Nani atavunja benki ipi soka la Ulaya msimu ujao?

MSIMU wa timu kubwa za soka duniani “kuvunja benki” ili kununua au  kuuza wachezaji wao nyota, sasa umefika.

Ni muda ambao mameneja na familia za wacheza soka husubiri kwa hamu na gamu ili kufaidi matunda ya ufundi wa ‘vijana’ wao uwanjani.

SAUTI KUBWA imefuatilia uuzaji, kubadilishana au hata uhamisho wa wachezaji nyota wa soka barani Ulaya katika msimu wa sasa unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kunasa saini za wachezaji hao.

Mchezaji Arkadiusz Milik (27), imebainika kuwa anawaniwa na timu mbili kubwa ambazo ni Juventus na AS Roma kutoka Italia, ambazo zinapambana kuhakikisha kijana huyo anacheza moja ya timu hizo.

Klabu ya Real Madrid ya Hispania inahusishwa na mshambuliaji wa Bayern Munich – ya Uingereza, Robert Lewandowski (32), hiyo imetokana na wakala wa mchezaji huyo kuweka wazi kwamba atasikiliza ofa kwenye dirisha la usajili mwisho wa msimu huu.

Klabu ya Inter Milan ya Italia imejiunga katika mbio za kuinasa saini ya mchezaji wa Chelsea – ya Uingereza, Tammy Abraham (23). Tayari Chelsea imeonyesha nia ya kupokea pauni milioni 40, sawa na Sh.  bilioni 120.

Totenham Hotspur ya Uingereza, imepania kumsajili mshambuliaji wa Brentford, Ivan Toney (25), ambaye anavivutia vilabu kadhaa nchini Uingereza baada ya kupachika mabao 29 kwenye michezo 43.

Leicester City ya Uingereza imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kumsajili Boubacary Soumare  anayekipiga kwenye klabu ya Lille ya nchini Ufaransa na mazungumzo yanaendelea.

Wakala ‘mtata’ Mino Raiola amekiri kuwa Klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani inaweza kushawishika kumuuza mshambuliaji wake machachali Erling Haaland. Imeripotiwa kwamba kinda huyo ana kipengele kwenye kandarasi yake kinachomruhusu kuondoka kwenye klabu hiyo kama dau la Uuro milioni 75, kipengele hicho kitaanza kutumika mwaka 2022.

Mshambuliaji wa klabu ya Juventus na timu ya Taifa ya Argentina, Paulo Dybala hana nia ya kuondoka katika klabu yake hiyo ya Jijini Turin. Amefikia maamuzi hayo baada ya kuhusishwa kwa vilabu kadhaa Barani Ulaya.

Klabu ya Arsenal ya Uingereza imejipanga kumshinda mpinzani wake Totenham kwa kupata saini ya kiungo wa Brighton, Yves Bissoum kwa ofa ya pauni milini 30. Vilabu kadhaa kutoka nchini Uingereza vinamnyemelea kiungo huyo.

Beki ‘kisiki’ wa klabu ya Real Madrid Sergio Ramos hajakata tamaa kwenye jitihada zake za kusaini kandarasi mpya ya miaka miwili na miamba hao wa Hispania licha ya klabu hiyo kutaka kandarasi ya miezi kumi na mbili tu.

Kocha wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Ubelgiji, Roberto Martinez, amekiri kuwa tayari kuinoa klabu ya Totenham Hotspur ya nchini Uingereza. Hiyo imekuja baada ya klabu hiyo ya Jiji la London kumfungia virago aliyekuwa kocha wake mkuu, Jose Mourinho mwezi Aprili 2021.

Klabu ya Manchester United itakuwa tayari kumuuza kiungo wake Paul Pogba kama akikataa kusaini kandarasi mpya. Uamuzi huo umekuja kutokana na kandarasi ya kiungo huyo kufikia mwisho msimu ujao.

Like
3