Sakata la Mbowe: Ni mkakati wa Ikulu, Usalama na Sabaya

IMEBAINIKA kuwa mashitaka ambayo Jeshi la Polisi linajaribu kumtengenezea Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, yana mkono mrefu wa Ikulu.

Taarifa za uhakika ambazo SAUTI KUBWA imezipata kwa vyanzo mbalimbali kutoka serikalini, jeshi la polisi na wastaafu wanaoaminika, zinasema kuwa “kinachotokea sasa ni matokeo ya mkakati wa muda mrefu tangu Mbowe alipofanikiwa kutolewa gerezani baada ya wananchi kuchanga mamilioni ya shilingi dhidi ya hukumu ya uonevu iliyokuwa imewatia hatiani yeye na viongozi waandamizi wa Chadema.”

“Hasira za rais zilihamishiwa katika kuunda kesi mpya ya kummaliza kabisa. Ndiyo hii,” kilisema chanzo chetu.

Uchunguzi wa SAUTI KUBWA umebaini kuwa mkakati wa kumtengenezea Mbowe “kesi mbaya” uliratibiwa na Idara ya Usalama wa Taifa iliyokengeuka, kwa maagizo ya rais, na kwa usaidizi maalumu wa Lengai ole Sabaya, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoa Kilimanjaro kwa shabaha ya “kummaliza Mbowe” ili aache kusumbua serikali.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza, mkakati huo uliodhaniwa kufika mwisho kutokana na kifo cha Rais John Magufuli mwezi Machi 17 mwaka huu, umeendelezwa na mrithi wake, Rais Samia.

Vyanzo vyetu ndani ya serikali, jeshi la polisi na Chadema vimethibitisha kwa nyakati mbalimbali kuwa Samia amerithi mkakati huu kutoka kwa mtangulizi wake, na jeshi la polisi linatumia mwanya huu kama mbinu ya kuzima harakati za Chadema kudai katiba mpya, kwa maelekezo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

SAUTI KUBWA ina taarifa kwamba Ikulu ilisuka mpango wa kumhusisha Mbowe na  ugaidi kwa kutumia baadhi ya maofisa wa idara za usalama za Tanzania wakisaidiwa kwa karibu na Sabaya ambaye alifanya jitihada binafsi za kuhusisha walinzi binafsi wa Mbowe ili “wamgeuke na kumchoma” kwa tuhuma za kutunga.

Baada ya Sabaya kutumia nguvu ya fedha na madaraka kuwashawishi wakagoma kumsaliti Mbowe, aliamua kutumia mabavu kuwatisha na kuwatesa lakini walikataa.

Ndipo walipochukuliwa na kufikishwa mahakamani wakifuguliwa mashitaka yasiyokuwa na dhamana. Sasa Jeshi la polisi linatafuta jinsi ya kumuunganisha Mbowe katika kesi hiyo namba 63 ya 2020.

Walinzi hao wa Mbowe wapo katika magereza ya Ukonga na Segerea, Dar es Salaam.

Sabaya anakabiliwa kwa kesi zenye mshitaka ya matumizi mabaya ya madaraka, wizi wa kutumia silaha.

Mstaafu mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina amesema: “Tulidhani taifa limeanza kupona, kumbe bado; polisi wametekeleza mkakati wao katika mazingira ambayo yanaifanya serikali yote ionekane si makini, ni ya uonevu na ukatili. Na kila mwenye kuelewa anajua kuwa hawa wametumwa tu, na wamekosa mashitaka yenye mashiko dhidi ya Mbowe. Wanamvua nguo rais…”

Wanasheria wanaingilia kati

WANASHERIA mahiri kadhaa nchini wameamua kufungua kesi Mahakama Kuu kushinikiza serikali imfikishe mahakamani Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, akiwa hai au amekufa ili haki itendeke.

Mbowe anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa zaidi ya saa 96 sasa (zaidi ya siku 4) kinyume cha sheria za Tanzania zinazotaka mtuhumiwa afikishwe mahakamani ndani ya saa 48 baada ya kukamatwa.

Ingawa Jeshi la Polisi limekataa kuweka wazi mahali alipo Mbowe, SAUTI KUBWA inaweza kueleza kwa uhakika kwamba kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani amefichwa katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam.

Mbowe alikamatwa jijini Mwanza usiku wa manane Jumatano iliyopita baada ya kuvamiwa na polisi akiwa hotelini, wakamteka, huku wakimlazimisha “kubeba kila alichonacho” na kuondoka naye.

Taarifa za uhakika ambazo SAUTI KUBWA imezipata usiku huu, zinaeleza kwamba Mbowe “amefichwa” kituoni hapo na kwamba kuna usiri mkubwa wa kuwepo kwake hapo.

Baada ya taarifa zake kukosekana huku polisi wakizuia wanafamilia na wanachama kumtembelea au kumpelekea chakula, kumekuwapo na tetesi kuwa amesafirishwa kwenda Mwanza. Hata hivyo, vyanzo vyetu vya kuaminika vimetuhakikishia kuwa hadi jioni ya Jumapili hii alikuwa Dar es Salam, kinachosubiriwa sasa ni uamuzi wa wakubwa ili kujua mahali pa kumpeleka.

Tayari Jeshi la Polisi limeeleza kwa umma kwamba litamfikisha Mbowe mahakamani kwa tuhuma za ugaidi na kupanga njama za kuua viongozi wa serikali, bila kutaja viongozi hao ni nani, wako wapi na wala madaraka yao.

Kufuatia kukamatwa kwa Mbowe na kuendelea kushikiliwa bila kufikishwa mahakamani, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kimeingilia kati na kutaka aachiliwe au afikishwe mahakamani.

Msimamo wa TLS umetolewa leo  Jumapili  Julai 25, 2021 na Rais wa TLS, Dk. Edward Hoseah  katika tamko lake lililosambazwa kwa umma.

Akinukuu Katiba ya Tanzania, Dk Hoseah amesema Ibara ya 21(1) inatoa haki ya kujumuika na Ibara ya 13(1) inatoa masharti ya watu wote kuwa sawa mbele ya sheria. 

Dk. Hoseah ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), amesema kitendo cha kumkamata usiku wa manane Mbowe na wenzake, kwa sababu ya kuandaa kongamano ni ukiukwaji wa Katiba na sheria za nchi.

Akizungumzia kuandaa kongamano, Dk. Hoseah amesema haijawahi kuwa kosa la jinai kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi. Amefafanua kuwa ikiwa kuna tuhuma nyingine dhidi yake bado kwa sheria za nchi alipaswa kufikishwa kwenye mamlaka za kisheria mapema.

“Natoa mwito kwa mamlaka kumwachia huru kwa sababu kuendelea kumshikilia ni kukiuka utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa sheria.

Mbowe na baadhi ya viongozi wa Chadema walikamatwa Julai 21 jijini Mwanza wakati wakijipanga kufanya kongamano la Katiba lililopigwa marufuku jijini humo.

Hata hivyo, Mbowe alisafirishwa kutoka Mwanza kuja Dar es Salaam ambako alipekuliwa nyumbani kwake, huku taarifa iliyotolewa na Polisi juzi ikieleza kuwa Mbowe alikamatwa akihusishwa na makosa ya ugaidi na njama za kutaka kuua viongozi wa Serikali.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu anayeishi nchini Ubelgiji, alisema tuhuma hizo ni hujuma za kisiasa zinazofanywa na Serikali ya CCM.

“Makosa hayo ni mlolongo mrefu wa makosa ya kubambika ya jinai ambayo Mbowe na viongozi wake kwa sababu tu ya kuwa viongozi wa Chadema wanapewa.

“Ni mlolongo wa vita dhidi ya Chadema inayoendeshwa na CCM na Polisi na vyombo vya usalama. Ni vita ya kisiasa,” alisema Lissu.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime akizungumza kuhusu tuhuma za Mbowe, alikataa kueleza kwa undani, akidai kuwa maswali mengi anayoulizwa majibu yake anaweza kuingilia ushahidi katika kesi hiyo.

Kuhusu kukamatwa usiku wa manane kinyume cha sheria, Misime alisema Tanzania haina sheria inayosema mtu asikamatwe usiku – “wakati wowote tunapojiridhisha na ushahidi wetu tutamkamata mahali popote.”

Lissu amekosoa ukamataji na upekuzi uliofanywa nyumbani kwa Mbowe akisema; “Upekuzi wa Mwenyekiti umefanyika usiku, sheria za Tanzania zinasema searching zifanyike mchana.”

Hata hivyo, akijibu madai hayo Kamanada wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alikanusha akisema kama kuna malalamiko ya mchakato mzima wa ukamataji yapelekwe mahakamani.

“Ni sheria gani iliyosema usiku mtu hapekuliwi? Usiku hakuna makosa? Kwa hiyo ukiambiwa kuna mali ya wizi iko sehemu fulani, ukapekue asubuhi ili ukute imehamishwa?”

Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kifungu cha 40, upekuzi hufanywa mchana usipokuwa kwa idhini ya mahakama.

Jamii ya kimataifa inamulika Tanzania kwa “jicho pana” kujua hatima ya Mbowe ambaye wachambuzi wengi wanasema amekamatwa kwa maagizo ya kisiasa kwa sababu ya hofu za watawala kwa lengo la kufifusha mjadala wa katiba mpya na kudhoofisha Chadema.

Like
8