Profesa Lumumba asema msimamo wa Magufuli kuhusu Corona ni ushirikina

PROFESA Patrick Lumumba, mwanazuoni wa Kenya ambaye kwa miaka kadhaa amekuwa swahiba na mtetezi mkubwa wa Rais John Magufuli, sasa amemgeuka. Ametofautiana naye katika msimamo juu ya maambukizi ya virus vya Corona.

Prof. Lumumba amekuwa akitumia mihadhara yake kadhaa kumpamba Rais Magufuli akisema ni mfano wa kuigwa katika Afrika. Amekuwa akimsifu rais huyo wa Tanzania kwamba ni mkweli, mwenye misimamo na anapenda nchi yake – ingawa misimamo mingi ya Rais Magufuli imekuwa ya “ajabu ajabu,” hasa kuhusu demokrasia, uhuru wa watu, na maambukizi na chanjo ya Corona.

Akizungumza na Watetezi TV jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita Prof. Lumumba alisema kuamini kwamba Mungu ameondoa Corona Tanzania – kama ambavyo Rais Magufuli alisisitiza mara nyingi – ni ushirikina. Prof Lumumba amesema kuwa sala bila kujali sayansi (hasa katika kukabiliana na magonjwa) ni ulozi.

Tangu Juni 2020, Rais Magufuli alitangaza kuwa Mungu ameondoa Corona Tanzania, na mekuwa akipinga taratibu na maelekezo ya kisayansi ya kuepuka Corona hadi majuzi alipolazimika kufuata msimamo wa maaskofu baada ya mfululizo wa vifo vingi vinavyosababishwa na Corona.

Prof. Lumumba, mwanasheria na mhadhiri mahiri, amesema sayansi ndiyo msingi wa kutatua matatizo ya kisayansi, ikiwamo afya, na kwamba kuamini sala pekee ni kutafuta majanga zaidi.

Lumumba pia amepinga watu wanaotaka Rais Magufuli aongezewe muda wa kuongoza kama ambavyo dalili zimeanza kujionyesha. Alisema wanaopigania Magufuli aongezewe muda ni “wahuni.”

“Namshauri Rais Magufuli awakemee wahuni hawa wasivunje utaratibu uliokuwepo muda wote, akatae wahuni hawa,” anaongeza Prof. Lumumba na kueleza kwamba anaamini Rais Magufuli hatakubali matakwa ya “wahuni” wanaotaka abaki madarakani.

Hata hivyo, wakati akihitimisha mahojiano yake, alisema Rais Magufuli anaingia katika orodha ya viongozi wa Afrika ambao anawapenda na kushabikia kwa misimamo yao.

(Prof. Lumumba)

Like