MASWALI MAGUMU YA IBRAHIM JEREMIAH, MKULIMA.WA SONGEA, KUHUSU MKATABA TATA WA BANDARI ZA TANZANIA

Rais Samia Suluhu Hassan

YAFUATAYO ni maswali muhimu yaliyoulizwa na “mkulima wa Songea,” Ibrahim Jeremiah, kuhusu mkataba tata wa bandari za Tanzania, ambao umeleta kelele kila kona. 

1. Ni utaratibu gani ulitumika kuipa Kandarasi Kampuni ya DP World;

Tulitangaza?
Ni makampuni gani yaliyoomba?
Ni vigezo vipi vya ziada viliipa ushindi wa Kandarasi hii Kampuni ya DP World?

2. Kwa mujibu wa Mkataba
Baada ya siku 30 za kusaini Mkataba wa Intergovernmental Agreement (IGA) Kampuni ya DPW ilianza kazi,
Je, Kampuni inawezaje kuanza kazi kabla ya mkataba kuridhiwa na kupitishwa na Bunge?

3. Rekodi ya Kampuni ya DP World ni mbaya kwasababu ilishaleta vurugu za 2014 Djibouti kutokana na mkataba Uliosainiwa mwaka 2008, Baada ya hizi vurugu ikalazimika kuvunjwa kwa mkataba mwaka 2018,
Kampuni hii pia haina rekodi ya kuongeza mapato ya asilimia 233 Kama Mh. Waziri alivyosema, Rekodi yake ya kuongeza mapato ni ya asilimia 20,
Serikali imewezaje kuiamini Kampuni hii?

4. Uwekezaji wa Dola milioni 500 ambayo ni sawa na Trilioni 1.2 si uwekezaji mkubwa ambao tunaushindwa, ni uwekezaji ambao tunaumudu,
Kwanini uwekezaji huu usifanywe na Watanzania kupitia Serikali ama mfumo wa hisa ili manufaa yote ya uwekezaji yainufaishe Tanzania?

5. Viongozi wa Wizara za Ujenzi na Uchukuzi na mamlaka za Bandari hawaoni mkataba huu unaonesha kuwa wao hawana sifa na vigezo vya kuweza kuongoza Bandari zetu?

Kama Kampuni ya DP World inaweza kusimamia Bandari za Dubai, Benbera, Luanda, Dakar, Sokhna na kwingineko iweje wao washindwe kusimamia Bandari za Tanzania pekee?

Kwanini Viongozi hawa wasijiuzulu wapishe Watanzania wengine waongoze?

6. Dubai haina kiti katika Umoja wa Mataifa, Ipo chini ya Falme za Kiarabu kwa mantiki hii haina mamlaka ya kusaini mikataba ya Kimataifa kwa hili tu inaonesha kuwa mkataba huu ni haramu.

Tanbihi: Para 6. Ni kweli “Emirate of Dubai” ni sehemu ya U.A.E na U.A.E ndio member wa UN. Hoja hapa je Emirate of Dubai inaweza kuingia mkataba wa kimataifa kama huu mkataba unavyodai?

7. Tanzania ni Jamhuri ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar na kuna wizara za Muungano na wizara zisizo za Muungano,
Inakuwaje Mkataba huu nyeti, muhimu na roho ya Uchumi wa Tanganyika usainiwe na Mh. Makame Mbarawa ambaye ni raia wa Zanzibar ?

Hatuoni kufanya hivi kutaleta mtafaruku katika Muungano wetu?

8. Ibara ya 12 inaelezea kuhusu masuala ya Ulinzi na Usalama
Ibara hii kipengele cha pili inasema kuwa Kampuni ya DP World itawajibika katika masuala ya Ulinzi na Usalama wa Bandari,
Hatuoni hii itahatarisha Usalama wa nchi yetu hasa ukizingatia tuhuma nyingi inazopewa Dubai za kuiba Rasilimali za Afrika hususani Madini ambapo wizi mkubwa wa madini unafanyikia Dubai, Wanyama ambapo taarifa zimetolewa kuwa wamerengeneza Mbuga za Wanyama waliowachukua toka Afrika, Upitishaji wa Madawa ya kulevya, Silaha n.k

9. Ajira
Kwa makampuni ya Kiarabu Ajira kubwa na nzuri nyingi hupewa watu wenye ngozi za kiarabu na watu wenye Imani ya Kidini inayofanana nao,

Hili mnaweza kulifanyia utafiti na mtalipatia majibu,

Nchi yetu ni nchi ya Waafrika weusi wengi kwa asilimia 99 na wenye Imani zote za Kidini,

Je, hatuoni uwekezaji huu utaleta ubaguzi, utaondoa umoja wa Kitaifa na kuleta vurugu hapo baadae?

10. Katika Ibara ya 19 inazitaka Serikali zijazo (Vizazi vijavyo) kurithi mkataba
Lakini pia mkataba huu unaonesha kuwa Serikali ya sasa ama zijazo hazitakuwa na mamlaka ya kuuvunja mkataba huu,

Je, hatuoni kuwa kuingia mkataba huu ni kuua matumaini ya watoto wetu, wajuu zetu na vizazi vyetu?

Je, hatuoni kuwa tunaingilia uhuru wa vizazi vijavyo vya Tanzania kujipangia sera na mipango yao?

Je, Kama tukiingia mikataba ya aina hii kwenye Ardhi, Madini na Bandari, Vizazi vijavyo vitaishije?

11. Hapo mwanzo tulikuwa na mkataba wa TICTS ambao ulilalamikiwa sana na Watanzania,
Je, kwa hali hii ya mkataba huu tunaenda kuzuri ama ndio tunakwenda kubaya mara elfu zaidi?

12. Ibara ya 26 inaonesha mkataba huu upo juu ya sheria, upo juu ya katiba na umekwenda mbali upo juu ya sheria za Kimataifa,
Hatuoni kuwa na mkataba huu ni kuisigina katiba?

13. Ibara ya tano inazungumzia haki za ardhi
Katika ibara hii kuna maneno ya Kiingereza yameandikwa The company will have the ability to posses the land, Ukienda kwenye tafsiri ya negotiate posses linamaanisha kumiliki,
Je, ikiwa mkataba huu utatoa mamlaka ya kumiliki ardhi kwa Kampuni ya Dubai hatuoni kuwa tumekwenda kinyume na Katiba?

14. Kwa kuzingatia umuhimu na Unyeti wa Bandari hususani kwenye Jamii ambayo ndio mmiliki, Uchumi na Usalama,
Kwanini mkataba wa Ubinafsishwaji wake uwe na usiri mkubwa?

15. Ikiwa tumebinafishwa Bandari, Ikiwa umiliki wa Bandari katika kipindi cha Ubinafsishwaji utakuwa ni wa asilimia 100 kwa Kampuni ya DP World/Uongozi wa Dubai yakiwemo masuala ya Ulinzi na Usalama kwa mujibu wa Ibara ya 12,
Je, maeneo yetu ya Bandari yatakuwa chini ya Serikali ya Tanzania ama yatakuwa chini ya Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu?

16. Ibara ya 21 inazungumzia governing laws kuwa tutatumia sheria za Uingereza na iwapo kutakuwa na mgogoro urapelekwa kutatuliwa kwenye baraza la usuluhishi,
Je, hatuoni kufanya hivi ni kuzinajisi sheria zetu?

Ikiwa sheria zetu za uwekezaji na Mahakama zetu ni mbaya ni Kwanini tusirekebishe kuliko kutumia sheria za Mataifa mengine?

Je, ukitokea mgogoro kwa nguvu ya kifedha ya Dubai tutaweza kupambana nayo kwenye mabaraza ya usuluhishi?

17. Dubai tumewazidi maarifa, tumewazidi nguvu kazi, wao wametuzidi fedha kwasababu hata teknolojia hawana nao wananunua toka katika Mataifa mengine,

Trilioni 1.2
Kwanini tusiwekeze sisi wenyewe?

18. Je, Accounts za kifedha zitakuwa kwenye Mabenki yetu hapa nchini ama kwenye Mabenki ya Dubai?

19. Je, hatuoni kuwa huu mkataba unaoutweza Uhuru wetu na kutuondolea sovereignty yetu?

20. Ni hatua gani zilichukuliwa kuhakikisha zoezi la mlolongo wa kupitisha mkataba huu haliathiriwi na Rushwa, Ufisadi na Conflict of interest kwa baadhi ya Watanzania wenzetu wenye dhamana wasio waadilifu?

Kwanini mkataba huu umekimbizwa kwa haraka bila ushirikishwaji wa kutosha wa wananchi, wadau na wawakilishi?

Haya ni maswali yangu machache kwa heshima na taadhima nitaomba kwa niaba ya Watanzania yajibiwe,

NB: Mkataba huu uvunjwe/usitishwe/ubatilishwe ni wa ovyo, haufai na haramu kwa Taifa la sasa na la baadaye.

Like
3