Timu za England zamnyemelea Mtanzania mwingine. Ni Kelvin John

BAADHI ya vilabu vikubwa vinavyoshiriki mashindano makubwa ya soka ya England, vimeanza kunyemelea saini ya mchezaji wa Tanzania, Kelvin Pius John.

Mchezaji huyo, kijana wa miaka 17 aliyezaliwa Kijiji cha Milama, Morogoro mwaka 2003, amekuwa akifuatiliwa kwa karibu na madalali wa wachezaji wanaohusishwa na timu za Arsenal, Leicester City, Manchester United na Chelsea, baada ya kuridhishwa na kiwango chake awapo uwanjani. 

Kevin kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji wanafunzi watatu wa chuo cha mpira wa miguu cha Brooke House College Football Academy kilichopo, Leicester, Uingereza ambao wamewekwa kwenye orodha kwamba “wameiva na wako tayari” kuingia mikataba na timu kubwa. Kevin anaweza kufuata nyayo za Mbwana Samatta aliyewahi kucheza timu ya Aston Villa ya Uingereza. Hivi sasa anacheza timu ya Fenerbahçe, ya Uturuki.

Wachezaji wengine walioko ubaoni pamoja na Kevin ni Jordan Neal kutoka Australia na Chinonso Emeka kutoka Nigeria.

Ndugu wa Kevin, Pius Mzeru ameiambia SAUTI KUBWA kwamba familia yao imepokea taarifa za ndugu yao kunyemelewa na vilabu vikubwa kwa furaha kuu, huku akisema “tunamuombea sana afanikiwe, kwani itakuwa shangwe, siyo kwa familia tu, bali sifa kwa Tanzania nzima.”

Kijana huyo alianza kuonekana kwa Watanzania na dunia baada ya kuwa mingoni mwa wachezaji wa Timu ya Taifa ya Vijana maarufu kwa jina la Serengeti Boys, ambapo uchezaji wake ulivutia wengi, akiwamo aliyekuwa kocha wa Timu ya Taifa, Taifa Stars, Emmanuel Amunike ambaye alifananisha uchezaji wake na Kylian Mbappé wa Ufaransa. Mbappé ni miongoni mwa wachezaji wanaolipwa fedha nyingi zaidi duniani. Hivi sasa Mbappé ni mchezaji wa timu ya  PSG anakolipwa jumla ya Sh. 1,080,000,000 kwa wiki.

Mwishoni mwa mwaka jana gazeti kubwa duniani la The Guardian la Uingereza, lilimtaja Kevin kuwa ni mchezaji mdogo anayeinukia na kwamba ni miongoni mwa vijana wanaoweza kuishangaza dunia kwa umahiri wao wanapokuwa uwanjani wakisakata kabumbu.

Kelvin anayetumia zaidi mguu wa kulia, alifanya vizuri kwenye mashindano ya mataifa ya Afrika ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U-17) mwaka 2019 ambapo alionyesha uwezo wake usiotiliwa shaka anapokuwa uwanjani.

Kevin anacheza nafasi ya kiungo wa kati, ingawa wachambuzi wa soka wanaeleza kuwa anaweza kuwa mfungaji mzuri endapo atapata maelekezo kutoka kwa makocha bora.

SAUTI KUBWA inamtakia kila jema Kevin katika safari yake ya kuingia kwenye “ulimwengu wa soka kubwa” huko Uingereza au mahali pengine atakakokuwa.

Like
5