Samia naye adai hatabagua watu kiitikadi

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema anajiandaa kufanya mabadiliko makubwa ya kisera, kisheria, kitaasisi na kiuongozi katika safu ya watendaji wake, na kwamba katika kutekeleza majukumu hatabagua watu bali atazingatia weledi wao.

Hata hivyo, kauli yake hii haitofautiani na ya mtangulizi wake – John Magufuli – ambaye, ingawa alisema mara kadhaa kuwa maendeleo hayana chama, aliongoza nchi kwa ubaguzi na chuki dhidi ya waliompinga. Magufuli alifikia hatua ya kubagua baadhi ya makabila hasa kutoka Kaskazini ya nchi.

Magufuli alitumia kauli hiyo kuwapa madaraka baadhi ya wanasiasa wa upinzani ambao baadaye aliwalazimisha kuhamia CCM. Wengine aliwahamisha kwa ahadi ya kuwapa vyeo na fursa nyingine. Wapo waliovipata, na baadhi ya waliovikosa waliishia kunung’unika chini chini.

Hata hivyo, Samia amesisitiza: “Mtu yeyote nitakayeona ana uwezo wa kusaidia taifa letu na kuleta tija katika eneo fulani, nitamteua afanye kazi bila kujali anatoka chama gani, ilimradi tu awe hana kasoro ya kiusalama wala dosari ya kimaadili.”

Samia amesema mabadiliko anayotaka kufanya yatajumuisha watu wenye uwezo bila kujali tofauti katika itikadi za kisiasa, kidini, kijinsia, au kikabila.

“Serikali itafanya mabadiliko makubwa kwa watendaji ili kuhakikisha maendeleo makubwa yanapatikana na kufaidisha umma wa Watanzania,” amesema Rais Samia.

Ameyasema hayo leo alipozungumza na umma wa Watanzania kupitia mkutano na wazee wa Dar es Salaam katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar esa Salaam.  

Rais Samia amesema kwamba mtu yeyote mwaminifu na mwenye uwezo, uzoefu na uadilifu ataingizwa katika utendaji wa serikali ili kuleta maendeleo makubwa yanayotarajiwa na wananchi.

Alitumia mkutano huu kuwaomba wazee wote nchini kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita katika juhudi zake za kuwahudumia wananchi.

“Tunaomba wazee mtuunge mkono katika hatua na mabadiliko haya tunayoenda kufanya kuanzia sasa, na haya tunayafanya kwa nia njema kabisa,” alisema Rais Samia.

Akiwa amezungumza kwa dakika 46, Rais Samia aliwahakikishia wazee na Watanzania kwamba serikali yake itasikiliza bila bezo wala dharau ushari wa kila Mtanzania, na hasa wazee na kwamba mengi yenye manufaa yatatekelezwa kwa dhati ili kuleta tija na maendeleo.

Katika mkutano huo Rais Samia aliozugumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee nchini Tanzania na kuahidi kuzitatua hatua kwa hatua.

Alisema kuwa Tanzania ina wazee kati ya  2,500,000 hadi 2,600,000, wakiwa ni watu wenye umri kuanzia miaka 60 na zaidi.

Alifafanua kwamba, tangu mwaka 2014, serikali imekuwa inatafakari kuwapatia stahiki wazee.

“Lakini kutokana na idadi kubwa ya wazee serikali bado inashindwa kuwapatia pensheni wazee hawa, hata kama ingekuwa ni shilingi 30,000 kwa mwezi,” alisema Rais Samia.

Hata hivyo, Rais Samia amewataka Watanzania kuendeleza utamaduni wa kuwatunza wazee katika familia zao badala ya kuiga utamaduni wa kigeni wa kuwatunza wazee katika kambi maalum za wazee.

Mbali na suala la wazee, Rais Samia pia alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kukomesha ujambazi na uporaji.

Katika ziara hiyo, Rais Samia aliambatana na Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima; na maofisa wengine wa ngazi za serikalini na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Like