Majaliwa ashutumiwa kwa kuwaiga Bashite, Musiba kutisha ndugu wa wakosoaji waishio ughaibuni

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, na Waziri wa Sheria na Katiba, Mwigulu Nchemba, wameingia katika kashfa mpya ya kutishia maisha ya baadhi ya Watanzania wanaohoji hali ya afya ya Rais John Magufuli.

Wakati, sku chache zilizopita, Nchemba alimuonya Tundu Lissu (ambaye alihoji alipo Rais Magufuli) akimkemea kwamba kusema sheria inaweza kuchukua mkondo dhidi yake kufuatia ujumbe aliouchapisha katika ukurasa wake wa Twitter, Majaliwa ametishia wanaharakati na wakosoaji, hasa walio nje ya Tanzania, akisema “ndugu zao wako hapa.”

Pamoja na kwamba Waziri Mkuu Majaliwa hakutaja majina ya Watanzania walioko nje ya nchi wanaohoji zaidi afya na alipo Rais Magufuli, alikuwa anawalenga Tundu LissuAnsbert NgurumoEvarist ChahaliMaria SarungiFatma KarumeMchungaji Godwin Chilewa na mwingine akitumia jina bandia la Kigogo2014.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Machi 6, 2021 Jumamosi usiku, Ngurumo ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuhoji juu ya hali ya Rais Magufuli akisema: “Yupo wapi Rais Magufuli? …Iwapo na Jumapili hii (kesho) hataonekana (hadharani) NI NEWS. Yupo wapi? Yukoje?”

Kesho yake Machi 7, 2021, Lissu akaandika kwa uwazi zaidi katika akaunti yake ya Twitter akihoji jambo lile lile; na ameendelea kuitaka serikali iseme aliko Magufuli, kabla na baada ya kauli ya vitisho ya Waziri Mkuu Majaliwa.

“Hiki ni kitisho, na hatukutarajia Majaliwa naye aanze kujiingiza kwenye ligi za kitoto za wapuuzi kina Bashite na Musiba. Na kusema watu wana ndugu zao hapa, maana yake anataka kuwafanya kitu gani? Sasa ajihadhari ndugu zao wasiumizwe. Majaliwa amekosea,” alisema mhadhiri mwandamizi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam ambaye hakutaka kutajwa jina.

Baadhi ya raia hawa wa Tanzania, wote wakiaminika kuwa nje ya Tanzania, tofauti na wenzao walioko nchini humo, wanahoji “kwa sauti,” – bila kificho, kupitia mitandao ya kijamii, wakitaka kujua alipo kiongozi huyo ambaye hajaonekana hadharani kwa siku 14 leo.

Wananchi wengi wanashangaa viongozi wa serikali kutisha watu wanaohoji alipo Rais Magufuli, badala ya kueleza alipo na kuwatoa wasiwasi wapigakura na walipakodi wa Tanzania.

Dk. Azavery Lwaitama anasema hakuna ubaya wowote kwa Watanzania na wengine wote kuhoji alipo kiongozi wao na kuwa siyo dhambi kutaka kujua hali ya afya ya mkuu wa nchi, kwani afya yake ni muhimu sana katika mustakabali wa taifa.

“Ikiwa kuhoji afya na alipo Rais Magufuli ni kosa na dhambi, basi kama nchi tumefika pabaya na kuna matatizo makubwa zaidi kuliko tunavyodhani,” alisema mhadhiri huo wa sayansi ya siasa.

Godlisten Malisa, mchambuzi wa masuala anuai wa Dar es Salaam, anaandika katika ukurasa wake wa Facebook – “hakuna kosa lolote kuuliza alipo baba, ni haki ya watoto kutambua alipo kiongozi wa familia.”

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu analeza kwamba ni haki kwa Watanzania na dunia kujia alipo Rais Magufuli na kwamba hakuna kosa lolote kutaka kujua afya yake.

Machi 12   – Ijumaa ya wiki hii inayomalizika leo, Waziri Mkuu Majaliwa akiwa ziarani Njombe aliwatisha wananchi wanaohiji alipo Rais Magufuli na kuwaita wazandiki, wenye husda na chuki dhidi ya Tanzania na kiongozi wao, Rais Magufuli.

Mtendaji mkuu huyo wa shughuli za serikali alisema watu wanaosambaza  taarifa hizo hawana mapenzi na nchi yao, huku akisisitiza kuwa rais hawezi kutoka iwapo hakuna shughuli ya msingi inayomfanya atoke wakati wasaidizi wake wapo.

“Ninasikitishwa na baadhi ya Watanzania ambao hawapendi maendeleo yetu maana kuna ambao wamejawa na chuki na husuda za kutaka kushuhudia Taifa hili linaporomoka kwa kuwa wao hawapo ndani wako nje ya nchi…

“Kuanzia juzi hadi leo asubuhi nimeona Watanzania wenzetu wenye husuda tena hawapo hapa nchini wapo huko nje  wanavishawishi vyombo vya kimataifa viseme Rais wa Tanzania anaumwa, amejifungia sisi tuliopo nchini tumekaa kimya na wanaona fahari kuisema vibaya nchi yao,” alisema Majaliwa.

Alibainisha kuwa wanaohoji alipo Rais Magufuli, pamoja na kuwa wapo nje ya nchi, lakini wana ndugu zao Tanzania; “lakini wengine tunawajua baba zao, mama zao, wadogo zao, wako hapa, lakini wao wanaona fahari kuisema nchi yao wakiwa huko, nataka niwaambie Watanzania mtulie.”

Kauli hii inahojiwa na wengi, kwamba kama anawajua ndugu wa hao Watanzania wanaohoji alipo kiongozi wao, anataka kuwafanya nini ndugu zao, kama siyo kuwatisha na kudhihirisha nia ovu ya “kuwasumbua” kwa kauli za kuhoji alipo Rais Magufuli?

Waziri Mkuu Majaliwa katika kuhitimisha karipio lake kwa wanaohoji alipo kiongozi wao, alisema “Rais anaendelea vizuri,” – kauli inayoelezwa na wachambuzi hao kuwa inathibitisha Rais Magufuli ni mgonjwa. Majaliwa hakueleza alipo.

Lissu kama ilivyo kwa Watanzania wengine, anaendelea kuhoji alipo Rais Magufuli  kupitia mitandao ya kijamii na kwa kuhojiwa na vyombo vya habari vya kimataifa vinavyoaminika, huku Maria Sarungi akiendeleza na kuambaza kishangilishi (hashtag) – #whereismagufuli? (#yukowapimagufuli?). Chahali yeye anaenda mbali zaidi akieleza Rais Magufuli kuwepo hospitali Dar e Salaam na kwaba hali yake ni tete- akiwa kitandani, hajitambui na kwamba anaumwa Corona.

Ngurumo amekuwa akiandika kuhoji alipo Rais Magufuli kupitia mtandao wa kijamii; Twitter, huku gazeti la mtandao la SAUTI KUBWA analoliongoza likiwa pekee – kwa Watanzania, linaloandika habari za uvumi wa ugonjwa na kuhoji alipo kiongozi huyo wa Tanzania.  

Vyombo vingi vya habari nje ya Tanzania na Afrika, kwa siku tatu sasa vimekuwa vikihoji alipo Rais Magufuli, huku viongozi wa serikali wakigoma kuzungumza ama kujib maswali wanayoulizwa kuhusu alipo na afya ya kingozi huyo.

“Kama vyombo vya Tanzania vinakuwa kimya, havitaki hata kuhoji alipo Rais Magufuli, basi vile vya nje, viachwe visaidie wananchi wengi kuhoji hadi hapo taarifa rasmi zitakapotolewa na wahusika ambao kukaa kwao kimya kunaongeza shauku ya kutaka kujua,” anaeleza Kingu Mathias, aliyejitambulisha kwa SAUTI KUBWA kuwa ni mwanafunzi wa chuo kikuu.

Hadi sasa vyombo vya habari vya Tanzania vimeshidwa hata kuandika habari za hisia, na kuacha uvumi wa hali a afya ya rais wan chi yao kuhojiwa na magazeti na televisheni vya nje. Vyombo hivyo vya Tanzaia, vimeandika tu kali ya Majaliwa kwamba Rais Magufuli ni “mzima wa afya” na kuonya wanaohoji alipo.

Rais Magufuli hajaonekana hadharani kwa wiki mbili sasa, mara ya mwisho ilikuwa Machi 11.

Hotuba ya waziri mkuu hii hapa

Like
1