Tanzania sasa imefunguka – Samia

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali yake iko tayari kubadili vifungu vya sheria ambavyo vinakwanza ustawi na maendeleo ya Tanzania.

Mbali na kauli hiyo, Rais Samia pia amesema: “Tanzania sasa imefunguka.”

“Kama kuna sheria hazitoi fursa, mseme, hatuwezi kuwa watumwa wa sheria tulizotunga wenyewe,” alisema Rais Samia jana jijini Nairobi, Kenya wakati akizungumza na Watanzania waliowekeza Kenya pamoja na kundi la wafanyabiashara aliombatana nao kutoka Tanzania.

Rais Samia alikuwa na ziara rasmi ya siku mbili nchini humo alikoalikwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Nilikuwa naongea na Rais Kenyatta, akaniambia kwamba kuna Watanzania wametoroka huko kwetu, lakini nikiwa hapa baadhi sasa wameninong’oneza wanataka kurudi nyumbani, kama mpo hapa, rudini nyumbani, rudini tu nyumbani, mtakuja kufanya biashara na mengine ambayo mtapenda,” alishauri Raus Samia.

Katika ziara hiyo, Rais Samia alipewa heshima ya kupigiwa  mizinga na fursa ya kukagua gwaride ikiwa ni ishara ya mwaliko rasmi kwa kiongozi wa nchi.

Akihutubia bunge la pamoja la Kenya; Bunge la Taifa na Seneti, Rais Samia alieleza wajumbe na umma kwamba “ugomvi” uliokuwapo baina ya mataifa hayo mawili, hakuwa mkubwa, bali ulichochewa na kutofatiana kwa kauli kwa baadhi ya viongozi na kwamba sasa Kenya na Tanzania zitaimarisha zaidi uhusiano wao kwa manufaa ya watu wa mataifa hayo ya Afrika Mashariki.

Wakati wa uongozi wa Rais John Magufuli, uhusiano wa kihisoria kati ya Kenya na Tanzania ulionekana kutetereka kutokana na kutofautiana kwa misimamo, hasa kuhusu namna ya kufanya biashara baina ya nchi hizo. Rais Magufuli alifariki Marchi 17, mwaka huu na nafasi yake kuchukuliwa na Rais Samia.

Kufuatia kauli na msimamo wa Rais Samia, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Mandeeo (Chadema), Freeman Mbowe ameguswa na kiongozi huyo na kueleza kwamba “akiendelea hivyo, basi Tanzania tunaweza kufika kwenye “usawa na demokrasia iliyoiva.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Mbowe pia ameandika; “kauli patanishi na unganishi za Rais Samia nchini Kenya zinaleta tabasamu pande zote mbili. Dunia imeona, inasikia na sasa inasubiri vitedo, Tanzania kulikuwa na uharibfu mkubwa zaidi, rejesha tabasamu la haki, uhuru na demokrasia.”

Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, katika ukurasa wake wa Twitter, alionekana kuguswa na kauli za Rais Samia ameandika; “naona watu walikokuwa wanavumilia kuwa Watanzania, sasa wameanza kujivunia kuwa Watanzania. Inatia moyo sana.”

Dk. Azaveli Laitama ameiambia SAUTI KUBWA kwamba endapo Rais Samia ataendelea na kasi aliyonayo ya kukataa uonevu na kupenda kuona haki ikitamalaki, Watanzania watarajie haki, neema na heri, tunu za ubinadamu ambazo walizokosa kwa miaka mitano.

“Miaka mitano iliyopita, kila mtu alikuwa na hofu kutokana na aina ya uongozi wa kuonea, kutisha na kukejeli tuliokuwa nao, sasa mamb haya yanaonekana kuondoka na neema inaonekana kila mahali hata kwa wale waliokuwa wakiushabikia kwa nguvu zote,” aliongeza Dk. Lwaitama, mhadhiri wa vyuo vikuu.

·        Katika hatua nyingine, Rais Samia Suluhu Hassan, kesho jijini Dar es Salaam, atakuwa na mkutano na wazee. Mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Mlimani City.

Like