Ronaldo: Nimerejea Man United kuandika historia tena

TAYARI Cristiano Ronaldo (36) ametangazwa rasmi kama mchezaji mpya wa klabu ya soka Manchester United ya England.

Hii imekuja baada ya klabu ya Manchester United na Juventus kukubaliana kwa dau la Euro milioni 15, ambazo zitalipwa kwa awamu ndani ya miaka mitano lakini pia dau hilo linaweza kuongezeka kwa Euro milioni 8 zaidi kulingana na uwezo wa mchezaji.

Baada tu ya kutangazwa kama mchezaji wa Manchester United, Ronaldo aliandika katika kurasa zake za Facebook na Instagram, akisema:

“Wote wanaonifahamu, wanaufahamu upendo usio na mwisho ambao ninao kwa Manchester United. Kipindi chote nilichoitumikia klabu hii, kilikuwa kipindi kizuri sana na njia tuliyoitengeneza kwa pamoja iliandikwa kwa herufi za dhahabu katika historia ya taasisi hii kubwa.

“Ni vigumu kuelezea hisia zangu kwa sasa, hasa ninapoona kurejea kwangu Old Trafford kukitangazwa dunia nzima, ni kama ndoto kuwa kweli, kwani hata pale nilipokuwa nikicheza dhidi ya Manchester United kama mpinzani, bado mashabiki waliniheshimu na kunionyesha upendo wa hali ya juu sana. Hakika haya ndiyo mambo yanayotengeneza muono!

“Ligi yangu ya kwanza ya ndani, taji langu la kwanza, kuitwa kwa mara ya kwanza kwenye timu ya taifa (Ureno), mchezo wangu wa kwanza katika ligi ya mabingwa Ulaya, kushinda kiatu cha kwanza cha dhahabu, na tuzo yangu ya kwanza ya mchezaji bora wa dunia (Ballon d’Or); mambo yote haya yalipatikana kutokana na muunganiko maalumu kati yangu na mashetani wekundu. Historia iliandikwa kipindi cha nyuma na ninawaahidi kuwa historia itaandikwa kwa mara nyingine.

“Niko hapa! Nyumbani! Tuendeleze pale tulipoishia! Sir Alex, hii ni kwa ajili yako.”

Cristiano anatarajiwa kuvaa jezi namba 7 ambayo ilikuwa ikivaliwa na Edi Cavani (El Matador), huku Cavani akipewa jezi namba 21, iliyokuwa ikivaliwa na Daniel James ambaye ametimkia Leeds United.

Je, kwa umri wa Cristiano, tutarajie makubwa katika ligi kuu ya England? Au kaja kustaafu tu?

Like
1