Lowassa amegeuka mbilikimo wa kisiasa

MOJA ya mambo ambayo hayapingiki ni ukweli kwamba kama Edward Lowassa, waziri mkuu wa zamani wa Tanzania, angeteuliwa kugombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2015, asingehamia kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ukweli mwingine ni kuwa iwapo Dk. Willibord Slaa angekuwa jasiri, akamgomea mkewe, akabaki Chadema, na akachukua fomu ya urais, akashiriki mchakato wa kura ya maoni dhidi ya Lowassa, ndiye angeibuka mshindi, na angekuwa mgombea wa Chadema na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Upo ukweli mwingine. Lowassa huyu huyu, ambaye hatimaye aligombea urais kuitia Chadema, akaungwa mkono na Ukawa; kama angetangazwa mshindi wa urais, asingerejea CCM.

Kwa hiyo, haya yanayotokea sasa, ni sababu ya urais ulioshindikana. Mengine yote ni porojo za kisiasa na kupigania fursa binafsi ambazo ni mbadala wa urais.

Alinyang’anywa urais, na hakuwa na ubavu wa kupigania kura zake. Maisha ya kisiasa aliyokuta katika upinzani hakuyatarajia. Aina ya siasa alizowahi kufanya – za kidiplomasia na ushawishi, maandamano na mikutano ya hadhara, na mijumuiko ya wapambe – hazikupewa fursa katika awamu ya tano.

Amejaribu kuwa mpinzani katika muda mfupi, akabaini kuwa hawezi kabisa siasa za kikatili, za kukimbizwa na polisi, kushinda mahakamani, kupelekwa magerezani na kunyimwa dhamana, kutekwa na kupigwa risasi, na kufilisiwa kibiashara.

Maisha ambayo wenzake wameyaishi kwa miaka 30, yeye ameshindwa kuyaishi kwa miaka mitano. Pamoja na umarufu wake, kwa kitendo chake cha kushindwa misukosuko ya kisiasa na kujisalimisha CCM, anapopimwa dhidi wenzake aliowakuta Chadema kama Philemon Ndesamburo (hayati), Freeman Mbowe, Victor Kimesera (hayati), Sylvester Masinde, na waasisi wengine wa chama waliosota kwa miongo yote mitatu kukijenga, Lowassa anageuka mbilikimo wa kisiasa.

Kwa haiba hasi aliyokuwa amejengewa na wenzake hadi 2015, na upinzani ukashindilia, kwa heshima aliyopewa na “matibabu ya kisaikolojia na kimwili” aliyopatiwa na chama chake kipya (Chadema); kwa mahaba aliyoonyeshwa na Watanzania akiwa mgombea kupitia Ukawa; na kwamba sasa amerejea CCM kinyonge hivi, amekuwa kama  kambale aliyevuliwa kwenye matope, halafu akateleza kutoka kwenye tenga na kurejea “nyumbani,” katika matope, mtoni.

Lowassa amerudi matopeni CCM akisema amerudi “nyumbani.” Baadhi ya vijana wamekosoa kauli yake wakisema kuwa aliyerudi nyumbani ni Ruge Mutahaba; yeye Lowassa ameendelea kutangatanga tu kisiasa.

Kwa watetezi wa demokrasia, Lowassa hajafanya kosa lolote. Tunapigania demokrasia. Naye ameitumia, akaondoka. Ametekeleza demokrasia. Lakini tunafahamu ukweli zaidi ya hilo. Lowassa hakurejea CCM kwa hiari. Hakuomba, wala hakuombwa. Amelazimishwa.

Lakini kwa hakulazimishwa hivi hivi. Alijipendekeza, akaomba fadhila, naye akapewa sharti gumu mithili ya ombi la Herodia kwa Herode babaye – kichwa cha Yohane Mbatizaji kwenye kombe. Ilikuwa lazima kipatikane. (Soma Marko 6:17-28).

Anasema tusimuulize anarudi CCM kufanya nini. Hatuhitaji kumuuliza. Tunajua. Alidhani yeye ni mjanja, akadhani anaweza kufanya siasa za “majadiliano” na watesi wake badala ya kufanya “harakati” dhidi yao.

Aliomba miadi Ikulu Januari 2018, akaomba rais amnusuru mkwewe, Sioi Sumari, ambaye yupo gerezani kwa miaka mitatu sasa bila dhamana. Kosa! Alisahau maelfu ya watanzania wanaoozea magerezani, akahurumia mkwewe mmoja.

Magufuli alimpa Lowassa sharti moja tu: “rudi CCM, nitajua jinsi ya kumwachia.” Lowassa alithubutu kugoma, lakini kwa kuwa alishaonyesha udhaifu wake, doa iliutumia vema.

Mbali na kumfunga mkwewe, serikali ilimyang’anya pia mali zake. Lowassa ana mashamba Handeni. Serikali imetaifisha sehemu kubwa ya mashamba hayo. Mkoani Dodoma, serikali imechukua shamba lake. Kawe, Dar es Salaam, nyumba zake na biashara zake za kufua nguo, zimeathirika mno kwa kupandishiwa kodi isiyo na maelezo.

Huko Arusha, shamba lake la Olasit nalo lilichukuliwa. Zaidi ya hayo, alitishiwa kuwa na pensheni yake itafutwa. Huku njaa, huku afya, huku mkwe; akaona bora ajiunge nao ili apone.

Mwanzoni, aligoma. Lakini Rais John Magufuli aliona hii ni fursa ya kisiasa ambayo anageweza kuitumia kuhadaa wananchi. Akatuma watu wawili waliowahi kuwa karibu sana na Lowassa.

Wa kwanza ni Apson Mwang’onda, swahiba wa Lowassa, aliyewahi kuwa mkuu wa usalama wa taifa. Aliitwa Ikulu, Desemba 2018, na katika mazungumzo, aliombwa kufanya awezalo amrejeshe Lowassa.

Wa pili ni Rostam Azizi, mfanyabiashara maarufu ambaye kwa miaka mitatu mfulilizo hakuwa na uhusiano mzuri na Rais Magufuli wala Lowassa. Rostam hakubaliani na siasa za Rais Magufuli. Ni mwekezaji na “bepari” asiyekubaliana na mwenendo wa ujamaa uchwara wa Magufuli.

Tangu 2015, Rostam alihamisha vitega uchumi vyake vingi, akavipeleka nje ya nchi. Aliamini, kwa usahihi kabisa, kuwa Magufuli ataongoza nchi kwa sera za kulazimisha, zisizo na mazingira salama kwa uwekezaji na ushindani kibiashara; na kwamba ataua uchumi.

Kwa muda mrefu, Rostam alikuwa anaishi nje ya nchi, lakini katika namna ambayo haijapatiwa maelezo sahihi, alirejea nchini wakati mdogo wake Akram Azizi alipowekwa ndani, na akanyimwa dhamana, kwa kesi mbaya.

Rostam alionekana Ikulu akiteta na Rais Magufuli, baadaye akamsifia kuwa anafanya kazi nzuri. Baada ya muda mfupi, kesi ya mdogo wake iliisha.

Inafahamika kuwa moja ya masharti aliyopewa Rostam ni kumshawishi Lowassa arejee CCM. Ametimiza sharti hilo. Na hakuifanya kwa kificho. Siku Lowassa aliporejea CCM, hakwenda na mtu yeyote kutoka kwenye familia yake, bali aliambatana na Rostam. Bado wananchi wanahoji, “Rostam ni nani katika CCM na serikali ya Magufuli?”

Kwa hiyo, kama ilivyokuwa katika miaka ya awali ya urais wa Jakaya Kikwete, Rostam amepata tena fursa ya kuwa “king maker.” Sasa anaaminiwa na rais katika kupanga nani awe nani katika chama na serikali. 

Haishangazi kuwa “urafiki” wao huu ndio umesababisha umiliki wa Channel Ten, kuhamia kwa CCM. Rostam amekuwa ni mmoja wa wanahisa wakuu wa kituo hicho cha televisheni.

Zipo taarifa pia kuwa sababu mojawapo ya Rais Magufuli kuwaomba Mwang’onda na Rostam wamlete Lowassa ni kumdhibiti Bernard Membe, ambaye amekuwa anatajwa kuwa anaandaliwa na kambi moja ya wanaCCM kuwania urais 2020.

Lowassa na Membe wamekuwa kama chui na paka katika siasa za CCM. Kwa hiyo, kurejea kwa Lowassa unaweza kuwa ni mkakati wa Rais Magufuli kujiimarisha dhidi ya Membe, akimtumia Rostam na Lowassa.

Ipo sababu nyingine ya kisiasa. Nguvu ya kisiasa ya Lowassa iliisha 2015 pale alipozuia vijana “kutetea kura zake.” Ndani ya Chadema alibaki na heshima tu, lakini hakuwa na mamlaka wala uamuzi juu ya jambo lolote. Hata jitihada za watu wake kukamata chama zilishindikana. Wamekuwa wanaishi kwa kunung’unika.

Kwa wengi, alionekana “mwoga” na “mnyonge.” Hakushiriki hata programu cha chama kama viongozi wengine. Kwa sababu za mshikamano wa kisiasa, hata pale alipoteleza, alikemewa kiutu uzima bila umma kujua.

Hata zilipojitokeza fursa ambazo, katika hali ya kawaida zingefaa kutumiwa na mtu aliyekuwa mgombea urais kuikosoa serikali, badala ya kuonyesha mawazo mbadala, Lowassa “alipongeza serikali.” Alitamani kupendwa na wapinzani na CCM.

Sauti yake katika masuala ya kitaifa ilizidiwa na za wanasiasa wengine kama Tundu Lissu, Halima Mdee, John Heche, Esther Bulaya, Peter Msigwa, Godbless Lema na wengine. Taratibu, wananchi walianza kumsahau.

Ndani ya wiki aliyoondokea kurejea CCM, kuna utafiti uliomweka Lowassa nyuma ya Lissu na Zitto Kabwe wa ACT Wazalendo – katika kupima wanasiasa wenye ushawishi Tanzania.

Na hii ni baada ya Lissu kusema wazi kwamba yupo tayari kugombea urais 2020 iwapo Chadema na Ukawa watamkubali. Kwa sababu hiyo, wapo wanaodai kuwa Lowassa amemkimbia Lissu baada ya kusoma alama za nyakati na kugundua kwamba mlango wa 2020 umefungwa.

Hapo ongeza na shinikizo la binti yake ambaye mumewe amekaa ndani kwa miaka mitatu bila dhamana – huku rais ameshaahidi kumwachia iwapo “kichwa kitaletwa kwenye kombe.” Katika mazingira haya, ilikuwa rahisi kwa Rostam na Mwang’onda kumaliza biashara waliyotumwa na rais.

Haya yote yana maana gani? Lowassa amefuata njia ile ile ya Yuda. Amesaliti waliomuunga mkono akiwa katika wakati mgumu zaidi kisiasa na kiafya.

Na katika uamuzi wake huu wa sasa, anayefaidika ni yeye binafsi, wala si CCM. Sasa Lowassa ana uhakika wa pensheni yake kutofutwa; ana uhakika wa kurudishiwa mashamba yake; ana uhakika wa kutopandishiwa kodi za biashara zake; ana uhakika wa mkwewe kuachiwa baadaye.

Hiki ndicho baadhi ya watu wake wa karibu wasiokubaliana naye wanasema ni ubinafsi uliopitiliza. Mmoja wa watu hao ni Makongoro Mahanga, ambaye SAUTI KUBWA kuwa kwa kuwa umaarufu wake ulishapungua mno, Lowassa ameacha Chadema ikiwa salama.

Anaongeza: “Ni mbinafsi sana. Urais ulishindikana, lakini ametoka wakati ambapo hana athari yoyote kwa upinzani. Sana sana anaweza kuwa na athari kubwa kwa CCM kuliko upinzani.

“Kule, waliompokea walishamnyanyasa na kumtukana. Na kuna makundi hayamtaki. Hawawezi kuwa salama. Watafutaje yale waliyosema juu yake? Sisi wengine tulishaamua kupigania demokrasia. Wakati ule niliondoka CCM nikiwa na sababu kama tatu hivi. Sasa hivi kama ningekuwa bado nipo CCM ningekuwa na sababu zaidi ya saba za kuondoka.”

Wanufaika wa pili katika kuondoka kwa Lowassa ni upinzani. Licha ya kuwa hakuwa na nguvu ya wazi kisiasa au kiuongozi, haiba yake kama mgombea urais 2015 ilikuwa inaweka kivuli kikubwa katika kujadili na kuamua hatima yake kisiasa. Kilichompeleka upinzani ni urais.

Ni wazi kuwa hata leo, bado anautaka. Lakini anatambua kuwa kama angeamua kuwania tena, lingekuwa jaribio gumu kwake kupitia upinzani. Na zamu hii alitarajiwa kupata upinzani mkali ndnai ya Chadema. Nyota yake ilikuwa ya 2015. Aliizima mwenyewe.

Vile vile, kuondoka kwake kumefanya wengi wapumue, hata baadhi ya viongozi wenzake ambao walishaanza kumuona kama mzigo. Jambo pekee lililomfanya adumu nao ni ile nidhamu na mshikamano wa kiuongozi.

Yapo mambo kadhaa yanayohitaji mjadala na majibu. Wale wale waliomwibia kura zake, ndio amejiunga nao, na wanamtaka awasifu na kuwapongeza hadharani.

Wale wale ambao majuzi tu walisema “majizi yamekimbilia Chadema,” ndio wanatumia fedha za umma kumwandalia mikutano na kumwomba ahamasishe wananchi waliompa kura 2015, ili sasa waunge mkono yule aliyepewa kura za wizi.

Katika suala la ushawishi, anapoteza muda kama punda aliyerudi mjini Yerusalem bila kumbeba Yesu. Ataungwa mkono na wale wale wanaomshangilia, waliomzunguka, waliomnyima kura ambazo hazikutosha. 

Naye anatambua kuwa jukumu walilompa ni gumu, kwakuwa enzi zake zilishapita, lakini amejipima kwa hao aliowakimbia, na kwa huyo aliyemchukua – ambaye alikuwa anambeza – na amegundua kuwa yeye ndiye amekuwa mdogo. Sasa hivi amegeuka mbilikimo kisiasa.

Kwa kuwa ameondoka wakati nakamilisha kitabu cha historia ya mapambano ya vyama vingi tangu 1991, na moja ya sura zake ni jinsi Lowassa alivyoingia Chadema, nimeona nianze na hiyo kabla ya kurudi kwenye simulizi la mwanzo kabisa. Tufuatane baadaye wiki hii ili tujadili jinsi alivyojiunga na Chadema, na mikono iliyompokea na kumponya hadi akafika hapo ambapo Magufuli na wenzake wameona sasa ndiye mtu anayestahili kusaidia CCM ikubalike kwa Watanzania.

Like
13

Leave a Comment

Your email address will not be published.