Sergio Ramos Kuondoka Real Madrid

BEKI ‘kisiki’ wa klabu ya Real Madrid na timu ya Taifa ya Uhispania Sergio Ramos (35), anatarajiwa kuondoka kwenye klabu yake hiyo baada ya kandarasi yake kufika mwisho msimu uliopita.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, hadi sasa, beki huyo wa kati ametumikia klabu hiyo kwa miaka 16 na anatarajiwa kuthibitisha uamuzi wake huo kwenye mkutano na waandishi wa habari Jumanne wiki ijayo.

Waraka kutoka kwenye klabu ya Real Madrid uliotolewa Jumatano wiki hii, ulisema: “Timu ya Real Madrid inatangaza kuwa kesho Jumatano ya tarehe 17 majira ya saa saba na nusu mchana, tafrija ya kitaasisi ya kumuaga nahodha wetu Sergio Ramos na tafrija hiyo itaongozwa na Rais wa klabu, Florentino Perez. Na baada ya hapo, Sergio Ramos ataongea na vyombo vya habari.”

Nini hatma ya Ramos?

Mpaka sasa, anahusishwa na timu za Paris Saint-Germain ya nchini Ufaransa pamoja na Manchester United ya Uingereza. Lakini pia kuna tetesi zinazodai kuwa huenda akajiunga na Ligi ya Uchina (Chinese Super League).

Ingawa mpaka sasa beki huyo ana umri wa miaka 35, bado anao uwezo wa kutandaza kabumbu safi kabisa, licha ya majeruhi aliyoyapata kwenye msimu uliopita, yaliyomuweka nje ya dimba kwa muda wa wiki kadhaa. Na ni kutokana na majeraha hayo yaliyopelekea asiitwe kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uhispania kwa ajili ya mashindano ya Euro 2020.

Baada ya kumuacha beki huyo, kocha wa timu ya taifa ya Uhispania Enrique alisema, “Ramos hajaweza kumalizia msimu kutokana na majeraha na hivyo alishindwa kufanya mazoezi na kikosi cha timu ya taifa. Ulikuwa ni uamuzi mgumu sana kumuacha na nilishauri kwamba baada ya kupona, angejiunga na kikosi cha timu ya taifa lakini haijawezekana.”

Like