IWAPO serikali ya Tanzania itaendeleza propaganda zake dhidi ya chanjo ya Corona, kuna uwezekano mkubwa wa Waislamu wa Tanzania kukosa fursa ya kwenda Hija mwaka huu, SAUTI KUBWA imeelezwa.
Taarifa tulizonazo zinasema Serikali ya Saudi Arabia inapanga kuweka zuio dhidi ya mtu yeyote ambaye hajachanjwa kuingia katika miji mitakatifu ya Makkah na Madinah.
Bila kitambulisho rasmi kinachoonyesha kuwa musical amechanjwa, itakuwa vigumu kuingia au kuvuka mipaka yote ya nchi hiyo ya Bara la Asia.
Julai kila mwaka, waamini wa Kiislamu “waliojaliwa,” husafiri kutoka maeneo mbalimbali duniani kwenda kufanya hija katika miji hiyo. Hija ni moja ya nguzo muhimu katika Uislamu.
Hadi siku chache zilizopita, Tanzania, kwa msimamo na matakwa ya Rais John Magufuli, kwa muda mrefu sasa, imekuwa ikidai “hakuna Corona.”
Hadi sasa Magufuli ameweka msimamo kuwa “serikali yake” haitapokea chanjo yoyote kutoka kwa “Mzungu.” Amekataa chanjo ya bure kupitia mpango maalum unaoratibiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Nchi zingine mbili zinazogomea chanjo na kukataa uwepo wa ugonjwa wa COVID-19 ni pamoja na Korea Kaskazini na Turkmenistan.
Waziri wa Afya wa Saudi Arabia, Tawfiq Al Rabiah jana alitoa mwongozo kwa taasisi zote nchini humo kuhakikisha kwamba watu wote wanaoajiriwa au kufanya kazi za kujitolea, lazima wapimwe Corona na kupewa kitambulisho kuwa ni wazima. Wale wanaokutwa na maambukizi hawataruhusiwa kufanya kazi zozote kabla na wakati wa mchakato wa hija.
“Nchi yetu imeathiriwa na Corona, lakini lazima tulinde watu wetu na ustawi wake kwa kudhibiti maamubukizi Zaidi,” ilisomeka sehemu ya mwongozo wa serikali ambao ulionwa na moja ya magazeti ya nchi hiyo liitwalo – Okaz.
Saudi Arabia tayari imepokea chanjo ya ugonjwa huo na kwamba imepanga kuchanja asilimia 70 ya wananchi wake ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Nchi hiyo ina watu wanaofikia milioni 35.
Katika hija ya mwaka jana, mahujaji 1000 tu ndiyo walioruhusiwa kutekeleza nguzo hiyo muhimu na serikali na taasisi zake, zilhakikisha kila hujaji anatekeleza matakwa ya kujikinga na ugonjwa huo.