Polisi Tanzania wadhalilisha wanawake wakiwa mahabusi

JESHI la Polisi nchini Tanzania limeingia katika hatua mpya ya uonevu na udhalilishaji wa raia, baada ya akina mama waliokuwa wameshikiliwa na polisi kwa siku kadhaa kinyume cha sheria kulalamika kuwa wamedhalilishwa kijinsia wakiwa mahabusi, SAUTI KUBWA imeelezwa.

Miongoni mwa matukio ya jeshi hilo kunyanyasa akina mama hao ambao ni wanachama na viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ni kuwanyima dhamana, fursa ya kwenda kutibiwa na wengine kunyimwa haki yao kupata taulo za kike (pedi) ili kujihifadhi.

Polisi wa Tanzania wamekuwa wanashutumiwa kwa kukiuka sheria, kanuni na taratibu dhidi ya wananchi – kunyanyasa, kutesa na hata kuua watuhumiwa.

Mahabusu hao ambao walihifadhiwa katika vituo mbalimbali vya polisi Mkoa wa Dar es Salaam kwa zaidi ya siku nne, vile vile walikataliwa kuonana na ndugu zao waliofika vituoni hapo kuwadhamini au kuwaletea chakula.

Baadhi ya wenzao waliowapelekea chakula nao walikamatwa na kuwekwa mahabusi. Akina mama hao walikamatwa na polisi ktika eneo la mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam walipokuwa wameenda kufuatilia kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Ijumaa iliyopita.

Polisi walidai kuwa waliwakamatwa kwa tuhuma za “kufanya fujo na kukusanyika kwa lengo la kuleta taharuki.” Waliwanyimwa dhamana, ikiwa ni kinyume cha sheria za Tanzania ambazo zinaelekeza kwamba mtuhumiwa akikamatwa anatakiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24.

Jana Jumatatu Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) liliandika taarifa kwa umma ili kutaarifu kuwepo kwa ukiukwaji wa sheria kwa kuwazuia wanawake 18 waliokuwa wakishikiliwa na Polisi, ambao walinyimwa haki ya dhamana matibabu na haki ya faragha ya kupata pedi kwa wale waliokuwa katika siku zao.

Baada ya kelele kuwa nyingi, jana jioni mahabusu hao na wenzao kadhaa waliokuwa mahabusi kwa takribani wiki nzima walipewa dhamana na kutakiwa kuripoti katika Kituo Kikuu cha Polisi leo saa nne.

Wanawake waliokuwa wameshikiliwa ni pamoja na Kaimu Mwenyekiti Bawacha Sharifa Suleman, Katibu Mkuu Bawacha Catherine Ruge, Mratibu Mwenezi Bawacha Aisha Machano, na Mjumbe wa Baraza Kuu Bawacha Susan Kiwanga.

Wengine ni Margreth Mugyabuso, Mussa Ndile, Gerald Shoo,Ralma John, Neema Abdallah, Mussa Bwashari, Christian Paul, Rose Mtwange, Remina Peter, Sado Msomali, Joseph Mniko, Lazaro Sawe, Brayan Evarist, Omari Mkama na Digna Daudi.

Zaidi ya wanachama 40 wa Chadema wamekuwa mikononi mwa polisi katika vituo kadhaa jijini Dar es Salaam wakishikiliwa bila dhamana tangu wiki wiki iliyopita.

Taarifa ya jana iliyosainiwa na Naibu Katibu Mkuu Bawacha, Nuru Ndosi, ilieleza kuwa kuna shinikizo la kisiasa kwa kwa jeshi hilo “kuwashughulikia” wanawake wa Chadema ambao waliansamana kuwasilisha malalamiko ya kuminywa kwa demokrasia na ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye balozi kadhaa, ukiwamo Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.

Msemaji wa Polisi, David Misime, alipohojwa na SAUTI KUBWA kuhusu tuhuma hizi alikanusha na kueleza kwamba jeshi hilo limekuwa likifuata sheria na taratibu zote katika kutekeleza majukumu yake na haliwezi kunyanyasa wala kuonea mahabusu.

Alisema jeshi hilo limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha haki za mahabusu zinalindwa na kwamba kama wapo askari wanaokiuka sheria, huchukuliwa hatua mara moja.

“Hizi tuhuma nimezisikia, lakini hazina ukweli wowote, huenda wameamua tu kusema ili kuchafua sifa nzuri za jeshi letu, lakini hawawezi kunyanyaswa wala kunyimwa haki zao za msingi, endapo wako kwenye mikono yetu,” alisema Misime.

Wakili Jebra Kambole alisema tuhuma kwa Polisi zipo na zingine zimethibitishwa na mahakama, hivyo jeshi hilo haliwezi kukwepa malalamiko yanayoelekezwa kwao, hata kama viongozi wake watapinga ukweli huo.

Leo Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, anazungumza na vyombo vya habari kuhusu masuala kadhaa yanayolisibu taifa ikiwa ni pamoja na unyanyasaji uliovuka mipaka unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa malengo ya kisiasa kwa faida ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Like