Mpina amkaanga Makamba bungeni

Ahoji sababu ya kutodai Sh trilioni 1.2 kutoka IPTL na Arab Contactors

Ahofia usiri unaoleta mwanya wa mikataba ya upigaji katika miradi ya gesi

WAZIRI wa Nishati, Januari Makamba, ametakiwa kuueleza umma sababu ya kutodai fedha zaidi ya Tsh 1.2 Trilioni ambazo zilipaswa kulipwa na kampuni binafsi ya kufua umeme IPTL, na mkandarasi wa Bwawa
la Nyerere, Arab Contractors ya Misri.

Kibano hicho kimetolewa na Luhaga Mpina, Mbunge wa Kisesa, wakati akichangia Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2023/2024 bungeni jijini Dodoma wiki hii.

Mpina, amesema fedha hizo ni asilimia tano (5) ya bei ya mkataba ya ucheleweshaji wa mradi wa Bwawa la JNHPP na za kesi dhidi ya IPTL.

“Serikali imeshindwa kudai fidia ya ucheleweshaji Sh bilioni 327.93 kwa mwaka (kwa miaka miwili ni sawa na Sh bilioni 655). Waziri hajaeleza hatua zozote zinazochukuliwa na Serikali kudai fedha hizo, licha ya CAG kulalamikia eneo hili.

“Wizara na TANESCO wameshindwa kuidai IPTL Sh bilioni 342; madai halali baada ya Serikali kushinda kesi mahakamani tangu Machi 2021. Waziri aueleze umma (Bunge) wa Watanzania fedha zao ziko wapi?” anahoji Mpina.

Anasema Wizara ya Nishati na TANESCO wameshindwa kukusanya madai haya ya kisheria ambayo ni zaidi ya Sh bilioni 926 katika Bwawa la Mwalimu Nyerere, huku madai ya IPTL yakiwa ni Sh bilioni 342 na kufanya jumla yote kuwa ni Sh trilioni 1.268.

Mpina, aliyewahi kuwa waziri chini ya Rais Dk. John Magufuli, anasema kitendo cha waziri wa nishati kushindwa kueleza hatua zilizochukuliwa kukusanya fedha hizo kwa mujibu wa mkataba ni.dalili kwamba hana nia njema.

Aliwataka wabunge kutopitisha bajeti ya Makamba iwapo hatatoa maelezo ya kuridhisha kuhusu ukusanyaji wa fedha hizo. Hata hivyo, Bunge tayari limepitisha bajeti hiyo.

Kuhusu Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (Liquefied Natural Gas – LNG) ambao majadiliano baina ya Serikali na wawekezaji; Kampuni ya Shell ya Uingereza na Equinor ya Norway yamekamilika,  Mpina, amesema:

“Pamoja na kazi nzuri inayoendelea, changamoto ninazoziona ni hizi: Hakuna taarifa ya kufanyiwa mapitio ya PSA katika vitalu na 1, 2 na 4 vinavyokwenda kutumika licha ya Serikali kusimamisha mazungumzo hayo
mwaka 2019 baada ya kubaini kuwa Country’s Gas Production Sharing Agreement zilikuwa na kasoro na kulifanya taifa lisinufaike vya kutosha na akiba ya gesi asilia iliyopo. PSA hizo zilikuwa zinanufaisha kampuni za kigeni zinazokuja kuwekeza.

“Je, Government Negotiation Team (GNT) imefika hitimisho ya vipengele vya mikataba wa HGA na vitalu na 1, 2 na 4 kwa ajili ya mradi wa LNG kwa kutumia nyaraka gani au PSA zipi ili kulinda maslahi ya taifa katika mkataba huo?”

Mbunge huyo anasema usiri wa majadiliano katika vipengele vya mikataba ya LNG unaleta hofu kuhusu vigezo na masharti ya mikataba inayokwenda kuingiwa na ni kinyume na kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya The Tanzania Extractive Industries (Transparency and Accountability) Act 2015.

Sheria hiyo inataka miradi, leseni, vipengele na mikataba kuwekwa wazi kwenye tovuti na kutangazwa kwenye vyombo vya habari.

Mpina anashangaa ukimya uliopo TEITI wakati Makamba na genge lake wakifanya uvunjifu mkubwa wa sheria bila kushirikisha Bunge wala wadau wengine wakiwemo wananchi.

Mbunge huyo pia anataka kujua sababu za Serikali kuingia mkataba na Kampuni ya Baker Botts LLP ya Uingereza kama mshauri elekezi katika masuala ya teknolojia, kifedha na masoko ya kimataifa ili kuuza gesi
iliyogundulika kwa misingi ya ushindani na kulinda maslahi ya taifa lakini wakati huo mmoja wa wabia Kampuni ya Shell nayo inatoka Uingereza akihoji: “Hapa tunawezaje kuzuia mgongano wa maslahi?”

Anaonyesha hofu kuwa usiri uliopo kwenye mkataba ya LNG unaweza kugharimu taifa baadaye kwa kuingia mikataba mibovu.

“Nchi yetu haina rekodi nzuri katika eneo la mikataba ya raslimali zetu, hivyo waheshimiwa wabunge lazima tuwe makini sana tunapofanya uamuzi,” amesema.

Kwa upande mwingine, Mpina anataka Makamba fafanue kuhusu uhalali wa serikali kuingia mkataba na Kampuni ya Tech Mahindra ya india katika utekelezaji wa ujenzi wa mfumo wa TEHAMA wenye thamani ya Sh bilioni
70.

“Hatujaelezwa mradi huu umefikia wapi na umeisaidiaje Tanesco kuboresha mifumo yake ya TEHAMA? Je, TANESCO ilipata kibali cha Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kama hakuna uwezo wa ndani ya nchi wa kujenga mfumo huo?” anahoji.

Kuhusu mwenendo wa bei ya mafuta katika soko la ndani, Mpina anataka kujua sababu ya bei ya mafuta kuendelea kuwa juu pamoja na serikali kuingiza ruzuku ya Sh bilioni 100 kwa mwezi tangu mwaka jana, akitaka mchanganuo wa fedha hizo.

“Hapakufanyika tathmini ya kina wakati wa kuweka ruzuku ya mafuta ya Sh bilioni 100 kila mwezi, na sasa ruzuku hiyo imondolewa bila tathmini ya kina na bila Bunge kuhusishwa,” amesema.

Akihitimisha mchango wake, Mpina ametaka kujua ukweli wa taarifa za kuvunjwa kwa vituo vya miito ya simu za huduma kwa wateja vilivyokuwepo mikoani na kuunganishwa kuwa na kituo kimoja, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

“Kuna taarifa kuwa kituo hiki kimebinafsishwa. Je, ni sahihi kwa eneo nyeti kama hili kupewa kampuni binafsi? Taarifa zote nyeti za kutokea hitilafu za umeme, majanga ya moto kuripotiwa kupitia kampunibinafsi!” anashangaa Mpina.

Hata hivyo, Mpina hakupewa nafasi ya kutoa mchango huu mbele ya umma hivyo akalazimika kuuwasilisha kwa maandishi na sasa upo kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge

Akijibu hoja za Wabunge, Waziri Makamba alisema kuwa wamepokea kwa faraja yale yote yaliyowasilishwa na wachangiaji kuhusu bajeti ya wizara hiyo na wamepokea maoni yao na watayafanyia kazi.

‘Mheshimiwa spika, tumepokea maneno ya faraja kwetu katika mjadala wa bajeti hii, tumeyapokea na tumefurahi bajeti yetu imekuwa na hamasa kiasi hiki, na sisi maneno yanayosemwa tunayasikiliza na yanatusaidia tuwe makini zaidi,” alisema.

Aliongeza: “Pili haya maneno yanatuongezea hamu na hamasa ya kupata matokeo sisi hamasa yetu ni Imani ya Mheshimiwa Rais Kwetu na hamasa yetu matokeo ya kazi yetu kwa uhai wa chama chetu na hamasa nyingine
ni kuwasaidia Watanzania kwa majukumu tuliyopewa.”

Like
1