Papa Francis ateua mrithi wa Pengo. Ni Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi

Pope Francis addresses faithfuls in St Peters square at the Vatican during his weekly general audience on June 20, 2018. (Photo by VINCENZO PINTO / AFP) (Photo credit should read VINCENZO PINTO/AFP/Getty Images)

BABA Mtakatifu Francis amemteua Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza Yuda Thaddeus Ruwaichi kuwa mrithi mtarajiwa wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ambalo limekuwa linaongozwa na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo. Kwa uteuzi huu, Askofu Mkuu Ruwaichi anakuwa Askofu Mkuu Mwandamizi Mwenye Haki ya Kurithi Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Padri Richard A. Mjigwa wa Vatican News  ameandika katika mtandao wa Vatican, na Padri Raymond Saba, Katibu Mkuu wa Baraza la Maskofu Tanzania (TEC) ametoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu uteuzi huo.

Kwa uteuzi huu maana yake ni kwamba mchakato wa kustaafu kwa  Kardinali Pengo umekamilika, hasa kutokana na matakwa ya kisheria kuhusu umri, na kwa sababu ya afya yake kutetereka.

Habari za uhakika ambazo SAUTI KUBWA limepata kutoka ndani ya Kanisa Katoliki ni kwamba Kardinali Pengo atastaafu rasmi mwakani (2019) atakapotimiza umri wa miaka 75.

Huyu wa Mwanza anahamia hapa ili kusubiri kuchukua jimbo,” chanzo hicho kimeeleza SAUTI KUBWA.

Kabla ya kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Pengo naye aliteuliwa kuwa askofu Mkuu Mwandamizi Mwenye Haki ya Kurithi tarehe 22 Januari 1990. Aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam tarehe 22 Julai 1992 baada ya kustaafu kwa Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa.

Kabla ya uteuzi huu, Askofu Mkuu Ruwaichi alikuwa ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza tangu tarehe 10 Novemba 2010.  Kwa uteuzi huu wa leo, Askofu Mkuu Ruwaichi amepitia katika mikono ya wateuzi watatu – Papa Yohanne Paulo II, Papa Benedicto XVI, na Papa Francis.

Askofu Mkuu Ruwaichi alizaliwa tarehe 30 Januari 1954, Mulo, Kilema, Jimbo Katoliki la Moshi. Alipadirishwa  tarehe 25 Novemba 1981, akapewa daraja la uaskofu tarehe 9 Februari 1999, kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Mbulu, na akawekewa wakfu tarehe 16 Mei 1999.

Tarehe 15 Januari 2005, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma na kusimikwa rasmi tarehe 19 Februari 2005. Tarehe 10 Novemba 2010, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteua kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Mwanza, akasimikwa rasmi tarehe 9 Januari 2011.

Polycarp Mdemu, mmoja wa vijana wa kikatoliki wanaozifahamu vizuri wa sheria za kanisa, anafafanua  kilichotokea ili kujibu hoja zilizoibuliwa katika mijadala mbalimbali, kutokana na watu wengi kutojua suala hili. Mdemu anatoa tafsiri ya askofu mkuu mwandamizi au kwa maneno mengine “askofu mrith,i” kwa Kiingereza “COADJUTOR ARCHBISHOP.”
Huyu ni Askofu aliyeteuliwa kurithi madaraka kamili ya kuongoza na kusimamia jimbo kuu endapo Askofu aliyepo madarakani ataacha kusimamia jimbo hilo kufuatia sababu yoyote ile (ugonjwa, kujiuzulu, kustaafu au kufariki).
Askofu Mku Mwandamizi huteuliwa na Papa kama wanavyoteuliwa Maaskofu wengine. Na anatarajiwa kumsaidia Askofu wa jimbo katika shughuli za usimamizi wa jimbo kulingana na mwongozo wa Kanisa Katoliki chini ya usimamizi wa Askofu mkuu aliyepo madarakani.
Kipindi hiki Askofu Mkuu Mwandamizi anakuwa hana madaraka kamili ya kuongoza au kusimamia jimbo ila humsaidia Askofu aliyepo madarakani. Hata hivyo mara nyingi Askofu aliyepo madarakani lazima amsikilize mwandamizi wake, kwa kuwa ndiye atakayepaswa kuendesha jimbo baadaye. Askofu mwandamizi anapewa na Papa mamlaka ya pekee, hasa kutokana na hali ya Askofu wa jimbo au ya jimbo lenyewe (hasa kama Askofu Mkuu ni mgonjwa au jimbo linahitaji uangalizi zaidi).
Upande wa sakramenti askofu Mwandamizi ni Askofu kamili kama walivyo Maaskofu wengine na huweza kutoa sakramenti zote zikiwa ni pamoja na daraja takatifu ila atahitaji ruhusa ya Askofu wa jimbo ili kufanya hivyo.
Kwahiyo Askofu Mkuu Mwandamizi Ruwaichi atamsaidia Askofu Pengo, mpaka pale Kadinali Pengo atakapopumzika (either kwa ugonjwa, kujiuzulu, kustaafu au kifo), ndipo Askofu Ruwaichi atachukua mamlaka kamili ya urithi wa jimbo na kusimikwa rasmi kuwa Askofu Mkuu.
Kuna watu wanahoji kama Askofu Mkuu Ruwaichi anaenda kumsaidia Askofu Pengo, mbona jimbo kuu Dar es Salaam linayo Askofu Msaidizi ambaye ni Baba Askofu Eusebius Nzigilwa? Jibu ni kwamba Baba Askofu Nzigilwa yeye ni Askofu Msaidizi (Auxiliary Bishop), lakini Baba Askofu Ruwaichi yeye ni Askofu Mkuu Mwandamizi (Coadjutor Archbishop). Wote wawili wanamsaidia Askofu Pengo lakini mwenye haki ya kurithi nafasi ya Pengo ni Askofu Ruwaichi (CUM JURE SUCCESIONIS).
Ikitokea Pengo amepumzika utumishi muda wowote kuanzia sasa (either kwa ugonjwa, kujiuzulu kustaafu au kifo), Askofu Ruwaichi atarithi nafasi hiyo, wala haitakuwa na haja ya kutangazwa tena ila atasimikwa tu. Na Askofu Nzigilwa ataendelea kuwa Askofu Msaidizi kwa Ruwaichi, kama alivyokuwa Askofu Msaidizi kwa Pengo (unless otherwise kama Papa atamuondoa Dar kumpeleka jimbo jingine).
Marekebisho ya sheria za kanisa (Cannon Laws) ya mwaka 1983 ndiyo yaliyoruhusu Askofu Mkuu Mwandamizi kupata haki ya moja kwa moja ya kurithi jimbo pale ambapo Askofu aliyepo madarakani atapumzika (kwa ugonjwa, kujiuzulu, kustaafu, au kifo).
Kabla ya marekebisho hayo Askofu Mwandamizi na Askofu Msaidizi yeyote kati yao alikuwa anaweza kurithi nafasi ya Askofu mkuu. Yani kama sio marekebisho ya Cannon Law ya mwaka 1983, kati ya Askofu Mkuu Mwandamizi Ruwaichi au Askofu Msaidizi Nzigilwa mmoja wao angeweza kurithi nafasi ya Pengo.
Kwa mfano mwaka 1965 Baba Mtakatifu Paul VII alimteua Askofu John Maguire kuwa Askofu Mkuu Mwandamizi (Coadjutor Archbishop) wa Jimbo kuu katoliki la New York. Wengi walitarajia kuwa Askofu Maguire angerithi nafasi ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa jimbo hilo Kadinali Francis Joseph Spellman. Lakini ajabu ni kwamba baada ya Spellman kufariki, Baba Mtakatifu Paul VII alimteua aliyekuwa Askofu Msaidizi (Auxiliary Bishop) wa jimbo la New York Baba Askofu Terence Cooke kuwa Askofu Mkuu wa jimbo hilo.
Lakini baada ya marekebisho hayo ya mwaka 1983 hasa katika kifungu “CUM JURE SUCCESIONIS” kwa kiingereza “WITH THE RIGHT OF SUCCESSION” kwa kiswahili kisicho rasmi “MWENYE HAKI YA KURITHI” Sheria za kanisa kwa sasa zinampa Askofu Mkuu Mwanadamizi haki ya urithi ya moja kwa moja, na sio Askofu msaidizi.
Kwahiyo muda wowote kuanzia sasa Askofu Mkuu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akipumzika (kwa ugonjwa, kujiuzulu, kustaafu au kifo) basi Askofu Mkuu Mwandamizi Yuda Thadei Ruwaichi anarithi moja kwa moja nafasi yake na kusimikwa rasmi. Hii ni pamoja na nafasi ya kuteuliwa kuwa kardinali (Soma sheria za kanisa CANON LAW, kuanzia CAN. 403 hadi CAN. 410).
Ni vizuri waandishi wanapoandika watafute taarifa kwa usahihi, badala ya kuandika mambo wasioyajua wakaishia kupotosha. Baba Mtakatifu Augustino aliwahi kusema “Roma locuta; causa finita est” yani Roma ikishaamua, mjadala umefungwa. Na tuufunge sasa mjadala huu wa Askofu Mkuu Mwandamizi Ruwaichi, na tumtakie heri katika majukumu yake mapya.

 

Like
6

Leave a Comment

Your email address will not be published.