Mwigulu Nchemba, mchumi mpotoshaji, afungwe breki

Tunahitaji akiba ya fedha za kigeni pale BoT ili kuendelea kudumisha ukwasi ikiwa itatokea mdororo wowote wa kiuchumi. Hizi siyo fedha za kujenga madarasa kama ambavyo Mwigulu analieleza bunge na wabunge wa CCM wanashangilia meno nje.

January 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alisema Tanzania ina jumla ya akiba ya fedha za kigeni $6.253 (TZS 14 trilioni). February 2023 tunaelezwa kiasi hicho kimebaki $3.5 bilioni. Kiasi hicho kimekwenda wapi? Mwigulu anasema wametumia kujenga madarasa.

Kinachoshangaza ni utetezi wa waziri wa fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba. Anasema akiba ya fedha za kigeni imepungua kwa sababu fedha zinetumika kujenga madarasa na kuagiza vifaa vya kimkakati. Imenishtua zaidi kwamba huyu ni daktari wa uchumi.

Hoja iliyopo mezani ni kwamba akiba ta fedha za kigeni imeporomoka kutoka $6.253 bilioni hadi $3.5 bilioni ndani ya miezi 12 tu. Hili ni poromoko la $2.8 bilioni. Waziri amekiri, na Utetezi wake ni kwamba fedha hizi zimetumika kujenga vyumba vya madarasa.

Kuporomoka kwa akiba ya fedha za kigeni, nchi itashindwa kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi, itashindwa kulipa madeni na mikopo, kulipa (obligations) za kimataifa. Kukosekana kwa akiba ya fedha za kigeni maana yake ni kukwama kwa biashara, uzalishaji na uchumi.

Wakati akiba ya fedha za kigeni ikiwa $6.253 bilioni January 2022 kiasi hicho cha akiba kilikuwa kinatosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa kipindi cha miezi saba. Hii $3.5 bilioni inatosha kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi mingapi?

Akiba ya fedha za kigeni ni kiasi cha jumla cha fedha za kigeni kinachoingia ndani ya nchi kupitia njia mbalimbali. Kwa ujumla akiba ya fedha za kigeni ndiyo huitwa (foreign exchange reserve account) iliyopo benki kuu ya Tanzania (BoT).

Mapato ya serikali yatokanayo na kodi (mapato, majengo, miamala) na mapato yasiyo na kodi (faida za makampuni ya serikali, faida katika hisa za migodi, misaada na mikopo yanaingia katika akaunti maalum ya hazina ya serikali (exchequer account) inayosimamiwa na wizara ya fedha

Hazina ndiyo wenye Jukumu la kugawanya fedha hizo (disbursement) kwenda katika matumizi kulingana na bajeti ya serikali inavyoelekeza. Wizara ya fedha ina Jukumu la usimamizi wa sera za kibajeti (fiscal policy) ambayo ni usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali.

Akiba ya fedha za kigeni siyo fedha iliyopo hazina. Akiba hiyo ipo katika akaunti maalum (foreign exchange reserve account) chini ya Benki kuu ya Tanzania (BoT). Akiba ya fedha za kigeni inatumika katika mahitaji ya nchi kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi. Siyo ujenzi wa madarasa.

Akiba ya fedha za kigeni ni nyenzo katika kutekeleza sera ya udhibiti wa thamani ya fedha (currency/exchange rate policy). Ikiwa akiba ya fedha za kigeni ni kubwa uwezo wa nchi kusimamia udhibiti wa thamani wa fedha ya nchi dhidi ya nyingine unakuwa mkubwa.

Inapotokea pressure ya kupungua thamani ya fedha ya nchi katika masoko ya fedha kimataifa (currency depreciation) benki kuu inatumia akiba ya fedha za kigeni kununua fedha yake kwa wingi sokoni ili ipandishe au ipunguze bei ya sarafu yake. HUNA, utanunua na nini tai yenye bendera ya Taifa?

Mwigulu, ningependa kusikia kutoka kwako kwamba, ili kuondokana na (dependence/non diversified) nchi yetu imetengeneza muundo wa uzalishaji wa vyanzo (diversified export structure) ili kuwa na ongezeko la hifadhi ya fedha za kigeni imara (resilient against shock).

Hoja ya uwiano wa biashara (imports & exports) akiba ya fedha za kigeni itaongezeka ikiwa nchi inauza zaidi kwenda nje ya nchi (exports) hivyo kiasi cha malipo ya fedha za kigeni kitaongezeka na takwimu zitaongezeka.

Uuzaji wa huduma nje ya nchi mfano shughuli za Utalii, kwa kiasi kikubwa zinategemea wageni kutoka nje ya nchi. Maana yake, watalii wengi, wanakuja na fedha za kigeni nyingi, wapo wanaobeba ‘cash’ au kuhamisha fedha hizi kwa njia za kibenki.

(capital flows) inapoongezeka, fedha za kigeni zinaongezeka, kutokana na kuingia kwa mitaji ambayo ipo katika fedha za kigeni. Katika nchi za Afrika ya Mashariki KIPIMO cha miezi 4 hadi 6 kinatumika kuonyesha kama akiba ya fedha za kigeni inamudu mahitaji ya nchi.

Mwongozo wa utekelezaji sera za fedha (Monetary Policy Statement) taarifa iliyochapishwa na (BoT) June 2021/2022 uk. 5, malengo ya sera ya fedha, lazima iwepo akiba ya fedha za kigeni itakayotosha kuhudumia uagizaji wa bidhaa kwa kipindi cha miezi 4

Nchi kuwa na hifadhi kubwa ya fedha za kigeni inategemea na ukubwa wa uchumi na uzalishaji kwenda nje ya nchi (productive capacity and diversified export structure). Nchi inayozalisha na kuuza inakuwa na vyanzo vingi vya uingiaji wa fedha za kigeni hivyo akiba inakuwa kubwa.

Nchi yenye uchumi mdogo wa uzalishaji uingiaji wa fedha za kigeni unakuwa mdogo. Mwenendo wa akiba ya fedha za kigeni inategemea na mwenendo wa biashara ya kimataifa wa nchi. Utaeleweka kupitia takwimu za biashara ya kimataifa (balance of payment statistics) ambazo huchapishwa na (BoT)

Mwigulu anasema pesa za IMF waliziingiza kwenye akiba ya fedha za kigeni na baadae wakatoa Sh. 1 trilioni na wakapeleka kwenye ujenzi wa vyumba vya madarasa. Mwigulu huyu ni mchumi kweli? Anajua anachokiongea? Anapotosha wabunge wenzake.

Tunahitaji akiba ya fedha za kigeni pale BoT ili kuendelea kudumisha ukwasi ikiwa itatokea mdororo wowote wa kiuchumi. Hizi siyo fedha za kujenga madarasa kama ambavyo Mwigulu analieleza bunge na wabunge wa CCM wanashangilia meno nje.

Mdororo wa kiuchumi ukitokea, Benki Kuu inaweza kuingilia kati na kubadilisha fedha zake za kigeni kwa fedha ya ndani (shilingi ya Tanzania) ili kuhakikisha makampuni au biashara zinaweza kuendelea kuagiza na kuuza nje kwa ushindani.

Mali ya akiba ya fedha za kigeni mbali ya noti, amana za kibenki, dhamana za serikali (bondi na bili za hazina), pia baadhi ya nchi huwa zinashikilia sehemu ya akiba zake kwa njia ya dhahabu na special drawing rights (SDR za IMF).

Lakini hizi SDRs (special drawing rights) ni akiba ya mali ya kimataifa (international reserve assets) iliyoundwa na IMF (International Monetary Fund) ili kuongeza akiba rasmi (supplement the official reserves) za nchi wanachama wake.

SDR za IMF siyo sarafu, bali madai maalum kwa sarafu zinazoweza kutumika kwa ajili ya wanachama wa IMF zinazoweza kutumika kuongeza ukwasi wa nchi. Matumizi yake yanachunguzwa na lazima iwe ni mgogoro mkubwa wa kiuchumi kama COVID-19.

Kapu la sarafu (basket of currencies) linalofafanua SDRs linajumuisha USD, EURO, YUAN ya CHINA, YEN JAPAN na PAUNI Uingereza. Kwa kuwa DOLA ya Marekani inatawala uchumi na biashara kimataifa (World Reserve Currency) akiba ya fedha za kigeni inawekwa katika DOLA

Viashiria vingine vya kiuchumi ambavyo vinawezwa kuelezwa katika DOLA ni pamoja na Deni la Taifa, Pato la Taifa (GDP), bajeti kuu ya serikali n.k. Hii ndiyo ukuu wa dola (US dollar supremacy). Rejea Bretton Woods Agreements, mkataba ambao ndiyo uliyounda IMF.

Hizi fedha za IMF siyo fedha kwa ajili ya kupambana na misukosuko ya ujenzi wa madarasa na madawati kama anavyotueleza Mwigulu Nchemba. Ni SDRs ambazo IMF wanatupa kwa ajili ya nchi yetu kwa ajili ya kurekebisha ukwasi endapo kuna mdororo wa kiuchumi.

Mwigulu, unakwenda bungeni kuwachamba wabunge wanaohoji masuala ya msingi kama hivi kwamba wakahoji masuala ya waganga wa kienyeji. Basi na sisi tunaomba ‘peer reviewed publications’ zako hapa za uchumi – ili tuamini zaidi kuwa: “this is my profession.”

Like