BARUA YA WAZI KWA RAIS SAMIA (4)

Rais Samia Suluhu Hassan

Ifuatayo ni sehemu ya nne na ya mwisho ya uchambuzi wa kitaalamu juu ya uchumi wetu katika muktadha wa mkataba wa bandari kati ya Tanzania na DP World ya Dubai. Ni barua ya wazi ambayo pia ni ushauri mwanana kwa Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wa masuala ya uchumi. Endelea.

UCHAMBUZI MAKINI WA SERA BADALA YA MIRADI YA KIMKAKATI

Mheshimiwa rais, nchi yetu imekuwa na miradi kochokocho ya kimkakati kwa miaka na mikaka sasa. Tumekuwa na miradi hii kwa mjina mengi, kama miradi kielelezo( flagship projects), miradi ya kimkakati au miradi muhimu ya serikali. Miradi hii imekuwa ikichukuliwa kama njia ya uhakika ya kutuvusha na hata pale ilipoonesha haina uwezo huo, hoja zimekuwa matokeo yake ni ya muda mrefu.

Miradi ya aina hii imekuwepo kwa muda mrefu lakini ya hivi karibuni ni kuimarisha shirika la ndege, reli ya kisasa, madaraja ya kulipia, kuhamia Dodoma, bwawa la Mwalimu Nyerere, barabara za tozo na mingine mingi.

Mheshimiwa rais, sina hoja ya kupinga umuhimu wa miradi ya aina hii. Hoja yangu ni jinsi miradi hii inavyobuniwa na kutekelezwa. Miradi hii pamoja na kuwa na nia nzuri na kuitwa miradi ya kimkakati, inakuwa na nakisi ya mazingira ya kimkakati kiuchumi.

Miradi hii ni matokeo ya mipango ya kueleza kuwa tunafanya mambo ya kiuchumi kwa lugha nyingi za taaluma ya uchumi (Economics) lakini zenye maudhui hafifu ya mfumo wa kiuchumi (The Economy). 

Mheshimiwa rais, hali hii imetukumba zaidi kwenye miaka ambayo, tumejaribu njia ya kuufanya uchumi wetu kuwa wa kiutandawazi. Kwenye kufanya hivi, tumekiuka kanuni kuu ya msingi ambayo ni; ubunifu na uchambuzi makini na wa kina wa hali ya uchumi, maana ya hali ya uchumi wetu kwenye uchumi wa kikanda na kidunia na tafsiri ya muda mrefu ya hayo mawili.

Hapa uchambuzi, si ule wa  taarifa tunazosoma bungeni kuhusu hali ya uchumi wa dunia na wa Tanzania kila mwaka wa bajeti. Huu ni uchambuzi wa sera kiuchumi, unaozingatia rasilimali kuu tatu kwa mfuatano maalum. Ambao ni:

 1. Mamlaka ya kisiasa.
 2. Muda wa kuratibu na kutekeleza sera.
 3. Rasilimali Fedha.

Kwa mfano, kwa kusisitiza kuwa; hoja inatakiwa kuwa miradi ya kimkakati badala ya uchambuzi wa kina wa sera za kiuchumi, tumejikuta tunaanza na rasilimali fedha badala ya rasilimali mbili za awali. Hapa tumekuwa tunakwenda popote tunakoweza kupata, na kuwekeza kwenye chochote ambacho mwenye fedha angependa tuwekeze au anakopigia chapuo kwa muelekeo wa siasa zake kidunia kwa wakati huo na kwa njia yotoyote ya kiuwekezaji.

Uwekezaji wa kwenye miundombinu ya kila aina umekuwa biashara kubwa duniani kwa mashirika makubwa ya fedha na nchi tajiri duniani. Kupitia mikopo kutoka nchi hizo, zimekuwa na uhakika wa kuamua mwelekeo wa kisera wa nchi zinazopokea mikopo hiyo.

Na hapa kwetu, hali siyo tofauti kwani uwekezaji wa aina hiyo umekuwa na mafungamano ya uhasibu wa Pato Ghafi (GDP Accounting) badala ya mfungamano wa kiuchumi (Economic connection) ambayo ina changamoto kwenye uchumi halisi, ukuaji wa uchumi wenye usawa na hoja hafifu ya kuwa; uchumi ni makusanyo ya mapato miongoni mwa athari lukuki kama nilivyokwisha kueleza huko mwanzo kwenye hoja hizi.

Tumekuwa na mwelekeo huu kwenye sekta za huduma kama mawasiliano, mwelekeo wa aina hii kwenye uwekezaji wa rasilimali za asili kama madini na gasi na sasa mwelekeo huo kwenye rasilimali za bahari na mito.

Mheshimiwa rais, naomba kutumia hoja za utetetezi wa uwekezaji wa kwenye bandari kupitia mkataba uliopo kwenye umma kutoa mifano hai.

 1. Trillion ishirini na sita za Kitanzania

Hii imekuwa hoja maarufu ya kwa nini tuwe na aina ya mkataba tulionao kuwekeza kwenye bandari. Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote wa kisayansi kuonesha mapato hayo kutoka kwenye uwekezaji unaokusudiwa.

Aidha, hata kama kungekuwa na ushahidi wa kisayansi, bado ushahidi huo usingeweza kuonesha kuonesha kiwango hicho cha mapato.

Hii ni kwa sababu, hata kama umefanya uchanganuzi wa kifedha(financial modelling) kwa kutumia taarifa za uwekezaji wa kampuni ya DP World nchi zingine ambako aina ya uwekezaji unaotajwa Tanzania ni kama wa nchi hizo, bado ungeishia kupata mapato ghafi ya shilingi trillion kumi na tatu (13 Trillion) kwa kipindi cha muda mfupi wa miaka mitano(5). Na mapato ya moja kwa moja kwa serikali kila mwaka yasiyozidi shilingi trilioni saba (7 Trillion).

Ushahidi huo ungeweza kuonesha kuwa tungepata kiwango hicho cha fedha hata kwa mikakati iliyopo sasa na inayoendelea ndani ya kipindi hicho.

Kwenye ajenda ya kutanua mawanda ya hoja hiyo, inasemwa kuwa mapato haya yataongeza bajeti kwa Trillion ishirini na sita kwa fedha za Kitanzania. Hii siyo tu kuwa inaonesha nakisi ya mipango kwenye kuendesha uchumi wetu, zaidi inaonesha kutokujali kwetu kuhusu eneo muhimu la uchumi wetu la mipango kwenye sekta ya fedha za umma (Public Finance).

Hata hivyo, mambo haya ya kurusha tu tarakimu ni kwa sababu kubwa mbili nilizokwisha kuzitaja ,na yafaa nizirudie. Moja ni kufikiria uchumi kuwa ni makusanyo ya mapato na pili, ni kutokuwa na kiini cha uchambuzi endelevu wa kuvuna rasilimali za asili kuwa rasilimali za kiuchumi.

 1. Ajira zitaongezeka

Hoja hii nayo inatokana na sababu zilezile. Lakini haina uhalisia kiuchumi.

Hoja hii imejikita kwenye nakisi ya mizania ya uchumi. Uwekezaji wa bandarini ni uwekezaji ambao wachumi wanaita capital intensive (uwekezaji wa mitaji na teknolojia). Kwa kawaida, uwekezaji wa aina hii, siyo tu kuwa unakuja na ajira kidogo sana, lakini pia hupunguza ajira za awali kwenye miradi husika.

Na hilo si jambo baya ikiwa uwekezaji huo unatengeneza faida msambao kwenye sekta zingine  hasa ambazo zinahitaji nguvu kazi, yaani labour intensive. Kwa taarifa rasmi za Seafright Insight; kwenye maeneo  thelathini na mbili (32) ambako DP World wamewekeza uwekezaji wa kisasa kama tunaoelezwa hapa kati uwekezaji wao jumla kwenye maeneo sitini na tisa(69), kwenye miaka miwili ya awali, ajira zaidi ya asilimi sitini na nane(68%) zilizokuwepo zilipotea. Hoja hapa, kwa nini tunadhani kuwa teknolojia hiyo itafanya vinginevyo hapa?.

Mheshimiwa rais, hoja hizi za mapato na ajira zingeweza kuwa bayana kwenye mipango yetu kama tungekuwa na uchambuzi wa kina na makini kwenye sera. Au hata kama kungekuwa na utamaduni wa uchambuzi wa ndani kabla ya waelimishaji wa umma ili walau wasema yale yanayowezekana.

Tutawapa wawekezaji 8% ya shughuli za bandari

Hii ni hoja ya hivi karibuni ili kujibu maswali ya kwa nini bandari yetu tuwaachie wawekezaji wa nje. Hata hivyo, hoja hii ina shida kubwa mbili.

 1. Gati namba moja hadi 7 haiwezi kuwa 8% ya shughuli za bandari yetu kwa maana maeneo yanayofanya kazi.
 2. Kama TPA na waliokuwepo walikuwa hawapati hata nusu ya Trillion ishirini na sita zinazotajwa kutokana na uwekezaji huu na wakati walikuwa na eneo lote, inawezekanaje mwekezaji anayepewa 8% atuwezeshe kupata Trilioni 26?

Hoja za namna hii ni hoja za kufunika makosa ya kutokuwa na uchambuzi makini na wa kina kuhusu uwekezaji tunaotaka kwenye nchi yetu.

Kuwasiliana Juu ya Mambo ya Uchumi

Mheshimiwa rais, hoja yangu ya tano kwenye barua hii ndefu ni ya jinsi ya kuwasiliana juu ya masuala ya kiuchumi nchini. Japo inaweza kuonekana kuwa hili siyo eneo muhimu sana kwenye kuendesha uchumi wa nchi; lakini tafiti nyingi zinaonesha kuwa; ubora wa mawasiliano kati ya watunga sera na umma, kati ya serikali na watunga sera, kati ya umma na wanahabari;ni jambo muhimu sana kwenye kuendesha uchumi wa kileo.

Kwa watunga sera ni njia nzuri ya kuleta imani kwenye uchumi (Economic Confidence) ambayo ni nguzo muhimu kwa watumiaji (Consumers) kwenye uchumi na kuwa na hakika ya yanayotarajiwa.

Kwa wawekezaji ni njia muhimu ya kujua usalama wa mitaji yao na mazingira ya siku usoni kwenye uchumi. Kwa hiyo ni nguzo muhimu ya kimahusiano kati ya wawekezaji na serikali.

Kwa serikali, ni zana ya uhakika ya kufikia maamuzi yenye nafasi ndogo ya kutengeneza matatizo ya kesho kwenye njia zilezile za uchumi kutokana na maamuzi ya leo.

Kwa ujumla ni njia kuu ya mfumo wa uchumi na wanaoendesha uchumi huo kutengeneza matumaini halisi kwa wananchi.

Moja ya mambo ambayo yamekuwa na changamoto kwenye uchumi wetu ni jinsi serikali inavyofanya mawasiliano hayo hata pale inapokuwa na imefikia uamuzi fulani kwa uchambuzi makini na wa kina. Na hapa changamoto kuu ni zifuatazo.

 1. Ukosefu wa wataalam wa mawasiliano kwenye masuala ya kiuchumi na hasa uchumi mpana.
 2. Ofisi za wasemaji wa serikali zisizo na wachambuzi wa sera wenye maarifa ya maeneo husika.
 3. Ukosefu wa mikakati ya mawasiliano inayosababisha
 4. kuwa na ujumbe tofauti kati ya wizara na msemaji wa serikali au kati ya wanasiasa na wizara au idara na idara kama iliivyojionesha kwenye suala la uwekezaji kwenye bandari.

MAPENDEKEZO

MMheshimiwa rais, msingi wa mapendekezo haya, siyo kuwa najaribu kusema kazi ya kuendesha uchumi ni rahisi. Nafahamu kuwa; kama njia ya kupata mapendekezo na kuyafanyia kazi ingekuwa rahisi, basi nchi zote zingekuwa tajiri.

Ni kwa msingi huo, nafahamu pia, kuwa; kuendesha uchumi si kazi ambayo unaweza kupata majibu kwa kuambiwa au kugugo. Hata hivyo, nafahamu  kuwa; ni kazi ambayo kimsingi, inahusu jinsi ya wanaoendesha uchumi wanavyofikiri. Na mimi naomba kuchangia juu ya fikra hizo.

Mosi, ni kuhusu hoja ya bandari.

Kama nilivyoeleza hapo awali, kwa kuzingatia mkataba ulioko kwenye umma na kwa kutilia maanani mjadala kwenye umma na maelezo ya serikali; ni dhahiri kuwa hatua ya sasa kuhusu suala hili haihitaji udharura bali uamuzi mpya na ulijaa uchambuzi makini na wa kina

MMheshimiwa rais, ikiwa utaona inafaa, nashauri mambo makuu mawili kwako.

Moja, “Samia Shock

MMheshimiwa rais, wewe ndiye Jerali mkuu kwenye vita hii ya kiuchumi. Wewe, ndiye unayeona zaidi ya majenerali wasaidizi. Wewe, ndiye mwenye nafasi na uwezo kutumia kila silaha inayoweza kusaidia nchi kufikiri zaidi juu ya uamuzi wowote wa nchi.  Kwa kutumia nafasi hiyo unaweza kubadili uamuzi na ukalishtua taifa japo kwa nia ya kupata matokeo bora zaidi.

Kama alivyofanya rais wa zamani wa Marekani, Richard Nixon, mwaka (1971) kwenye mfululizo wa mamuzi ya kiuchumi lakini kubwa yakiwa mamuzi ya kukabiliana na mfumuko wa bei kwa kuzuia kupandisha bei ya bidhaa na kupandisha mishahara kwa siku tisini (90) kinyume na matarajio ya waliokuwa wakipigania hoja ya kuliacha soko liamue; unayo nafasi mheshimiwa rais, ya kuamua kinyume na wanaosema kuwa hii ni hoja ya uchumi wa soko. 

Mheshimiwa rais, hii siyo hoja ya uchumi wa soko kama nilivyojaribu kujieleza mwanzo. Hii ni hoja inayohusu maslahi ya haki za pana za kiuchumi dhidi ya haki hafifu za muda mfupi za kibiashara.

Pili, Kutumia Daraja la Dhahabu

Mheshimiwa rais, kama anavyoandika San Tzu kwenye The Art of War kuwa; kwenye mapambano zipo nyakati ambazo pande zinazopambana hufikia hatua ya kuwa na  daraja la dhahabu ili kuepusha maafa zaidi. Hapa pande zote huamsha mikono na kuamua kusitisha mapigano na kuchagua sehemu moja ya kuzika wale waliowapoteza kwenye mapambano.

Mheshimiwa rais, ikiwa unaona inafaa; unaweza kuamua lifikiwe daraja la dhahabu kwenye sakata hili, kwani ni dhahiri linalipasua taifa sasa. Unaweza kuwataka wanaounga mkono wakiongozwa na serikali yako na wale wanaopinga, kufunga mjadala huu na kwa pamoja kukubaliana juu ya Samia Shock kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Mheshimiwa rais, kwenye hili, unaweza kuwaeleza wale wanaosema utumia ushupavu wa uongozi kwa kutokuangalia nyuma kuwa; hakuna ushupavu wa uongozi unaozidi uamuzi wa kulilinda taifa lako dhidi ya mipasuko inayoweza kuzamisha hata hizo ndoto njema za manufaa ya uwekezaji.

Mosi ni kuhusu Uchumi kwa Ujumla.

Mheshimiwa rais, kuhusu uchumi wetu kwa ujumla, unayo nafasi nzuri sana ya kubadili mfumo wa uchumi wetu kwa kubadili jinsi waendesha uchumi wanavyofikiri kuhusu uchumi wetu Kwa njia hii, tunaweza kuyaona mambo madogo kwenye uchumi lakini yanayoathiri matokeo ya mipango mikubwa.

Pili ni kuhusu uchumi Jumla.

UCHUMI JUMLA

Mheshimiwa rais, kwa unyenyekevu, naomba, kupendekeza yafuatayo kwenye jitihada za kubadili hali ya uchumi wetu.

Mosi, Kuandaa Dira ya Maendeleo 2050 inayojikita kwenye masuala ya msingi ya uchambuzi halisi. Ni muhimu dira hii kuiweka hoja ya Pato Ghafi kama hatua tu ya uchumi kusimama badala ya kuiona kama kipimo jumla cha afya ya uchumi. Hii ni pamoja kuzingatia yafuatayo;

 1. Kuhakikisha mipango ya kibiashara inakuwa ni matokeo ya maono mapana ya uchumi wetu na siyo kinyume chake.
 2. Taasisi za kiuchumi kuwa kwenye kitovu cha mipango yetu badala ya rasilimali fedha.
 3. Kuwekeza zaidi kwenye uchumi(the economy) badala ya tunachokiita maendeleo.
 4. Kuimarisha ukuaji wa tija kwenye uchumi mpana badala ya tija kwenye kampuni za kibiashara pekee. Hii itasaidia kuwa na ukuaji halisi kutokana na Mitaji, Tija na Pato Ghafi.
 5. Kuwekeza zaidi kwenye maarifa ya uchambuzi wa kina na sera badala ya maarifa kwenye kubuni miradi kielelezo.
 6. Kuwekeza Ofisi ya msemaji mkuu wa serikali kuhusu masuala ya uchumi mpana na sera. 

Pili, Kuwa na Industrial Policy inayoeleweka.

Mheshimiwa rais, nimetumia neno la kiingereza kwa sababu nakusudia kusema; sera maalum ya nchi ya maeneo ya kimkakati Kiuchumi ambayo inalenga kuwa nguzo ya maendeleo na mikakati hii lazima ilindwe na serikali bila tu kuiacha mikononi mwa soko la dunia ambalo hatuna uwezo wa kulidhibiti. 

Mheshimiwa rais, nchi zote duniani, zimeendelea kwa kuwa na Industrial Policy

Tatu, Kutumia sheria kama zana ya uchumi mpana bila kuiweka sheria kama mbadala wa mikakati ya kiutawala.

Mheshimiwa rais, kufanya hivi kutatusadia mambo makuu mawili.

 1. Kuweza kuhakikisha tunaepuka migogogoro ya kiuwekezaji. Tutaweza kulifikia hilo kwa sababu itakuwa rahisi kujua mantiki ya sheria za kibiashara za kimataifa ambazo hazioani na mantiki ya mikakati ya uchumi wetu.

Mheshimiwa rais, mara nyingi mantiki ya kiuchumi inayoongoza sheria za kimataifa siyo mantiki inayoongoza mikakati ya uchumi wetu. Ni muhimu kufahamu hili kabla ya hatua kuchukua hatua muhimu za kiuwekezaji.

 1. Itasaidia kunufaisha nchi zaidi ya mapato tu kwenye hatua za kuzifanya rasilimali zetu za asili kuwa za kiuchumi.p

Nne, ni kubadili mifumo yetu ya kiutawala itakayotoa nguvu zaidi kwa wananchi juu ya uchumi wao.

Tano, kubadili aina ya siasa zinazotufanya kuwa na ushirikiano wa kijima(primitive solidarity) kutegemeana na upande, hata kama ushirikiano huo unasigina hatma njema ya taifa letu.

Mheshimiwa rais, kama nilivyotangulia kusema; huu ni mchango wangu tu juu ya jinsi tunavyoweza kubadili mistari tunayotumia kufikiri hatma ya uchumi wetu. Nafahamu kuwa, siyo lazima hoja hizi zichukuliwe, lakini naamini unaweza, ikukupendeza mheshimiwa rais, kutazama upya mambo haya kwenye uchumi wetu.

Mheshimiwa rais, kama asemavyo mchumi Thomas Sowell, kuwa; matatizo mengi ya leo kwenye mifumo ya uchumi, ni matokeo ya suluhu zilizotafakariwa vibaya Jana.

Mheshimiwa rais, nakutakia kila jema, kwenye kuongoza tafakari sahihi za suluhu ya matatizo yetu ya kiuchumi leo, yatakayo kuwa na matokeo mazuri na salama kesho.

Mwandishi wa uchambuzi huu ni mtaalamu mbobezi katika uchumi, mkurufunzi wa vyuo vikuu, na mshauri wa masuala ya uchumi kwa taasisi za kimataifa na serikali kadhaa za Afrika Mashariki.

Like