Chipukizi Kelvin John afuata rasmi nyayo za Samatta. Asajiliwa na KRC Genk ya Ubelgiji

MWANASOKA chipukizi wa Tanzania, Kelvin John – maarufu kwa jina la kisoka ‘Mbappe,’ sasa amejiunga rasmi na klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.

SAUTI KUBWA ambayo imekuwa ikimfuatilia kwa karibu imedokezwa kwamba Kelvin amesaini mkataba wa miaka mitatu kuichezea klabu hiyo ambayo nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta, aliwahi kuichezea kabla ya kujiunga na Aston Villa ya nchini Uingereza.

Kelvin ambaye amekuwa katika mafunzo zaidi ya kukuza kipaji chake, alitia Saini hiyo jana na kwamba uongozi wa Genk umeeleza kufurahishwa na kiwango cha kijana huyo ambaye pia anaichezea timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Ngorongoro Heroes ya Tanzania.

Habari zinaeleza kwamba mchakato wa kusajiliwa kwa Kelvin kumewezeshwa na ushawishi wa Samatta ambaye alianza ‘kumpigia debe’ kijana huyo baada ya kuona kipaji chake anapokuwa uwanjani.

Mchezaji huyo kijana wa miaka 17 aliyezaliwa Kijiji cha Milama, Morogoro mwaka 2003, alikuwa akifuatiliwa kwa karibu na madalali wa wachezaji wanaohusishwa na timu za Arsenal, Leicester City, Manchester United na Chelsea, baada ya kuridhishwa na kiwango chake awapo uwanjani.

Kevin alikuwa miongoni mwa wachezaji wanafunzi watatu wa chuo cha mpira wa miguu cha Brooke House College Football Academy kilichopo, Leicester, Uingereza ambao wamewekwa kwenye orodha kwamba “wameiva na wako tayari” kuingia mikataba na timu kubwa. Kevin anaweza kufuata nyayo za Mbwana Samatta aliyewahi kucheza timu ya Aston Villa ya Uingereza. Hivi sasa anacheza timu ya Fenerbahçe, ya Uturuki.

Like
2