KATORO WAPIGA KURA KUKATAA MKATABA WA BANDARI

– Wasema: “hatutaki bandari zetu ziuzwe”
– Mbowe awaongoza kufanya uamuzi wa wazi

WANANCHI wa mji wa Katoro, Jimbo la Busanda, mkoani Geita, wameukataa mkataba baina ya serikali ya Tanzania na Dubai, unaohusu uendelezaji wa bandari za Tanzania na maeneo mengine mahsusi ya kiuchumi, yaliyowekwa chini ya kampuni ya DP World, ya Dubai.

Hatua hiyo ilifuatia hotuba ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, aliyefanya uchambuzi wa vifungu vya mkataba huo na kueleza kuwa vinahatarisha maslahi ya Taifa.

Mbowe aliwaongoza wananchi hao kupiga kura ya wazi, huku akiwauliza kuhusu mkataba huo ambapo maelfu ya wananchi waliofurika kwenye mkutano huo, kila mmoja akipunga mkono wake juu, walijibu:

*”hatutaki bandari zetu ziuzwe…”

Awali, akichambua hali ya maendeleo, Mbowe alisema CCM imeshindwa kuwaletea maendeleo watu wa Katoro, licha ya jimbo la Busanda kuwa na utajiri mkubwa wa dhahabu, kilimo cha pamba na kuwa jirani kabisa na ziwa Victoria.

Alisema Chadema itaibadilisha Katoro na Tanzania kwa ujumla kwa kutekeleza sera bora zinazozingatia haki na fursa sawa kwa kila mwananchi, uhuru, demokrasia na maendeleo ya watu.

Baada ya Kagera, mikutano ya Chadema ya Operesheni +255 kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria (Kagera, Geita na Mwanza) imeingia leo katika mkoa wa Geita kwa kuanzia na jimbo la Busanda.

Like