Mke wa Rais Magufuli naye mgonjwa? Azuiwa kumwona mumewe hospitalini

WAKATI uvumi juu ya afya ya Rais John Magufuli ukiendelea na serikali ikigoma kutoa taarifa rasmi, imebainika kuwa hata mkewe Janet (61) hana taarifa za hali ya mumewe kwa sababu amezuiwa kumwona.

“Janet hajui kabisa aliko mumewe. Hajui kama ni mgonjwa au mzima,” chanzo kimoja kimeiambia SAUTI KUBWA.

Janet hajaonekana hadharani kwa takribani siku 50 sasa, wakati mumewe hajaonekana hadharani kwa takribani siku 20. Habari kutoka kwa watu wake wa karibu zinasema naye amekuwa anaumwa hata kabla ya mumewe.

Baadhi ya wasaidizi wake wa karibu na maofisa kwenye makazi yake – Ikulu Dar es Salaam na Dodoma – wameiambia SAUTI KUBWA kwamba naye alipata “changamoto ya upumuaji” mwanzoni mwa Februari, 2021.

SAUTI KUBWA imeelezwa kwamba baada ya yeye kugundulika kuwa na maambukizi hayo, mumewe alimshauri aendelea kutumia “tiba” za asili, ikiwamo kujifukiza.

Hata hivyo, daktari wa familia Profesa Mabula Mchembe alishauri Janet atumie pia dawa nyingine za hospitali, ambazo hazijafahamika ni zipi na kama zimethibitishwa kutibu changamoto hizo za upumuaji.

Inaelezwa kwamba mke huyo wa Rais Magufuli alipendekeza  warudi Ikulu ya Dar es Salaam ili wawe karibu na daktari  mwingine wa familia.

Kumekuwepo siri kuu kuhusu kuumwa kwa Janet na iwapo hicho kinachotajwa kuwa ni changamoto ya upumuaji ni Corona au vinginevyo. Zipo taarifa kuwa sasa anaendelea vizuri.

Familia ya karibu ya kiongozi huyo, wakiwamo watoto wake, nao hawana taarifa ya afya za baba yao, baada ya kuwepo usiri mkubwa unaodhibitiwa na vyombo vya ulinzi na usalama kwa uratibu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).

Taarifa zilizoifikia SAUTI KUBWA zinaeleza kuwa Janet aliruhusiwa kumuona mumewe kwa siku kadhaa mara baada ya kupata kiharusi, akiwa Ikulu, Dar es Salaam.

Hakuna taarifa za uhakika ni lini hasa alikumbwa na kupooza huko, ingawa inafahamika kuwa Rais Magufuli ana matatizo ya ugonjwa wa moyo.

Hata hivyo, afya ya Rais Magufuli ilipozorota zaidi siku 10 zilizopita, Janet alizuiwa kumuona mumewe kwa maelekezo ya TISS.

Inaelezwa kuwa katika kudhibiti hali ya afya ya Rais Magufuli kusambaa kwa umma, vyombo vya usalama vimezuia familia ya kiongozi huyo wa nchi, akiwamo mkewe na Watoto kutumia simu za mkononi.

Habari hizi za kuugua kwa mke huyo wa Rais Magufuli zimeifikia SAUTI KUBWA wakati dunia nzima ikihoji alipo mumewe baada ya kutoonekana hadharani kwa kipindi cha karibu wiki tatu sasa.

Tayari imethibitishwa kwamba Rais Magufuli anaumwa, ingawa kama inavyokuwa kwa ugonjwa wa mkewe, habari zinafichwa kwa kiwango kikubwa na serikali, hasa kwa uratibu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Kutokana na hofu iliyovikumba vyombo vya habari vya Tanzania haviwezi kuandika habari zozote za hali ya afya ya Rais Magufuli hadi viongozi wa seriakali wanapotoa matamko chanya kuhusu rais.

SAUTI KUBWA imebeba jukumu hilo katika mazingira ya usiri uliopitiliza ambao umezaa tetesi na uvumi mwingi kuhusu afya ya rais.

Vyombo vingine vinavyoheshimika duniani ikiwamo Aljazeera, BBC, DW na vingine vingi, vimekuwa vikifuatilia habari za kutoonekana hadharani na ugonjwa unaomsumbua Rais Magufuli.

Like
26