Mwekezaji wa gesi Msumbiji kuhamishia mradi Tanzania

MRADI mkubwa wa gesi asilia ulioanza kutekelezwa nchini Msumbiji sasa utahamia Tanzania baada ya wawekezaji – TOTAL – kuuondoa nchini humo kwa sababu ya machafuko yanayohusisha kundi la waasi linalosaidiwa na Dola la Kiislam la IS, SAUTI KUBWA imeelezwa.

Mradi mkubwa huo uliomo katika Mkoa wa Cabo Delgado umekumbwa na kadhia ya mapigano baina ya serikali ya Msumbiji na waasi hao na kwamba idadi kubwa ya wananchi wa nchi hiyo wanaendelea kupoteza maisha kila siku.

Cabo Delgado uko zaidi ya kilomita 1,600 kutoka Mji Mkuu wa Msumbiji, Maputo.

Mradi huo wa gesi asilia unaotekelezwa na kampuni ya Ufaransa ya Total, ukiwa na thamani ya dola bilioni 60 za Marekani, sasa hauwezi kuendelea huko na sehemu pekee ambayo iko salama ni Tanzania.

Tayari hatua za awali za kuanza kwa mazungumzo kati ya Tanzania na Total zimeanza kuchukuliwa kutoka pande mbili kuhusu mradi huo unaoelezwa kuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James Mataragio ameeleza kwamba mazungumzo na wawekezaji; Total, yataanza mara moja.

Nchini Msumbiji, Total ilisema wiki iliyopita kwamba ilianza kuondoa wafanyakazi wake nchini humo kutokana na “mabadiliko ya hali ya usalama”, baada ya kusimamisha shughuli huko Cabo Delgado kufuatia shambulio la Machi 24, mwaka huu ambalo lilisababisha makumi ya watu kuuawa na wengine wengi wakikimbia katika mji wa Palma.

Shambulio hilo lilikuwa mojawapo ya mengi yaliyotokea katika mkoa huo katika miaka mitatu iliyopita, wakati wa mivutano na machafuko yaliyohusishwa na Dola la Kiisilamu.

Ofisa Mkuu wa Fedha wa Total, Jean-Pierre Sbraire, amenukuriwa na SAUTI KUBWA akieleza kwamba kampuni yake imelazimika kuchukua uamuzi wa kuhamishia shughuli za mradi huo wa gesi nchini Tanzania baada ya kutokea kwa machafuko – na yanaoendelea Msumbiji.

Like