Magufuli amteua Utoh na kuibua mzozo wa kikatiba

RAIS John Magufuli amemteua Ludovick Utoh kuwa mwenyekiti wa taasisi ya uhamasishaji uwazi na uwajibikaji katika raslimali za madini, mafuta, na gesi asilia.

Utoh ni mstaafu ambaye alikuwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG). Kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano, mtu ambaye amewahi kuwa CAG hawezi kuteuliwa kushika wadhifa wowote katika serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Ibara ya 144 (6) ya katiba inasema: “Mtu ambaye ni mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu au aliyepata kuwa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu hawezi kuteuliwa kushika au kushikilia madaraka ya kazi nyingine yoyote katka utumishi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano.”  Ibara ya 144 (7) inasema: “Masharti ya ibara hii hayatatumika kwa mtu yeyote aliyeteuliwa kuwa kaimu mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu.

Wakili Albert Msando, ambaye alihamia katika CCM hivi karibuni akitokea ACT-Wazalendo, ametetea uteuzi huo akinukuu sheria inayompa rais mamlaka hayo. Anasema:

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, Ibara ya 144(6) inakataza mtu yeyote aliyewahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu kuteuliwa kushika madaraka kwenye utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

“Ndugu Ludovik Utouh amewahi kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu. Hivyo ni kwa sababu hiyo baadhi ya watu ambao siku zote wamekaa ‘standby’ kukejeli, kucheka, kukosoa na kumzodoa Rais, Dkt John Pombe Magufuli wamekurupuka na kudai amekiuka Katiba.

“Kwa mujibu wa Sheria inayounda Kamati hiyo na Sheria ya Utumishi wa Umma Mh. Rais hajakiuka Katiba kwa kumteua Ndugu Ludovik Utouh kuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

“Ukisoma Sheria ya iliyoanzisha Kamati ya Uhamasishaji Uwajibikaji na Uwazi Katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia ya mwaka 2015, kifungu cha 4, inaunda Kamati hiyo ambayo kama chombo huru. Na kifungu cha 5 kinataja wajumbe wake ambao ni, Mwenyekiti anayeteuliwa na Mh. Rais na wajumbe wengine wasiozidi 15.

“Kifungu cha 6 cha Sheria hiyo kinaunda Kamati ya Uteuzi (Nomination Committee) ambayo kazi yake ni pamoja na kupendekeza majina matatu kwa Waziri ambayo atayapeleka kwa Rais kwa ajili ya uteuzi wa Mwenyekiti wa Kamati.

“Kifungu cha 13 cha Sheria kinaunda Sekretarieti ya Kamati na kutamka wazi kwamba watumishi (Staffs) wake ndio watakuwa watumishi wa umma (public servants). Ingekuwa ni lengo la watunga sheria basi ingetamkwa wazi kwamba wajumbe hao wa Kamati wakiteuliwa wanakuwa watumishi wa Serikali (kama kwa nafasi zao sio watumishi tayari).

“Kifungu cha 3(a)(ii) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, 2002 kinatafsiri, kwa ufupi, kuhusu ‘utumishi wa umma’ na kueleza kwamba mtumishi wa umma ni mtu yeyote anayetoa huduma kwenye utumishi wa umma ISIPOKUWA mtu ambaye ameteuliwa kama mjumbe kwenye Kamati iliyoundwa na Sheria.

“Kwa tafsiri hiyo Ndugu Ludovik Utouh sio mtumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania au Mtumishi wa umma kwa uteuzi wake. Uteuzi wake haujakiuka Katiba hivyo Rais hakuna alipokosea kwa kumteua.”

Hata hivyo, wachambuzi wanahoji: “kipi kikubwa kati ya sheria na katiba?” Swali ambalo Msando hakujibu ni je, kama Utoh si mtumishi wa serikali ameteuliwa awe mtumishi wa nani? Na kama si mtumishi wa serikali kwanini ateuliwe na rais?

Japhet Matarra, a naye kitambulisho kama mhandisi, anasema:

Tumehoji uteuzi kwa sababu haujafuata katiba ya Jamhuri ya Muungano… Maana katiba ndio sheria mama, lazima tujue inasemaje. Hakuna sheria yoyote au kanuni yoyote inayoruhusiwa kupingana na katiba.”

Kwa mujibu wa Matarra, tafasiri ya neno kiongozi wa umma unapatikana katika kifungu cha 4 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.

“Mtumishi au kiongozi wa umma inajumuisha watu hawa wafuatao:

“Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Spika na Naibu Spika, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Waziri, Naibu Waziri na Mkuu wa Mkoa.

Wamo pia mwanasheria mkuu, jaji na hakimu, mbunge, balozi mwakilishi wa Tanzania nchi za nje, katibu mkuu kiongozi, katibu mkuu, naibu katibu mkuu, katibu tawala wa mkoa na mkuu wa wilaya, mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, katibu wa bunge, mkuu wa jeshi la ulinzi, inspekta jenerali wa polisi na kamanda wa polisi wa mkoa, mkuu wa jeshi la kujenga
taifa.

Wamo pia kamishna mkuu wa magereza, mkurugenzi mkuu wa usalama wa taifa; mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa, meya, mwenyekiti, diwani au mtendaji mkuu wa serikali ya mtaa; gavana, naibu gavana, mwenyekiti au mkurugenzi wendeshaji, meneja mkuu au mkurugenzi kuu wa shirika ambalo serikali ina maslahi makubwa.

” Inajumuisha pia, *mwenyekiti na wajumbe wa tume zote walioteuliwa kwa misingi ya kudumu, viongozi wanaosimamia Idara za serikali,
Makamishna wa kodi katika mamlaka ya mapato Tanzania, makamishna na wakurugenzi wa wizara za Serikali.

“Halikadhalika, bila kuwasahau na wale viongozi wa umma ambao Mhe. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete aliwaongeza katika orodha ya viongozi wa umma alipokuwa madarakani mnamo mwaka 2013.

SAUTI KUBWA linaambatanisha ibara hiyo ya katiba hapa chini:

Like
2

Leave a Comment

Your email address will not be published.