Sabaya atisha waandishi wa habari akiwa rumande

WAANDISHI wa habari watatu wanaofuatilia na kuandika zaidi habari za aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya (34) na walinzi wake watano, wanaoendelea kushikiliwa mahabusu, wametishiwa maisha.

SAUTI KUBWA ina taarifa kuwa waandishi hao – Mussa Juma (Mwananchi), Sechelela Kongola (TBC) na Asraj Mvungi (ITV) – wamepigiwa simu kutoka kwa watu wasiowatambua wakiwataka kuacha kuandika habari za Sabaya.

“Tangu kuanza kwa Sakata la Sabaya kukamatwa na Takukuru (Taasisi ya Kupambana na Kuziua Rushwa), nami kuanza kandika habari zake gazetini, ninapigiwa simu kwa njia ya namba za simu za watu nisiowajua, wananitisha na kunitaka niache kuandika habari hizo,” amesema mmoja wao.

Alisema kwamba wanaompigia simu ni watu tofauti na wanatumia namba tofauti wakisema, “tunakuomba uache, tutakupoteza.”

Imebainika kuwa wanaopiga simu kwa waandishi hao ni watu walewale na kwa kutumia namba zilezile. (Namba hizo zinahifadhiwa kwa sababu uchunguzi bado unaendelea).

Tayari waandishi wawili kati ya watatu wameripoti tukio hilo kituo cha Polisi na kwamba jeshi hilo limeanza kufuatilia kujua wanaohusika na jambo hilo.

SAUTI KUBWA kwa sasa haiwezi kuandika majina yao wala vyombo wanavyofanyia kazi kwa sababu ya usalama wao. Pia namba zinazotumika hazitatajwa ili kutooharibu uchunguzi wa Polisi.

Kufuatia vitisho hivyo, Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC), kimetoa tamko kulaani vitisho hivyo na kuwataka wanaofanya uhalifu huo kuacha mara moja.

Mwenyekiti wa APC, Claud Gwandu, katika tamko hilo lilifikia SAUTI KUBWA leo jioni, ameeleza kwamba mbali na vitisho hivyo kwa njia ya simu, baadhi ya watu ambao hawajitambulishi wamefika mara tano nyumbani kwa mwandishi na kuuliza watu wa familia yake kuhusu alipo na kutaka kuelezwa muda anaorejea numbani.

Gwandu ameeleza kwamba tayari suala hilo limewasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella ambaye ameanza kuchukua hatua kwa kuliagiza Jeshi la Polisi kuchunguza haraka.

Sabaya na watu wengine watano wanaodaiwa kuwa walinzi wake walifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha Juni 4, mwaka huu wakikabiliwa na makosa mbalimbali yakiwamo ya  uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kupokea rushwa.

Sabaya ambaye alisimamishwa na Rais Samia Suluhu Hassan Mei 13, 2021 kupisha uchunguzi, alifikishwa mahakamani hapo akiwa amefungwa pingu na baada ya wote kushuka kwenye magari ya polisi, walitakiwa kuchuchumaa na kisha kupelekwa katika chumba maalum na baadaye kuingizwa mahakamani.

Waendesha mashtaka wa Serikali, Tumaini Kweka, Abdallah Chaula na Tresla Garvas mbele ya Hakimu Mfawidhi, Martha Mahumbuga na Hakimu Mkazi Mkuu, Salome Mshasha wamesema Sabaya na wenzake walitenda makosa hayo Januari 20 na Februari 9, 2021.

Kweka alisema  Sabaya na wenzake watano anatuhumiwa kwa makosa ya kuunda genge la uhalifu, uhujumu uchumi,  kujipatia fedha kwa njia ya rushwa na utakatishaji fedha ambapo Sabaya alijipatia Sh. milioni 90 kutoka kwa mfanyabiashara, Francis Mroso mkazi wa kwa Mromboo ambaye alikuwa anatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi ili amsaidie jambo ambalo ni makosa.

Pia, Sabaya na walinzi wake wawili, Sylivester Nyengu (26) maarufu kicheche na Daniel Mbura (38) wanakabiliwa na  makosa mawili ya ujambazi wa kutumia silaha wakidaiwa kuyatenda Februari 9, 2021.

Like