Kijazi alimnusuru Majaliwa kufukuzwa uwaziri mkuu kwa sababu ya korosho

KAMA si ushauri wa Balozi John Kijazi, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, ambaye aliaga dunia siku chache zilizopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikuwa afukuzwe kazi kutokana na msimamo wake juu ya sakata la korosho kutofautiana na wa bosi wake mwaka 2018.

SAUTI KUBWA imeelezwa kuwa Rais Magufuli alikuwa ameshaamua kumfukuza Majaliwa, akikasirishwa na msimamo wake na baadhi ya wabunge watokao Kusini, waliokuwa wanapinga hatua ya serikali kukwapua pesa za mfuko wa korosho na kupangia wakulima masoko na bei elekezi.

Mazingira haya ndiyo yalisababisha hasira za Rais Magufuli hata akatishia kupiga shangazi za waliokuwa wanapanga kuandamana, akisisitiza kwa kauli ya kibabe kuwa angeanza na “shangazi wa waziri mkuu.”

Mbali na Majaliwa, mwingine aliyekuwa na msimamo dhidi ya uamuzi wa rais ni George Mkuchika, Waziri wa Utumishi na Utawala Bora. Wote ni wenyeji wa mikoa ya kusini – Lindi na Mtwara – inakolimwa Korosho kwa wingi.

Majuzi, katika salamu zake wakati wa kuaga mwili wa Balozi Kijazi Dar es Salaam, Rais Magufuli aligusia pia suala hili, akisema baadhi ya viongozi wanaendelea na nafasi zao kwa kuwa Kijazi “alimzuia kuwafukuza.” Hakuwataja majina.

“Kijazi alikuwa mshauri wangu. Kuna kipindi nilitaka kutumbua baadhi ya viongozi wakubwa, lakini alikuwa akiniambia nisubiri kwanza, na pengine kuniambia niache hadi siku inayofuata na nikirudi kweli nabadili msimamo wangu,” alisema Rais Magufuli.

Sakata la ununuzi wa zao la korosho nchini Tanzania lililoibuka mwishoni mwa mwaka 2018, lilileta mtafaruku, si kwa viongozi wakuu tu, bali hata kwa wananchi na wabunge kuhusu bei na mnyororo wa ununuzi.

(Mkuchika)

Majaliwa na Mkuchika ulikuwa walitaka kila mkulima auze anakotaka na kwa bei anayopenda. Rais Magufuli aliweka bei elekezi kwamba iwe Sh. 3,300 na inuulie na serikali.

Hata hivyo, licha ya majigambo ya rais kwamba serikali ilikuwa na uwezo wa kuzinunua zote, na kwamba zinatakazobaki zitabanguliwa hata kwa meno, serikali ilishindwa kununua korosho. Na jeshi ambalo Magufuli alilipatia jukumu la ununuzi – ili kutisha wakulima na wabunge – lilishindwa kuzinunua na likaingia katika mgogoro na wakulima.

Hata kampuni moja ya Kenya iliyopewa tenda na serikali kinyemela ili inunue korosho hizo, baadaye iligundulika kuwa ya kitapeli. Msimamo wa Magufuli uligeuka kashfa kwa serikali.

Wakulima walisita kuuza korosho zao kwa serikali wakiamini kuwa watacheleweshewa malipo au kutolipwa kabisa, licha ya kutangaziwa bei kubwa kuliko ya wafanyabishara binafsi.

Baada ya uamuzi wa Rais Magufuli kupita, wabunge nao walijadili sakata hili Bungeni jijini Dodoma huku baadhi yao wakihoji kuwa kwanini ununuzi wa zao hilo linafanywa tofauti na agizo la Raisi John Magufuli aliyeagiza linunuliwe kwa bei ya Sh. 3,300 tofauti na ilivyokuwa ambapo wakulima wa zao walilipwa Sh. 2,600 huku wengine wakicheleweshewa malipo yao.

Wakulima wa korosho walidhamiria kuandamana ili serikali iwaache waamue wanachotaka kuhusu korosho zao. Baada ya tishio la Magufuli “kupiga shangazi” zao akianza na shangazi wa waziri mkuu, hakuna mwananchi aliyendamana.

Baadhi ya wananchi, hasa wachambuzi, walisema kauli ya Magufuli ni mwendelezo wa maneno yake ya udhalilishaji wa akina mama.

Like
3