Samia amefunika kombe mwanaharamu apite

WAPENDA demokrasia nchini kote na hasa wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo Ijumaa Machi 4, 2022 wanaweza kujihisi kuwa na furaha kuu kutokana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuamua kuiondoa mahakamani  bila masharti kesi ya ugaidi iliyokuwa ikimkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wenzake watatu – Mohamed Ling’wenya, Halfan Bwire na Adam Kasekwa. 

Awali Februari 18, 2022 Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ilisema wana kesi ya kujibu baada ya upande wa mashitaka kufunga ushahidi wao mbele ya Jaji Joachim Tiganga aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo.

Kesi hii imekuwa na mjadala mkubwa katika jamii ya Kitanzania, kimataifa kiasi cha kuibua hisia kwamba ilikuwa imechochewa kisiasa ili kuvunja nguvu Chadema ambao mwaka jana walianza vuguvugu kubwa la kudai katiba mpya nchini.

Jaji Tiganga alikuwa jaji wa tatu kusikiliza kesi hiyo baada ya wengine wawili kujitoa katika kuisikiliza. Awali mmoja alikataliwa na washitakiwa na wa pili alitaja majukumu mengi kuwa sababu ya kushindwa kuendelea na kesi hiyo.

Kesi hii ilikuwa na msisimko mkubwa kwa wananchi kwani ilikuwa inafuatiliwa kwa karibu sana na watu wengi.

Ilikuwa ikiripotiwa na mitandao ya kijamii kama vile iko live, kiasi kwamba umma ulijiona kama vile uko mahakamani kusikiliza na kufuatilia kesi hiyo.

Swali kuu la kujuliza, je, furaha hii ina maana gani? Ni kweli Mbowe na wenzake wako huru. Lakini, kuwa huru huku wakati mahakama ilikuwa imekwisha kusema wana kesi ya kujibu bila kwanza kusikiliza utetezi wao kunalenga nini?

Je, kwa Mwendesha Mashitaka wa Serikali yaani Mkurugenzi (DPP) kutumia kifungu cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kifungu cha 91 (1), kwa nini kuibuke baada ya Jaji kuwa ametamka washitakiwa wana kesi ya kujibu? Kwamba wameondoa mashitaka, lakini je, nini majaliwa ya washitakiwa juu ya tuhuma hizi mbele ya safari kisiasa na kijamii?

Je, kwa nini Jamhuri pamoja na ushahidi wote uliokuwa unawasilishwa mahakamani kuonenakana mwepesi tangu awali, tena ni wa kuumba, kiasi cha mashahidi wa kugongana wenyewe katika walichowasilisha na hata ilipoonekana dhadhiri kwamba tarehe za kufunguliwa kwa upelelezi na madai ya watuhumiwa kupanga ugaidi vilikuwa vinagongana mno, bado iling’angana na kesi hii ambayo sasa imeacha aibu kuu mbili.

Moja aibu dhidi ya Jeshi la Polisi na pili aibu kwa majaji waliosikiliza kesi hii kwa nyakati tofauti? 

Ni jambo la kufurahia kwamba Mbowe na wenzake wako huru leo, lakini nani hasa analipa gharama ya mateso na muda waliopoteza wakiwa mahabusu wakiendelea na hii kesi ya aibu kuu kwa taifa?

Nani hasa atawajibika kwa madhila ya watuhumiwa walioteshwa na kushinikizwa kukubali kukiri makosa yao? Je, hizi gharama za kesi nani anabeba. Jaji kutoka Mwanza na kukaa Dar es Salaam siku zote hizo?

Mawakili wa serikali waliokusanywa katika mikoa tofauti nao kugharimiwa na serikali kwa sababu tu ya kesi iliyoumbwa na Ramadhani Kingai na wenzake kwa sababu zao wanazozijua?

Wakati wapenda demokrasia wakisherehekea kuachiwa huru kwa Mbowe na wenzake, hawana budi kusherehekea kwa hadhari kubwa.

Juzi Bunge limefanya marekebisho ya sheria ya ugaidi. Yapo mambo ambayo hapo awali yalikuwa hayatambuliki kama ni ugaidi. Kwa mfano katika marekebisho ya sheria hiyo sasa maandamano yoyote yakifanyika na akafa mtu, basi maandamano hayo ni ugaidi. Kutishia mtu kwa maneno nayo sasa ni ugaidi.

Kwa kifupi kesi ya Kina Mbowe ilitoa darasa kwa Jamhuri kwenda kuisuka upya sheria ya ugaidi na kwa maana hiyo kuweka wanasiasa kwenye mtego mgumu sana wafanyapo siasa.

Kwa maneno mengine kipigo ambacho mawakili wa Jamhuri walikumbana nacho mahakamani juu ya mambo ya ugaidi, sasa yamesaidia serikali kwenda kuirekebisha sheria ya ugaidi kiasi cha kuifanya kuwa mbaya zaidi dhidi ya uhuru wa kujieleza, kukusanyika na maoni.

Kubwa zaidi ya yote, wakati Mbowe na wenzake wakiwa uraiani leo, ni vema tukajiuliza kwa nini Jamhuri ikafunga milango yote kupitia mahakama ya washitakiwa hawa kuutikisa ushahidi uliokuwa umewasilishwa mahakamani, hivyo kuunyima umma fursa ya kujua ukweli wa kiini cha mashitaka haya? 

Hapa Jamhuri aimefunika kombe mwanaharamu apite. Imechutama. Lakini ikiwa imechelewa sana. Ilikwisha kujianika hadharani siku nyingi. 

Katika kutafakari maswali haya, je, umma bado unakumbuka kwamba mwaka 2020 ulifanyika uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge uliokuwa ‘kituko’ cha karne?

Ni kwa kiwango gani kesi ya kina Mbowe imesaidia ama kuzuia au kuahirisha hoja mbalimbali ndani ya jamii juu ya uchaguzi huo?

Na sasa Jamhuri inaweza ikainua mabega na kusema kuwa imetafakari na kuona kwamba kesi hiyo haikuwa na maslahi ya umma. Kwa maana hiyo ikapata pongezi mbele ya jamii ya Kitanzania na ile ya Kimataifa? 

Ni haki na vema kabisa umma kushangilia kuachiwa huru kwa kina Mbowe bila masharti. Ni jambo la kupendeza sasa atapata fursa ya kuendelea kujenga chama chake kuelekea 2025, lakini umma usiache kuhoji Jamhuri ilifikiri nini hata ikaruhusu mashitaka ya ovyo kufikishwa mahakamani?

Iliwaza nini hata kuruhusu Jeshi la Polisi kujitumbukiza katika aibu hii ambayo imechafua sana taswira ya taifa letu kote duniani, kwamba Jamhuri ina la kujifunza juu ya mwenendo wa Jeshi la Polisi kwa nia ya kuligeuza kuwa chombo cha kulinda raia na mali zao na siyo chombo cha kutunga na kubambika watu kesi za ovyo kama hii ya kina Freeman Mbowe na wenzake? 

Hakika tufurahie Mbowe na wenzake kuwa huru, lakini wote waliohusika kutengeneza kesi hii wazomewe na wajisikie vibaya kwamba dhamana walizopewa wamezitumia kuidhalilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kote duniani. Aibu!

TAZAMA UCHAMBUZI KATIKA VIDEO YETU HAPA

Like
5