MBOWE ATIKISA NYARUGUSU

– Asema dhahabu ni fursa, lakini watawala wameigeuza mkosi kwa wananchi
– Alia na mikataba mibovu, ufisadi vinavyotesa wananchi

Freeman Mbowe

AKIHUTUBIA maelfu ya wananchi wa Nyarugusu, mkoani wa Geita, hivi punde, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amesema ufisadi na sera mbaya za CCM zisizojali wananchi, zimewaacha wananchi wa Nyarugusu, wenye migodi mingi ya dhahabu, kwenye umaskini mkubwa.

“Dhahabu ni fursa, lakini kwa sababu ya ufisadi na uongozi mbovu wa CCM, dhahabu imekuwa ni mkosi kwenu. Mna dhahabu lakini wote choka mbaya, mna dhahabu na ziwa Victoria lakini hamna maji safi na salama ya kunywa, huduma za afya ni mbovu. Mikataba mibovu ya madini na ufisadi wa serikali ya CCM vimewaacha kwenye umaskini,” alisema.

Mwanasiasa huyo amewahamasisha wananchi wa Nyarugusu kujiunga na kujisajili rasmi kwa wingi kuwa wanachama wa Chadema, ikiwa ni maandalizi ya msingi ya kujikomboa kutoka katika utawala usiowajali wa CCM.

Alisema Chadema ikichukua dola itaanzisha mfumo wa utawala wa serikali ya majimbo ambao utahakikisha wananchi wanaanza kunufaika na utajiri wa raslimali zilizopo kwenye maeneo yao kwanza kabla ya sehemu ya mapato ya raslimali hizo kuchangia maendeleo ya sehemu nyingine za nchi.

Pichani juu ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (BAWACHA) Mkoa wa Kagera, Pendo Ngonyani, akihutubia katika moja ya mikutano ya Mbowe mkoani Kagera, kwenye Kata ya Nemba, Biharamulo, leo kabla ya msafara wake kuanza ziara katika mkoa wa Geita. 

Like