoja 2019-2020. kutokana na kesi za wafanyabiashara na wafanyakazi wa baadhi ya idara za serikali na mashirika ya umma zilizoangukia utaratibu wa kukubaliana na ofisi ya DPP.

Hizo ni pamoja na kesi iliyomkabili Harry Kitilya, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wafanyakazi wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare, Sioi Solomon, Bedason Shallanda na Alfred Misana ambao walihukumiwa kulipa faini ya Sh. 1,000,000 kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi sita jela na kila mmoja kulipa fidia ya Sh 1,500,000,000 waliyoisababisha Serikali. Walihukumiwa Agosti 25, 2020.

Mwingine aliyeingia makubaliano ya kumalizana na DPP ni mfanyabiashara wa upatu, Tariq Machibya maarufu Mr. Kuku ambaye aliamuriwa kulipa kulipa faini ya Sh. 5,000,000 au fidia ya Sh. 5,400,000,000.

Kesi nyingine iliyofikiwa makubaliano na DPP ni iliyowahusu Rais wa Migodi ya Pangea, North Mara, Exploration na Bulyanhulu, Deodatus Mwanyika na wenzake wawili ambao walikubali kulipa kulipa fidia ya Sh. 1,500,000,000 na kulipa faini ya Sh. 1,500,000 kila mmoja.

Wakurugenzi na baadhi ya watendaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Halotel waliwatia hatiani na kuhukumiwa kulipa faini ya jumla ya Sh. 24,000,000, fidia ya Sh. 42,000,000,000.

Pia wafanyabiashara wawili wa madini wa Dar es Salaam, Jamal Mohamed na Haji Hassan walihukumiwa kulipa fidia ya Sh. 40,000,000 na madini yao ya dhahabu yenye thamani ya Sh. Sh. 543,000,000.

Katika mkumbo huo, vigogo wawili wa kitengo cha uthaminishaji almasi na vito Tanzania (Tansort) kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo na Edward Rweyemamu walikiri makosa mahakama ikawatia hatiani kulipa faini ya Sh. 1,000,000 kila mmoja kutaifishwa madini waliyokutwa nayo yenye thamani ya Sh. 61,900,000,000.

Utaratibu huo pia ulikamua Sh. 207,000,000 za mfanyabiashara Abdulrahman Omary wa Dar es Salaam baada ya kukiri makosa kwa DPP.

Ofisa wa Benki ya CRDB, Andrew Babu na wenzake watatu walilazimika kulipa fidia ya Sh. 106,000,000 kwa serikali ili kukwepa mateso ya kulala korokoroni.

Raia wawili wa India, Manish Khattar na Rajesh Velram walilipa faini ya Sh. 230,000,000 baada ya kupatikana na hatia na pia mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Rajabu Katunda na mtaalamu wa mawasiliano, Baraka Mtunga walilazimika kulipa fidia ya Sh. 267,000,000 na faini ya Sh. 1,500,000 kila mmoja ili kuwa huru.

Uchunguzi wa SAUTI KUBWA umebaini kuwa sehemu kubwa ya fedha hizi zilizotoka kwa wahusika zilichotwa kwenye akaunti zao za benki. Wengine walichangishana na ndugu zao, huku wengine wakilazimika kubaki masikini kwa kuuza rasilimali zao, hasa nyumba na viwanja ili kujinusuru na kifungo magerezani au muda mrefu wa kukaa mahabusu wakisubiri hukumu za kesi zao zinazochukua muda mrefu kukamilika.

Katika makubaliano na DPP, muda mrefu wa kukamilisha malipo hao ya adhabu ni miezi tisa, huku wengi wakibanwa kumaliza kwa kipindi cha miezi sita tu.

Seth Harbinder Sing, anayeshitakiwa kwa kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha pamoja na mfanyabiashara James Rugemalira, alikataliwa kumalizana na DPP mwaka jana baada ya kujaribu kutoroka mikononi mwa Jeshi la Magereza, akiwa hospitali ya Muhimbili.

Pamoja na kuanza kwa makubaliano hayo, ambayo Rugemalira hajayaafikki hata leo, akisema anataka haki iendeke na siyo kukiri kosa wakati anaamini ana haki zote katika shauri linalomkabili na kuwa anaonewa bure na serikali ya Rais Magufuli.

Katika mazungumzo ya awali na DPP, taarifa zinaeleza kuwa Seth alikuwa tayari kulipa Sh. 15,000,000,000 ili awe huru, mchakato uliokoma baadaye.

Wanasheria, watetezi watoa kauli

“Huenda hawa wasiwe watetezi wa mwisho kukamatwa na kubambikwa kesi. Tunazo taarifa kwamba wengine bado wanafuatiliwa, hasa wale wanaokosoa utawala wa Magufuli kwenye mitandao na maeneo mengine, lakini hii siyo sawa, kwa Tanzania, nchi iliyozoeleka kuwa kitovu cha amani na haki. Sasa imegeuka kuwa pango la kuumiza raia wake,” amesema mwanasheria mmoja mwandamizi aliyeomba jina lake lisitajwe kwa sasa.

Alisema kinachofanywa na serikali ni kutisha na kuminya uhuru wa watu kukosoa serikali inayowaongoza na kwamba hatua hiyo imekuwa ikitumika kwa nchi zenye historia mbaya ya kuonea raia wake kwa kuwa tu wana mtazamo tofauti na watawala. Ameitaja Rwanda, inayoogozwa na Rais Paul Kagame kuwa moja ya nchi zenye kutesa na kuua wapinzani wa mfumo wa utawala ulioko madarakani.

Mtetezi mkubwa wa haki za binadamu nchini, Dk. Hellen Kijo-Bisimba akizungumzia hatua ya serikali kukamata wanaoonekana kuikosoa na kubambika kesi na hukumu nje ya mahakama, alisema hiyo ni njia mbaya inayobeba mazingira ya kuwafunga midomo wenye mawazo mbadala katika kuendesha nchi.

Alisema utaratibu wa watuhumiwa “kumalizana” na DPP upo nchi nyingi, lakini unaweza kutumika vibaya kuumiza wengi ambao wanakosa namna –  kwa kuwa wanateswa, isipokuwa kukiri makosa yao ili wawe huru.

Mwanasheria mwingine, Mika Maporu, akizungumzia kukamatwa na kuonewa kwa wanaoikosoa serikali inayoongozwa na Rais Magufuli alisema; “kwanza ieleweke kwamba hakuna kosa lolote kisheria kuisema serikali; iwe kwa ubaya ama uzuri wake, isipokuwa matusi yanayojenga chuki dhidi ya watendaji wa serikali linaweza kuwa kosa.”

Anasema kuwepo kwa sheria ya makubaliano na DPP iliyoanza mwaka juzi, 2019 baada ya kile kinachoitwa ushauri wa Rais Magufuli kwa vyombo vya sheria na baadaye kupitishwa na Bunge kabla ya kusainiwa na yeye – na kuanza kutumika mwaka huohuo, kumenyang’anya haki za wengi ambao wanakamatwa, lakini wanaamua tu kujiepusha na mateso ya gereza kwa kuwa mashitaka wanayopewa huchukua muda mrefu mahakama, hivyo njia ya kujiepusha ni kukiri makosa na kuingia kwenye makubaliano ya kulipa fidia.

Vifungu vya sheria ya makubaliano hayo vinaeleza kuwa baada ya pande zote zinazohusika na shauri, mahakama huelezwa hayo na hukumu hutolewa na mahakama kwa kuzingatia mkataba a mtuhumiwa na DPP.

Mwanasheria huyo anasema, amepitia hati nyingi za mashtaka na kuzungumza na baadhi ya waliokiri, lakini mazingira ya kuwatia  hatiani kimahakama yanakosa nguvu kubwa ya ushahidi, hivyo kama yangeendeshwa kwa haki mahakamani, kuna nafasi finyu ya serikali (mshitaki) kushinda.

Like
5