CRISTIANO Ronaldo ameisababishia kampuni ya Coca-Cola hasara ya dola za Kimarekani bilioni 4 kutokana na kitendo chake cha kuziweka kando chupa za soda za kampuni hiyo na badala yake kuweka chupa ya maji wakati akiongea na vyombo vya habari Jijini Budapest.
Kama hiyo haitoshi, mchezaji huyo ambaye ni mshindi wa tuzo za Balon’dor mara tano, alinukuliwa akisema “kunyweni maji.”
Nguli huyo wa soka duniani, anayekipiga katika klabu ya Juventus ya nchini Italia, anatambuliwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa bora zaidi duniani sambamba na Muargentina Lionel Messi.
Ronaldo aliondosha chupa mbili za soda ya Coca-Cola zilizokuwa mbele yake na kuweka chupa ya maji. Kampuni ya Coca-Cola inadhamini mashindano ya Euro 2020, ambamo timu ya taifa ya Ureno inshiriki huku ikiongoza na Cristiano kama nahodha.
Gazeti la Uhispania Marca, liliripoti kuwa hisa za kampuni ya Coca-Cola ziliporomoka ghafla baada ya tukio hilo na hivyo kupelekea hasara ya mabilioni.
“Hisa za kampuni ya Coca-Cola zimeporomoka kutoka dola za Kimarekani 56.10 hadi 55.22 muda mfupi baada ya kitendo cha Ronaldo. Maana yake ni kwamba thamani ya kampuni hiyo imeshuka kutoka dola za Kimarekani bilioni 242 hadi bilioni 238,” ilidai ripoti kwenye gazeti la Marca.
Anguko hilo la thamani ya kampuni hiyo, lilitokea ndani ya nusu saa baada ya tukio hilo kutokea.
Jambo hili halikuwashangaza wengi kutokana na Cristiano mar azote kuunga mkono mlo sahihi na pamoja na tukio la kukasirishwa na motto wake mkubwa, Cristiano Jr pale amkutapo akila vyakula kama hivyo ambavyo yeye huviita ‘vyakula vya hovyo.’
Mara kadhaa mwanangu (Cristiano Jr) hutumia kinyaji cha Coca-Cola au Fanta na viazi vya kukaanga, anajua vyema kuwa sipendezwi na tabia hiyo,” Ronaldo aliwahi kusema hivyo siku za nyuma.
Siku moja baada ya kusababisha madhila hayo kwa kampuni ya Coca-Cola, Ronaldo aliipaisha timu yake ya Ureno kwa ushindi wa bao tatu dhidi ya timu ya taifa ya Hungary, kwa kuifungia timu yake mabao mawili.
Pia ameendeleza ubabe wake zaidi kwa kuwa mchezaji mwenye mabao mengi zaidi katika historia ya mashindano hayo kwa kufikisha mabao 11.