Watanzania wana maisha magumu – ripoti

ZAIDI ya watu 600,000 nchini Tanzania wameingia kwenye mduara wa “umasikini wa kutupwa” na wanaishi magumu kutokana na mdororo wa uchumi – katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Mdororo huo wa uchumi unatokana na sera mbovu za uchumi na biashara, kutokuwa na vipaumbele kwenye mambo yanayokuza uchumi na kukwamisha ustawi wa jamii.

Jana, Ripoti ya Hali ya Uchumi Tanzania inayotolewa kila mwaka na Benki ya Dunia, inaonyesha kwamba idadi hiyo – ya watu 600,000, kutumbukia kwenye shimo la umasikini wa kutupwa ni sawa na asilimia 27.2 ya watu walionusurika kutoka kwenye kadhia hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja.

Pamoja na wachumi, wasomi na hata waandishi wa habari wa Tanzania kuogopa kueleza wazi juu ya anguko la uchumi na maisha kuwa magumu, taarifa zinaonyesha kuwa wananchi wengi wamepoteza ajira katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, hivyo kutokuwa na kipato.

“Inasikitisha wasomi wetu hawasemi, lakini uchumi wetu uko vibaya mno, hata kama serikali inatamba kukusanya fedha nyingi za kodi kila mwezi, watu hawana ajira, hivyo hakuna kipato na biashara zimefungwa,” anasema Dk. Julius Mwelu, mtaalamu wa uchumi na ushauri wa biashara wa Dar es Salaam.

Anasema kuwa wafanyabiashara wengi wamefunga shughuli zao kutokana na kubambikwa kodi kubwa, ushuru usioendana na bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi, wawekezaji kukwamishwa kutokana na mlolongo wa kuanza biashara na taratibu zinazokatisha tamaa kupitisha fedha nyingi Benki Kuu (BoT).

Katika uzinduzi wa ripoti hiyo ya 15 tangu kuanzishwa kwa utaratibu huo, Tanzania inaonekana imepoteza mapato makubwa katika kila sekta, ikiwamo utalii, ambayo katika kipindi cha mwaka 2019, ilikusanya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2.1, lakini mwaka jana imeambulia dola 483 milioni pekee.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa pato la taifa limeshuka kutoka asilimia 5.8 hadi kiwango kinachokadiriwa kuwa asilimia mbili.

Benki ya Dunia inashauri kwamba ili kuondoa watu wengi katika umasikini, serikali ifikirie namna nzuri ya kupanua mpango wa kunusuru kaya masikini na mingine ili kupunguza hatari kwa kaya hizo na kwamba katika kipindi kifupi, serikali iimarishe mbinu za kulinda ajira na kutoa msaada wa biashara ndogo na za kati.

Wachumi wa benki hiyo ya dunia wanaeleza kuwa mpango wa Tanzania kusaidia kaya masikini (Tasaf) bado ni finyu na kuwa hauonyeshi kinagaubaga namna unavyowakwamua masikini.

Dk. Mwelu anaeleza kuwa uamuzi wa serikali kuingiza fedha nyingi katika miradi mingi mkubwa katika kipindi kifupi, ni sababu nyingine ya kupungua kwa mzunguko wa fedha, hata kama apo wachache wanaofaidika na ajira katika miradi hiyo.

Anataja mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere, ujenzi wa reli ya kisasa, ununuzi wa ndege, kuwa ni uamuzi usiozingatia neema ya uchumi na ustawi wa jamii.

Katika uzinduzi huo jana, ripoti hiyo inaonesha kwamba janga la Corona pia limechangia kudorora kwa uchumi na ustawi wa jamii Tanzania, kama ilivyo kwa nchi nyingine.

Prof. Honest Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema pamoja na athari za ugonjwa wa Corona, zipo nchi kama Ghana na Kenya zilipunguza kodi kwa wafanyabiashara wake, hivyo kuwapa mwanya wa kuongeza juhudi kutengeneza faida, huku wakilipa kodi kwa wingi. Anasema anatamani hata sasa Tanznaia iige mfano huo.

Dk. Blandina Kilama, Mtafiti Mwandamizi, REPOA anasema Corona bado ni janga nab ado athari zake zipo na huenda zikaendelea kuonekana, hivyo ni vyema sasa serikali iweke mikakati ya kulinda rasilimali watu na kuhakikisha uzalishaji unaongeza huku ubunifu,kwa kutumia teknolojia ukiwekewa mkazo.

Like